Ghana: Mkuu wa Mkoa, Kofi Opoku-Manu, Anapoteza Umaarufu?

Mkuu wa Mkoa wa Ashanti, Kofi Opoku-Manu, hivi karibuni alionja joto ya jiwe kutokana na matamshi aliyoyatoa kwenye hotuba yake kwa mashabiki wa chama tawala, Nationa Democratic Congress (NDC) tarehe 6 Januari.

Kwa mujibu wa Ato-Kwemena Dadzie, Opoku-Manu “aliwasihi mashabiki wa chama kutumia ghasia kusuluhisha tofauti zao.”

Dadzie anataarifu kwenye makala yake “Opoku-Manu Lazima Ang’oke” kwa nukuu ya moja kwa moja kutoka kwa Mkuu huyu wa Mkoa:

Kama unaweza kumpiga kofi, fanya hivyo.

Dadzie anaeleza:

Maoni kama haya hayana maana na ni ya kipuuzi. Huwezi kutegemea mtu aliye kwenye nafasi ya Bw. Opoku-Manu kuropoka maneno hayo. Lakini ndivyo alivyofanya.

Siku mbili baadaye, hakuwa na kumbukumbu ya kile alichosema mpaka rekodi ya sauti ilipochezwa mbele yake. Hapo ndipo aliporudi kwenye fahamu zake, akakubali ujinga wake na kuomba radhi, hatua ambayo ilikuja baada ya baadhi ya watu wenye nguvu kubwa ndani ya serikali kumwelekeza asafishe uchafu alioutengeneza.

Hili hapa chini ni tamko la kuomba radhi kama lilivyonukuliwana Dadzie:

Nitakuwa mtu wa mwisho kupendelea vita ya namna yoyote na baada ya kusikiliza (sauti hii) mwenyewe, ni lazima niseme najisikia kusikitika sana.

Dadzie anakatiza na maoni yafuatayo:

Lakini hakuishia hapo. Alitoa hoja za kujitetea kwa njia ya mzunguko. Anasema alikuwa anazungumza katika “mazingira ya hasira”, hiyo ikimaanisha kwamba hakuwa anatumia kichwa chake. Alikuwa akizungumza kwa moyo. Ungeweza kusema alikuwa akitoa mashuzi kwa mdomo wake.

Kwa kule kuufungua mdomo wake kwa upana na kutapika upuuzi wa hatari kama huo, Bw. Opoku-Manu amejionyesha mwenyewe kuwa mtu asiyewajibika ambaye hastahili kukalia nafasi aliyonayo. Ni lazima afukuzwe kazi. Na kama kuna mtu anayestahili kuzabwa kibao ni yeye. Kuomba radhi kwa moyo ulio nusu nusu alikokufanya baada ya kuelekezwa kufanya hivyo hakutoshi.

Ni lazima atoke.

Mwitikio wa wasomaji kwa maoni ya Opoku-Manu yanaonekana kuwa hasi zaidi.

David S. aliacha maoni kwenye posti ya blogu ya Dadzie:

Katika wakati ambao demokrasia ya Ghana ipo katika uchanga wake, kitu cha mwisho tunachohitaji ni mtu kushabikia ghasia za siasa. Hakuna anayetaka nchi hii iwe kama Zimbabwe au Iran. Ni lazima alazimishwe kujiuzulu kwa kuwataka watu kuharibu demokrasia yetu kwa vurugu za kisiasa. Ni adui wa demokrasia.

Banske alisema haya kuhusu posti hiyo hiyo.

Ninashangaa kwa nini watu wanataka afukuzwe kazi –kufukuzwa hakutatui tatizo. Kama Ohene Ntow angetoa tamko hilo, pangetokea nini? Kama Wereko-Brobby, Jake nk wangetoa matamshi kama hayo…BNI/Usalama wa taifa wangefanya nini? Na watu wanajidanganya kwamba Mills ana ubinadamu. Kumng’oa (Opoku-Manu) hakungesimamisha amri aliyoitoa na ile inayofanana na yake iliyotolewa na wafuasi wa Rawling, Vanderpuyes, Anyidoho nk. Kumng’oa (Opoku) kama Mkuu wa Mkoa na kumleta kwenye Uraisi? Mtu huyu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa RCC chini ya NPP na hiyo haikumtosha.

Kama umezaliwa mjinga, unaweza kuwa na miaka 1000 na utaendelea kuwa mjinga na hicho ndicho OM amekithibitisha. Ni mjinga tu anayeona nafasi ya kuteuliwa kisiasa kama kazi ya kudumu. Upuuzi unaweza kutafsiriwa kama kuona uteuzi wa kisiasa kama suala la kufa na kupona. Pamoja na hayo Mills ni mjinga, mpole na asiye na nguvu na kwa hiyo hajasikia wala kuona chochote.

Nana Poku aliandika kwenye makala yake katika Modern Ghana, ”Opoku-Manu lazima aondoke, awe kaomba msamaha au la”:

Mantiki ya muhimu zaidi ni hii: anawezaje kuwahakikishia haki wapinzani wake wa kisiasa? Wanawezaje kumwamini kuwa mwamuzi mwaminifu ikitokea suala lolote la machafuko ya kisiasa likaletwa kwake kama Mwenyekiti wa REGSEC? Anahakikisha vipi usalama na ulinzi wa watu hao hao anaotaka wapigwe?

Ninaamini amepoteza heshima inayotakiwa kwa nafasi ya Mkuu wa Mkoa. Ni lazima ajiuzulu au alazimishwe kufanya hivyo. Wote tumekuwa mashahidi wa matukio mengi ya kutishwa na kubughudhiwa kwa wanasiasa wa upinzani wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2008. Jambo la mwisho tunalolihitaji katika nchi hii ni maafisa, ambao kimsingi wangepaswa kujua zaidi, wawe wachuuzi ghasia na vitisho,

Tamko kwa vyombo vya habari lililotolewa na Chama cha Kukuza Demokrasia (AAD), kikundi chenye kutafuta ukuzaji wa Demokrasia ya Ghana, lililotundikwa na MyJoyOnline linasema:

AAD ingependa kumlaani Mkuu wa Mkoa wa Ashanti Mhe. Opoku-Manu kwa maoni yake yenye kinyaa na ya hovyo aliyoyatoa mwishoni mwa juma; yenye mwelekeo wa kuvuruga amani na usalama wa taifa hili.

AAD vile vile inauona wito wa Chama cha NPP kujiuzulu na kukaribishwa na wakala wa Ulinzi kwenye suala hilohilo kama wa kusikitisha na wa kinafiki. AAD inaamini kwamba, yule atafutaye usawa lazima aje na mikono iliyosafi na kwamba udhaifu wa chama cha NPP wa kushindwa kulaani vitendo vya vurugu vya Mkuu wa Mkoa wa Kati –Mhe. Edumadzie, na maoni kama hayo hayo ya Mhe. MaxwellKofi Jumah, Mhe. Mike Ocquaye, Dk. Nyaho, Tamakloe , nk kama yanayomomonyoa maadili na mwishowe kuharibu nia njema yoyote ya kusimika utawala wa sheria na kuimarisha amani na usalama nchini Ghana.

AAD inaamini kwamba kuomba radhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ashanti ni dalili za ukuaji wa dhana ya kuwajibika na lazima ikubaliwe kwa imani njema lakini hata hivyo tunasisitiza kwamba matamshi yake hayo yameidhalilisha hadhi yake kama Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Mkoa. Kwa hiyo tuna maoni yenye msisitizo kwamba ni lazima ajiuzulu kwa heshima au Rais lazima atambue ni muhimu kumng’oa kutoka kwenye ofisi yake. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008, Rais alitangazwa kuwa mtu wa amani (“asomdwehene”) na lazima kwa hiyo ajitoe mhanga katika kufanya kazi na maafisa wa umma na wateule wao wanaoakisi tabia na kanuni zake.

Sonia aliacha maoni kujibu taarifa ya AAD kwa vyombo vya habari:

Nimefuatlia harakati za AAD na nimehitimisha kwamba mwelekeo wao wa msimamo na uelewa katika masuala ya kitaifa lazima yaungwe mkono na Waghana wote wenye nia njema. Ninatamani AFAG na makundi yote ya kushinikiza wajifunze kutoka kwenye vichwa makini nyuma ya AAD. Ninaamini katika mantiki kwamba yeye atafutaye usawa lazima aje kwa mikono safi. Na NPP lazima iwe imara kujilaani wao wenyewe vinginevyo hawatachukuliwa kama watu makini.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.