Marekani: Dkt. Martin Luther King, Jr. Akumbukwa

Martin Luther King Jr. alizaliwa tarehe 15 Januari, 1929 na akawa mmoja wa wasemaji na watetezi wakuu wa Harakati za Haki za Kiraia huko Marekani. Nchini Marekani, anaenziwa kwa sikukuu ya taifa, inayoadhimishwa kila mwaka siku ya Jumatatu ya tatu ya mwezi Januari. Leo, wanablogu wengi nchini Marekani wanaadhimisha kumbukumbu yake kwa kuandika makala za kumuenzi, huku wakiungalisha urithi wake wa masuala ya haki za jamii na masuala ya leo, wakionyesha wazi kuwa miaka 42 baada ya kuuwawa kwa King, maneno yake bado yana maana.

The Color Line ni blogu inayotilia mkazo masuala ya elimu ya jamii kuhusu rangi za watu, asili za watu, na uhamiaji katika Marekani. Mwanablogu C.N. anauliza je ni kwa kiasi gani tu karibu na kutimiza ndoto ya Martin Luther King Jr.:

Wamarekani wengi walifikiri kuwa kuchaguliwa kwa Barack Obama kulikuwa ndio kilele cha kutimia kwa ndoto ya Dkt. King na uthibitisho madhubuti wa kuwa tumeendelea na kufikia kwenye jamii “baada-ya-ubaguzi,” jamii isiyoona rangi. Kwa bahati mbaya, kama mimi na wataalamu wa sayansi ya jamii pamoja na watoa maoni tulivyosema, hata katika mwaka huu uliopita, tumeona matukio kadhaa ambayo yanaonyesha kwa kiasi gani utofauti wa rangi na ubaguzi wa rangi bado uemeenea katika jamii ya Marekani.

Kufuatia mijadala na mifano mingi ya masuala ya rangi katika Marekani, mwanablogu huyo anahitimisha:

Hatimaye, njia yetu bora zaidi katika kufikia njozi ya kutoona rangi za wengine ni kwa kutambua, kukubali, na kuelewa kuwa utofauti wa rangi bado upo na kwamba ubaguzi huo bado ni msingi unaoendeleza ubaguzi na ukosefu wa usawa katika jamii ya Kimarekani leo. Ni kwa kufanya hivyo tutaweza kusonga mbele kufikia njozi ya mwisho ya Dkt. King – usawa wa kweli wa watu wa rangi zote.

Lova Rakotomalala wa Global Voices, Mmadagaska ambaye anaishi Marekani, aliandika makala yenye kichwa “Somo kutoka kwa Dkt. Martin Luther King, Jr kwa Madagaska,” ambayo kwayo alisema (akilinganisha na matukio ya mwaka jana nchini Madagaska):

Uongozi ni jambo muhimu. Viongozi wa kweli hutoa hotuba na hufuata kwa vitendo maneno yao, wakiwa mstari wa mbele. Viongozi huwa hawatokomei kivulini wakati wanapofahamu kuwa mambo yanakaribia kuwa ya hatari na kuwaacha waandamanaji waingie matatani ili kutimiza ajenda (za kiongozi).

Jambo pekee tunalojua kwa hakika kuhusu kile kilichotokea nchini Madagaska mwaka mmoja uliopita ni kuwa tungeliweza kumtumia mtu kama Dkt. King wakati ule.

Blogu iliyoko Marekani Immigration Impact iliweka sambamba mambo yanafanana kati ya harakati za haki za kiraia za miaka ya 1960 na uhamiaji wa leo, inaandika:

Hivi sasa, zaidi ya wakati mwingine wowote, ni muhimu kukumbuka ujumbe wa Dkt. King unaosema watu wote wanaumbwa sawa – sio tu kwa wale wenye asili ya Kihispania na Waafrika-Wamarekani, bali kwa watu wote wanaohamia katika nchi wakitafuta ile Ndoto ya Marekani.

Mwanablogu wa Preventing Homelessness anatukumbusha kuwa kumuenzi Martin Luther King, Jr. maana yake ni utumishi:

Leo ni siku ya Martin Luther King, Jr. Siku yetu ya kufanya kazi ili kuboresha maisha, kujenga madaraja kwenye vikwazo vya kijamii, na kuipeleka nchi yetu Karibu zaidi na “Jamii Pendwa” ambayo Dkt. King aliiota. Leo ni siku ya kutumikia, lakini hatupaswi kuishia hapo tu. Tunaweza kuazimia kuufanya mwaka huu kuwa mwaka wa kutumikia na hivyo kubadilisha hali kikweli katika jamii yetu!

Na mwisho lakini si kwa uchache, blogu inayopinga ubaguzi wa rangi, Racism Review inatuacha na wazo juu ya kusikiliza somo la King:

Katika siku hii ya Dkt. Martin Luther King, Jr., natumaini na kuomba kwamba tutajifunza masomo ambayo Dkt. King alitufundisha. Bila ya kujali watu wengi wanasema nini, kauli za Marekani ya uanaharakati wa maendeleo ziko maili nyingi mbele ya matendo (angalia mahubiri ya King “Waraka wa Paulo kwa Wakristu wa Marekani”) na utaona kuwa harakati za kufikia malengo pole pole siyo jibu. Harakati za pamoja, upinzani wa kijamii wa kibunifu na wa muda mrefu, uhamasishaji wa watu wa rangi na maskini – ambao kwao kuzama kwa njia ya maingiliano ndani ya jamii kubwa au kusitisha uhusiano kabisa na jamii kubwa si machaguo yanayowezekana – ndiyo njia pekee za kuweza kufikia na kudumisha mabadiliko ya kweli nay a kimfumo.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.