Kadiri watu katika sehemu mbalimbali za dunia wanavyozidi kuwa karibu kwa sababu ya teknolojia ya kisasa, na njinsi vikwazo vya kiutamaduni na tofauti ya asili vinavyozidi kuondolewa na kuacha nafasi kwa kuelewana na kuheshimiana; basi ndoa za watu wenye asili tofauti nazo zinazidi kuwa jambo la kawaida. Idadi kadhaa ya familia za watu waliocahanganyika kiasili na wa dini tofauti wanasimulia kuhusu uzoefu wao kupitia ulimwengu wa blogu. Kuuchunguza utamaduni na nchi kupitia macho ya mtu mgeni kunatoa fursa ya kujifunza mengi.
Katika blogu ya ndoa za watu wa asili tofauti, mwanaume wa Ki-Australia ambaye pia ni mwanablogu amemwoa mwanamke mwenye asili ya U-China ambaye pia si mwamini Mungu. Aliandika kuhusu jinsi walivyosherehekea sikukuu ya Noeli kama familia pamoja na mtoto wao, hapo anaeleza jinsi mara nyingine inavyomwia vigumu kujaribu kuelewa maoni ya mkewe kama mtu asiyeamini katika Mungu huku akishikilia matambiko fulani ya kiutamaduni ya Kichina.
“Inawezekana kwamba Bibie B haamini katika Mungu kwa sababu hakuna ushahidi wa kuthibitisha kuwepo kwake, lakini imani yake hii haimzuii kuamini katika Bahati, au imani ya Feng Shui, au katika Elimu-Namba, au katika vijiimani vyovyote vidogovidogo vingi ambavyo vinaelekea kwamba vimeenea sana miongoni mwa wanajamii wa Kichina.
Mara nyingine huwa ninamshuhudia Bibie B akifanya matambiko ya ajabu nyumbani yakiwa na lengo la kuondoa Bahati Mbaya, na hata ameshawahi kutugharimu kiasi kikubwa cha fedha ili kuijenga upya milango ya mbele na nyuma ya nyumba yetu ili kuweza kunasa Bahati Nzuri katika nyumba yetu kupitia miungu wazuri wa Feng Shui.
Mimi pia sioni kama kweli imani zake hizi zina maana yoyote, lakini ninazivumilia ili nisimwudhi Bibie B. Nafikiri naye ananichukulia hivyohivyo kutokana na imani yangu ya dini.”
Linapokuja suala la utamaduni wa kigeni, kujaribu kuelewa mafumbo si jambo jepesi, jinsi inavyoelekea; hiyo ni hata uwe umeoana na mtu anayetoka kwenye utamaduni huo. Lakini, je, unafanyaje pale unapojaribu kukumbatia taratibu za kiutamaduni za mwenzako na kuishia kuonekana tofauti miongoni wa wenzako?
Katika GoriGirl kuna mwanablogu, mwanamke mzungu aliyeolewa na Mhindi wa kutoka Bengali, yeye pia anatushirikisha uzoefu wake wa “kujipaka sindoor (doa la kwenye paji la uso) wakati yeye ni mwanamke wa kizungu”. Wanawake wa Ki-Hindu walioolewa hujipaka sindoor (aina fulani ya chokaa ya rangi) kwenye mapaji ya nyuso zao na ni jambo la kawaida katika maeneo mengi katika nchi za India na Nepali. Lakini je, utaratibu huo utakubalika katika jiji la Washington DC?
“Hapana, tatizo langu linalotokana na kujipaka sindoor ni kwamba katika siku nyingi ninakwenda kazini ambapo kuna idadi ya kutosha ya wanawake wa Ki-Hindi. Hakuna hata mmoja wao anayevalia mavazi ya asili ya Ki-Hindi, labda kwa kiasi kidogo vazi lile fupi la kurta – na kwa hakika karibu hakuna mwanamke aliyeolewa anayejipaka sindoor miongoni mwao! Mwanamke mmoja mtu mzima mfanyakazi mwenzangu mwenye asili ya Bengali hata alinishangaa kwa kuwa nilikuwa nafuata utamaduni “uliopitwa na wakati” wa kuvalia bangili ya loha – bangili iliyopakwa dhahabu ambayo hutumika kama pete wakati wa harusi miongoni mwa wanawake wa Ki-Bengali – katika mkono wangu wa kushoto kila siku.
…………Katika hatua nyingine (ndiyo, ndiyo, najua) mara ya mwisho nilipojipaka sindoor na kwenda ofisini, bosi wangu alitaka kujua kama nilihitaji kupewa bandeji ili nijifunge kidonda nilichokuwa nacho kichwani kwangu. Ndiyo, ni kweli kabisa, wala si utani, najua. Hivi, kuna mtu mwingine anayepata shida na hali hii?”
Kuonekana u tofauti lilikuwa pia jambo lililokuwa kwenye akili ya mwanablogu wa TheGoriWifeLife, yeye ni Mwamerika aliyeolewa na mwanamme wa Kipakistani. Anaandika kuhusu namna anavyovaa pale anapokwenda nchini Pakistani:
“Safari hii, nilibeba jozi mbili za nguo aina ya jeans na mashati kadhaa kwa sababu niliwaza kuwa ninapokuwa nyumbani basi napenda nijihisi kutobughudhiwa, maana hayo pia ndiyo mavazi yangu ya kila siku nyumbani kwetu. Lakini mara kadhaa niliishia kuvaa suruali ya jeans na juu shati la Kipakistani na dupatta hasa tunapotoka, huenda mara nyingi tu kadiri ambavyo nimewahi kuvaa nguo aina ya shalwar kameez. Hata tumefanya matembezi katika maeneo ya jirani mara kadhaa na linaonekana kuwa jambo la kawaida na wala halisumbui.
Lakini kwa sababu moja au nyingine safari hii hali imekuwa tofauti.”
Ugumu wa kuelewa na kukubalika katika utamaduni tofauti ni jambo ambalo wanandoa wenye asili tofauti hukutana nalo kila mara. Mara nyingine hujikuta pia wakikabiliana na maswali kuhusu msingi wa uhusiano wao, na pale inapotokea ndoa na masuala ya uhamiaji yakagongana, basi huwa ni karaha tupu.
Katika IndiaTies, mwanablogu Heather Lurdkee, Mwamerika aliyeolewa na Mhindi anawahoji watu wanaozitazama ndoa za watu wa asili tofauti kama alama ya hadhi au njia ya kupata sifa ya ukaazi wa kudumu.
“Kwa upande wa mume wangu, ile kunioa mimi (mwanamke wa kizungu) siyo njia ya kupanda hadhi – hakuamua kutafuta mwanamke wa Ki-Amerika au mzungu kwa ajili ya lengo hilo. Siyo kwamba “alinihitaji mimi” ili kufika mahali fulani katika maisha yake. Ilitokea tu kwamba tulikuwa mahali sahihi kwa muda sahihi na mambo yakajipa nasi tupo pamoja.
Hata hivyo, baadhi ya marafiki wa Ki-Hindi wa mume wangu wamemweleza nia zao za kutafuta wanawake wa kizungu. Mmoja wao (ambaye ametoka India kuja Marekani hivi karibuni) alimwambia mume wangu “Du, rafiki yangu wewe umepatia, na mimi ngoja nitafute mwanamke wa kizungu kama wewe…” Na siyo kwamba alikuwa anatania! “
Majaribu na mahangaiko ya watu waliooana huku wakiwa ni wa asili tofauti yaonyesha, kama kioo, ni kwa kiasi gani sisi – kama watu tuliostaarabika – tumefikia katika kupokea na kuheshimu tafauti zetu. Blogu hizi ni sehemu tu ya kioo hicho na pia ni zana ya kusaidia kuelewa tamaduni na jamii nyingine.