Slovakia, Hungaria: Heri ya Mwaka Mpya!

Uhusiano kati ya nchi mbili jirani za Slovakia na Hungaria ulianza kutetereka katika mwaka uliopita, hasa kwa sababu ya kile kinachoitwa “sheria ya lugha” iliyoanzishwa huko Slovakia. Raia wa Hungaria na Slovakia walijikuta wakishuhudia wanasiasa wao wakianza hata kuhusisha taasisi ya Jumuiya ya Ulaya, yaani, Shirika la Usalama na Ushirikaiano la Ulaya, kwa kifupi OSCE, katika mivutano hiyo.

Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2009, raia wa Hungaria na wale wa Slovakia walianzisha kampeni ya mtandaoni ambayo ilikuja kupata sura yake maridhawa mwezi Januari 2010. Kikundi cha Facebook kinachojulikana kama Wa-Hungaria na Wa-Slovakia (HUN, SLO,ENG) tayari kimeanzishwa “Kwa lengo la kuweka uhusiano mzuri kati ya Wa-Hungaria na Wa-Slovakia!”, na sasa wanaunga mkono kundi jipya linalojulikana kama Štastný nový rok, Slovensko! / Boldog Új Évet Magyarország! (SLO, HUN, “Heri ya Mwaka Mpya, Slovakia!/Heri ya Mwaka Mpya, Hungaria!).

Maelezo ya kundi hilo – ambalo kila mara linaingiza mambo mapya kwenye ukurasa wake kwa lugha za KiSlovak na KiHungaria – yanaeleza (HUN, SLO):

Je, ni nani anayependa kuishi katika mvutano usiokoma na jirani yake? Hivi ni sababu gani hasa ya kufanya mtu utafute makosa ya mwenzako, na ni kwa jinsi gani inavyoudhi kama kuna mtu anayejaribu kutafuta makosa yetu saa zote?!

Hali ya upinzani inazidi kuwa tete, na ili kupunguza mvutano unaotokana na hali hiyo, tunaanzisha mawasiliano yanayolenga jamii, kwa sababu tunaamini kwamba mvutano huo zaidi unachagizwa na siasa tu.

Tunakiri kwamba katika kupitishiana hukumu, vyama vya kiraia katika nchi hizi mbili vinaweza kuambukizwa kwa njia iliyo ya chanya kwa msaada wa kampeni zinazohusisha pande mbili.
[…]

Lengo kuu la kampeni hii ni kusambaza ujumbe rahisi wa Mwaka Mpya katika nchi zote mbili kupitia njia zote za mawasiliano na kuhusisha pia Asasi Zisizo za Serikali (AZISE) na raia wa kawaida katika kutakiana Heri ya Mwaka Mpya. Kwa ajili ya lengo hili zilianzishwa tovuti mbili kwa ajili ya waungaji mkono Wa-Hungaria na Wa-Slovakia: boldogujevetmagyarorszag.sk ambayo ni tovuti ya Ki-Hungaria inayoishia na .sk, ambayo ni kodi ya nchi ya Slovakia, na stastnynovyrokslovensko.hu ambayo ni kwa ajili ya watu wanaozungumza Ki-Slovak huku ikiwekewa kodi ya nchi ya Hungaria. Vilevile, kuna video mbili zilizorekodiwa kwa ajili ya kila nchi:

Mpaka sasa, ReTRo ndiye mwanablogu pekee aliyekwishatoa maoni ya kuanzia katika lugha ya Ki-Hungaria kwa kuandika hadithi fupi (HUN) kuhusu majirani waliochukiana, lakini ambao uhusiano wao baadaye ulianza kuwa mzuri kwa sababu kuna theluji iliyoondoshwa kwa nasibu tu kutoka katika baraza la nyumba ya jirani mmojawapo anayechukiwa.

Huenda alikuwa hajaamka bado, au labda ile theluji ilifunika tu ile chuki yake, au labda aliipuuzia,lakini hakugundua kwamba siyo kuwa alikuwa amesukumizia theluji mbele ya lango la jirani yake, bali aliiondoa kabisa kutoka hapo. Aliamua kujiambia kwamba basi hilo lilikuwa ni tendo moja jema katika wiki hiyo. Alieleza jambo hili kwa Sanyi, mkewe, ambaye alimkemea na kumwambia kwamba alikuwa mpumbavu kwa kufanya kazi katika sehemu ya jirani waliyemchukia.

Walipofika nyumbani jioni ile, walikuta ndiyo kwanza theluji imeondolewa kutoka kwenye lango la kuingilia nyumbani kwao. Kumbe ilikuwa ni shukrani kutoka kwa jirani yao. Hali iliendelea hivyo kwa muda wa siku tatu. Kwanza walikutana siku ya Jumamosi. Kila mmoja akiwa na sepeto ya kusombea theluji. Walisalimiana. Walianza kuzungumza…

Ilipofika Jumatatu theluji ilikuwa imekwishayeyuka. Kuna kitu kilikuwa kimefika mwisho…

… au ndiyo kilikuwa kimeanza.

[…]

Ndiyo, kuna jambo limezinduliwa nalo linaitwa „Boldog Új Évet Magyarország! – Štastný Nový rok, Slovensko!”. Kumbe tunaweza kuanza na kuzoleana theluji…au siyo?

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.