Philippines: “Muswada wa Mkataba wa Ndoa Jadidifu”

Kikundi kimoja cha masuala maalum ya jamii nchini Philippines kinataka kuwasilisha sheria ambayo itaufanya mkataba wa ndoa kuwa na nguvu kwa miaka kumi tu. Pendekezo hili la kipekee ni jibu la kutatua tatizo la utaratibu mrefu na wa gharama wa kubatilisha ndoa. Nchi hii yenye Wakatoliki wengi haina sheria ya talaka.

Kwa mujibu wa kikundi hicho, “Muswada wa Ndoa Jadidifu” utawakinga wanandoa wasioelewana dhidi ya gharama zinazoambatana na utaratibu mrefu wa kisheria kabla ndoa zao hazijabatilishwa.” Kikundi hicho kiliongeza kuwa mkataba wa ndoa “unatakiwa uwe kama pasi ya kusafiria au leseni ya kuendesha gari. Ikiwa hatuna haja ya kuongeza muda wake, basi (mkataba huo) unapoteza nguvu yake.”

Zaidi ya ndoa 500,000 husimamiwa na Kanisa Katoliki kila mwaka wakati ndoa zinazobatilishwa na kuripotiwa ni pungufu ya asilimia 10.

Kama ilivyotarajiwa, muswada huo wa ndoa uliopendekezwa ambao una muda wa kuwa na nguvu kisheria umezua mijadala katika ulimwengu wa blogu.

Akiandika kwa ajili ya Lex Fori Philippines, Oscar anasisitiza athari za pendekezo hili kwenye uhusiano wa mali.

Ikiwa tutalinganisha ndoa na leseni ya gari, je tunaweza kumchukua mwanandoa mtarajiwa ili kumjaribu kwanza? Kwa njia hiyo, watu hao wawili wataepuka kupitia adha ya kujadidisha au kutojadidisha leseni yao ya ndoa inayokwisha muda wake na kuokoa fedha ambazo huandaa shughuli aghali ya harusi.

Tuchukulie kuwa ndoa itakwisha muda wake baada ya miaka kumi, ni nini kitachotokea kwenye uhusiano wa mali baada ya miaka 10? Uhalali wa mikataba ambayo wanandoa waliingia pamoja? Je mali hizo zitataifishwa, mikataba itasitishwa, na kuwaambia watoto wategemee muda mchache na wazazi wao ikiwa wazazi wote watafunga ndoa tena na kupata watoto wengine?

John Odonnell R. Petalcorin anapendelea muswada ambao utapunguza gharama za kesi za kubatilisha ndoa.

… kama pendekezo hili lilianza kufikiriwa kwa sababu ya gharama kubwa za kesi za kubatilisha ndoa, basi ningependekeza muswada wa kupinga ili kuweka kikomo cha gharama za kubatilisha. Ili kuufanya mchakato uwe wa haraka, tunaweza pia kujumuisha kipengele kinachosema kuwa kubatilisha kunaweza kupitishwa mara moja ikiwa wote, mume na mke, watabadilishana kwa mdomo ahadi za kukana mapenzi kwa mwingine mara tatu

Ice9web Blog anajiuliza kama watu watatoa ahadi mpya ya ndoa kwenye sherehe za harusi.

Ikiwa itatokea, basi siku za ahadi za ndoa kupewa umuhimu unaostahili “Mpaka kifo kitakapotutenganisha” zimepita?
Sasa ahadi hiyo itakuwaje? Mpaka mwisho wa mkataba utakapotutenganisha?

Wengine wanasema kuwa hilo ndilo jibu hapa Philippines ambako hatuna talaka na kubatilisha ndoa kunachukua muda na pesa nyingi… je ujadidishaji ndiyo jibu la kweli?

Pinoy Politico haelewi kwa nini wanandoa wasioelewana wasubiri mpaka miaka kumi ipite kabla ya kufuta ndoa yao

Sielewi kwa nini mtu asubiri kwa muongo ili amtose mke wake anayetembea nje. Hii ni kwa wanawake pia. Ikiwa mume wangu ananipiga kila siku baada ya mwaka 1 wa ndoa, kwa nini nisubiri miaka mingine 9? Pengine mngependekeza kujadidisha ndoa kila siku ili kwamba mfuatilie hali ya ndoa yao.

Capt. Nemo anaunga mkono pendekezo hilo

Naam pendekezo hili linataka kutatua hali YA SASA ambayo wanandoa wengi wa Kifilipino wanakabiliwa nayo siku hizi. Kutokana na mtazamo wangu, jambo hili ni bora na ni suluhisho ambalo linawatendea sawa watu wa jinsia zote mbili kuhusiana na ndoa. Kwani ubatilishwaji wa ndoa unaweza kufanywa na wale wenye uwezo wa “kulipia” utaratibu mzima. Vipi kuhusu maskini ambao wanataka kusitisha uhusiano wao usiofanya kazi, wanaweza kufuata utaratibu huo huo?

Pendekezo hili litawahamasisha wanandoa kuthamini uhusiano wao uliopo. Kwa kweli, wana UTASHI HURU wa ama kujadidisha mkataba wao wa ndoa au kuitupa hiyo karatasi baada ya miaka 10.

Jappysworld ana hofu juu ya ustawi wa watoto ikiwa wanandoa wataamua kutojadidisha ndoa yao

Hili sio suluhisho. Sielewi ni vipi kuna watu wengi ambao hawawezi kuwa kwenye ndoa hata kwa dakika moja zaidi, je nini kitakachotokea kwa watoto wao ikiwa pendekezo hili litafanya kazi. Linaweza kuwa na manufaa kwa wapenzi waliotengana lakini watoto wao ndio watakaoteseka zaidi. Ni sawa na kusema katika siku ya kwanza ya kuadhimisha miaka 10 ya ndoa; mtu aliye kwenye ndoa anaweza kufanya chochote atakacho bila ya kujali wajibu wao na na uaminifu kwa familia zao.

Maureen Flores anaamini kuwa muswada uliopendekezwa unauzunguka utakatifu wa ndoa

Hili limekuwa suala la kuchekesha kati ya mume wangu na mimi kwa wiki nzima. Tunasherehekea maadhimisho ya miaka 10 ya ndoa yetu leo, unaona. Lakini kweli, pendekezo la mkataba wa ndoa unaoisha nguvu baada ya miaka 10 halichekeshi.

Na pia ninaeleza kutokukubaliana kwangu kwa dhati juu ya pendekezo hili. Nina hofu na vile litakavyoathiri familia na jamii yetu ikiwa litapitishwa. Utakatifu wa ndoa unaepukwa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.