Marekani: Raia wa Haiti Wapatiwa Hadhi ya Hifadhi ya Muda

Hadhi ya Hifadhi ya Muda (inayojulikana kama TPS) ni hadhi maalumu inayotolewa na Marekani kwa raia wa kigeni wanaotoka katika nchi fulanifulani ambamo kunakuwa kumetokea aina fulani ya janga au pigo la karibuni, kama vile vita au tetemeko la ardhi. Hadhi hiyo inamtaka mtu anayenufaika nayo awe tayari kwenye ardhi ya Marekani, na mtu hana budi kutuma maombi ya kuomba kupata hifadhi hiyo na maombi yatafikiriwa. Mpaka sasa hifadhi ya aina hii imekwishatolewa kwa raia wa nchi za El Salvador, Honduras, Nicaragua, Somali na Sudani. Kama inavyooneshwa na muda wa hifadhi hiyo, utaratibu huo ni jambo la muda tu na haiwezi kubadilika kumfanya mtu awe na sifa za kupata ukaazi wa kudumu (kupitia mpango wa Kadi ya Kijani) au hata kuwa raia wa Marekani.

Juma hili, kufuatia tetemeko baya lililofikia kipimo cha 7.0 ambalo liliikumba nchi ya Haiti, wanasiasa na waandishi wa habari kadhaa waliitaka Marekani kuwapa hifadhi ya aina hiyo raia wa Haiti wapatao milioni moja au mbili (kwa makisio ya juu) ili waweze kuishi katika nchi hiyo bila bugudha. Majaribio kadhaa ya kushawishi uwezekano huo, likiwemo lililofanywa na breakthrough, yalitumwa huku na huko, na wajumbe 83 wa Baraza la Kongresi walitia saini barua iliyotumwa kwa Rais Obama kuomba raia wa Haiti wapewe hadhi hiyo ya hifadhi ya muda.

Ilipotika Ijumaa tarehe 15 January, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Janet Napolitano, alitoa ruhusa ya raia wa Haiti wanaoishi Marekani hivi sasa kupewa TPS kwa kipindi cha miezi 18.

Kabla ya tangazo hilo, mwanablogu The Latin Americanist alitoa maoni haya:

Wataalamu kuhusu nchi ya Haiti na watetezi wa masuala ya uhamiaji kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakihimiza kwamba ruhusu itolewe ili raia wa Haiti wapate hadhi ya TPS hasa kwa kuzingatia majanga ya vimbunga na dhoruba nyingine ambazo zimekuwa zikiipiga nchi hiyo katika muongo uliopita. Ingawa maombi yao hayo yameangukia katika masikio kiziwi ya watawala wa awamu zote mbili za Bush na Obama, utetezi wa upewaji TPS kwa raia wa Haiti umepata uungaji mkono wa watunga sheria muhimu.

Vilevile, kabla ya uamuzi huo, mwanablogu wa Kimarekani na mtaalamu wa masuala ya uhamiaji, Koulflo Memo, alibainisha kwamba TPS “si kihitaji akili””

Mrengo wa kulia wa Shirikisho la Mageuzi ya Mfumo wa Uhamiaji Marekani (Federation for American Immigration Reform (FAIR)) umetangaza kupinga utolewaji wa TPS kwa raia wa nchi ya Haiti. Sababu wanayoitoa ni kwamba wanaamini kuwa mara baada ya kupita muda wa hadhi hiyo, raia wa Haiti hawatataka kurejea kwao. Wanasema pia kwamba hali iliyotokea nchini Haiti haikidhi vigezo vya mtu kupewa TPS. Ama kwa hakika upinzani huu unaotolewa na FAIR hautazami mambo kwa haki bali unatokana na kiburi tu. Vilevile una mwelekeo wa kibaguzi.

Natumaini Rais Obama hatumii jambo hili kupima fursa zake za kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa uhamiaji baadaye mwaka huu kwa kuwafurahisha FAIR kuhusu jambo hili lenye umuhimu wa pekee katika masuala ya kiutu. Kama hataitikia miito anayopewa ya kutoa ruhusa hiyo, basi atakuwa amewatupa mkono raia wa Haiti walio katika hali ya kuhitaji sana msaada.

Mwanablogu wa Kimarekani anayejulikana kama Deep Thought alitoa maoni kuhusu uamuzi wa utawala wa Rais Obama, aliandika akisema:

Rais Obama ameonyesha kuwa ni kiongozi makini baada ya kufanya uamuzi huo mzito kwa haraka ili kuwasaidia watu wa Haiti. Yeye na Waziri Napolitano pia walionyesha huruma kwa kusogeza mbele uondoshwaji kwa nguvu wa raia wa Haiti kutoka nchini Marekani kwa miezi kumi na nane baada ya kuwapa TPS raia wanaoishi nchini humo hivi sasa; kuwatupilia mbali baadhi ya watu katika kipindi hiki halitakuwa jambo lenye msaada, sana sana litakuwa na mwisho mbaya. Ndiyo, viongozi hawa wanapata upinzani mkali kutoka kwa vikundi vya kutetea wenyeji lakini kipimo cha kweli cha uongozi ni uwezo wa uongozi huo kufanya maamuzi magumu kwa sababu maamuzi hayo yako sahihi.

Mwanablogu na mzazi anayeasili all buttoned up waliungana na kumshukuru mwakilishi kwa kusaidi upatikanaji wa TPS na pia wanaomba kwamba msaada zaidi utolewe kwa mayatima wengi walio nchin Haiti, anaandika:

Jambo hili limekazaniwa sana kwenye vyombo vya habari hivi sasa. Natumaini kwamba juhudi hizo zitaleta matunda, lakini wewe na mimi tunajua kwamba watu wanachoka kuona huzuni ileile tena na tena. Kulikuwa na zaidi ya mayatima 200,000 walikokuwa wakiishi jijini Port-au-Prince kabla ya tukio hili la majuzi, na kwa vyovyote vile unavyoyachukulia mambo haya – na ni magumu – na hakuna hata uingiliaji kati mmoja unaopuuzia mshikamano wa watu wa Haiti au hamu yao ya kuwatunza watoto wao wenyewe. Imetokea tu kwamba kwa sasa hawawezi kufanya hivyo. Hili ni suala la kiutu.

Ingawa raia wa Haiti hivi sasa wana kinga kwa muda wa miezi 18 ijayo kwa uchache huku wa wakifanya kazi, bado Haidi inahitaji msaada. Hapa kuna baadhi ya asasi zinazotoa misaada nchini Haiti, na hapa kuna njia chache zinazokupa fursa ya kuchangia.

Tafadhali pitia Ukurasa wa Global Voices wa Tetemeko la Ardhi la Haiti kwa taarifa zaidi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.