Siku ya Januari 18 Global Voices itazindua Mtandao wa Teknolojia na Uwazi, ambao ni utafiti wa pamoja wa kuorodhesha na kuiweka kwenye ramani miradi ya kwenye mtandao wa intaneti ambayo inatangaza na kutetea uwazi, uwajibikaji wa serikali, na makutano ya kijamii. Hii ni ya kwanza kabisa katika mfululizo wa makala ambazo zitavinjari mada zinazohusiana kwa kupitia macho ya wanablogu duniani kote. Kwa kuanza tunaangalia jinsi wanablogu walivyoitikia Siku ya Kimataifa Dhidi ya Rushwa, ambayo ilitiwa saini kuwa sheria mwaka 2003 kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa na huadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Disemba.
Katika Sehemu ya Uwazi, blogu rasmi ya Transparency International, Georg Neumann anaangalia hali ya uanaharakati dhidi ya rushwa kwa mwaka 2009:
Wanaharakati dhidi ya rushwa wamekuwa katika mstari wa mashambulizi. Wanahabari wanaoandika kuhusu ufisadi kwenye siasa na jamii kama vile Lasantha Wickramatunga wa Sri Lanka waliyatoa maisha yao mwanzoni mwa mwaka huu. Wanaharakati kutoka Bosnia na Herzegovina, Burundi, Guatemala au Zimbabwe wamekabiliana na vitisho au wamenyamazishwa. Siku ya Kupinga Rushwa inasimama kama siku ya kuwambuka, kuwatambua na kuwaenzi watu hawa majasiri na wasio na woga, ambao walikwenda jela au walipoteza maisha yao wakiamini kuwa kwa kupigana dhidi ya rushwa wataifanya dunia kuwa bora.
Neumann pia anabaini kuwa mwaka 2009 pia ulishuhudia kupitishwa kwa vigezo vya kupima vyenye kasoro ambavyo havizitaki nchi wanachama kupata mapendekezo kutoka kwa Asasi huru Zisizo za Kiserikali zenye makao ndani ya nchi wanachama. Katika video ya dakika tano ya YouTube Peter Eigen, mwanzilishi wa Transparency International, anaeleza jukumu muhimu la jamii za kiraia katika kupigana na rushwa na kuboresha utawala:
Lakini mwaka 2009 haukuwa na habari mbaya pekee, anaandika Neumann. Hivi sasa kuna Vituo 40 vya Utetezi na Ushauri wa Kisheria duniani vinavyotoa ushauri wa sheria kwa waathirika na rushwa. Pia, uanahabari wa kijamii mtandaoni umejidhihirisha kuwa chombo chenye nguvu katika kutangaza uwazi na kupigana dhidi ya rushwa. Nchini India, kwa mfano, J.N. Jayashree alianzisha ukurasa shirikishi ili kumlinda mume wake ambaye usalama wake ulikuwa hatarini kutokana na vitendo vyake vya kufichua siri. Nchini Morocco mwanaharakati asiye na jina ameanza kutuma video za maaskari wanaopokea rushwa kwenye YouTube.
Katika Global Voices makala kadhaa ziliadhimisha Siku ya Kupinga Rushwa mwezi uliopita. Bhumika Ghimire anaandika kuwa Nepal iliorodheshwa na Tansparency International kama moja ya nchi zenye ufisadi zaidi duniani. Akiwa na viungo vya wanablogu wengine wa Nepal, makala ya Bhumika inaonyesha jinsi rushwa inavyoathiri uchumi, utawala, utumishi wa umma, na hata ndoa katika Nepal.
Huko Brazil ghasia zilizuka katika siku ya Kupinga Rushwa kati ya polisi na waandamanaji:
Waandamanaji wamekuwa wakidai kuondolewa madarakani kwa Gavana wa Wilaya ya Kitaifa, Jose Roberto Arruda, na makamu wake, Paulo Octavio, pamoja na uchunguzi wa kina wa pande zote zilizotajwa katika kesi ya hongo ambayo ilipelekea operesheni ya polisi iliyopewa jina la Kasha la Pandora. Kwa mujibu wa uchunguzi, Gavana Arruda anawezekana akawa ndiye kiongozi wa mpango wa rushwa wa R$ 600,000 (Takriban dola za Kimarekani 340,000 ) kwa mwezi ambao umewanufaisha wabunge, wafanyabiashara na maofisa wa serikali.
Lakini pia kuna sababu ya matumaini katika Brazil kwani inapokuja kwenye uwazi na utawala wazi, kama alivyoeleza Paula Goes wiki moja kabla ya Siku ya Kupinga Rushwa Duniani:
Kambi ya kwanza ya Siku ya Kuvamia Kompyuta kwa Ajili ya Uwazi [Transparencia Hackday] “siku mbili za kuvamia kompyuta za siasa za Brazil”, ilifunguliwa mwanzoni mwa mwezi Oktoba mjini Sao Paulo, na kambi ya mwisho iliendeshwa wiki hii, mnamo Disemba 1 na 2 katika mji mkuu wa Brasilia [pt]. Matukio haya yaliandaliwa na wanahabari Daniela Silva na Pedro Markun [pt], ni matukio yenye kiingilio bure na yanatoa fursa kwa watengeneza programu za kompyuta, wanahabari na watafiti kukutana pamoja na kutafuta njia za “kukomba’ taarifa kutoka kwenye tovuti rasmi za ofisi na kutengeneza applications ambazo zitaweza kuleta uwazi na ushiriki kwenye mchakato wa siasa.
Wahariri wa Global Voices pia wanawaelekeza wasomaji wao zilipo makala zinazohusiana na uwazi, rushwa na uwajibikaji serikalini katika ulimwengu wa blogu. Peter Marton anaangalia athari mbaya ya rushwa katika kuijenga tena Afghanistan. Wakati huo huo huko Ukraine, Petro anawapongeza wakazi wa Kabul kwa kumhukumu meya wao mika minne jela kwa kosa la rushwa na wanafikiria ni kwa haraka kiasi gani magereza ya Kyiv yatajaa ikiwa sheria hizo hizo zingefuatiliwa katika nchi yake. Akiandika katika tovuti ya Registan.net, Alexander Visotsky anaangalia mashtaka ya rushwa dhidi ya Mukhtar Dzhakishev yaliyotokana na uuzaji wa madini ya Uranium kinyume cha sheria na kuhitimisha, “Vita dhini ya rushwa nchini Kazakhstan ni mchezo wa kisiasa zaidi ya jitihada za kuing’oa rushwa.” Akiandika kutoka Japan Scilla Alecci anaonyesha kesi kumi mbaya zaidi za Transparency International nchini Japan. Na mwisho, akiandika kutokea Kisiwa cha Karibea cha Puerto Rco, “Gil the jenius” anaomba adhabu kali zaidi dhidi ya maofisa wa serikali wanaoshtakiwa dhidi ya rushwa.
Tukiangalia nyuma katika uanaharakati dhidi ya rushwa katika mwaka 2009 tunaona kuwa utamaduni wa rushwa bado umeenea duniani kote. Lakini pia tunauona mjadala wa mtandaoni unaokua juu ya nini kinachoweza kufanywa kuzuia rushwa, kutangaza uwazi na kuongeza makabiliano ya kijamii. Katika makala zitakazofuata baadaye tutaangalia zaidi na hasa majadiliano ya mtandaoni pamoja na miradi ya kwenye intaneti inayotangaza uwazi na kupigana dhidi ya rushwa nchini Naijeria na China.