Haiti: Uenezaji Habari na Taarifa

Sisi tulio nje ya Haiti tunaweza tu kujenga picha kichwani kuhusu hali halisi ya maisha ya kila siku yalivyo huko baada ya tetemeko baya la ardhi – lakini katikati ya juhudi za kuwatafuta wapendwa ndugu, juhudi za kuwahudumia waliojeruhiwa na jukumu zito na gumu la kuwafikishia msaada wa kiutu wale wanaouhitaji zaidi – wanablogu walio huko Port-au-Prince na maeneo ya jirani wanawasiliana na ulimwengu wa nje, ambao nao unahangaika kutaka kupata taarifa kutoka kwa wale waliokuwa katika eneo lenyewe kabisa la janga.

Blogu-tovuti ya The Livesay [Haiti] imejitolea kwa moyo mmoja kutoa taarifa mpya za kila wakati kupitia makala zake, wakati ambapo Troy, mkuu wa kaya, akiandika kupitia Twita kila baada ya kitambo kifupi pamoja na kutuma picha kupitia kwenye mkondo wa picha wa flickr. Bwana Troy ambaye ni Mwamerika anayefanya kazi ya umisionari huko Haiti wala hafichi jinsi anavyohusudu umadhubuti wa watu wa Haiti:

Kiwango cha masumbuko ya sasa kilichosababishwa na tetemeko la ardhi si rahisi kufahamika hivi sasa…ni vigumu kukadiria idadi. Lakini, kama jinsi wanavyopambana na harakati za maisha za kipindi hiki za siku hadi siku ni kiashirio kwa namna yoyote – basi watu wa Haiti wataibuka upya.

Mkewe anayeitwa Tara naye kwa upande wake anatupatia taarifa za maana:

Mafuta ya diseli yatatumika sana na yatahitajika sana kwa aina yoyote ile ya mawasiliano.

Kama unakuja huku hauko tayari kujiweka katika hatari na kujichanganya katika kusafisha vidonda vya kutisha basi kutazidisha tu machungu kwa watu ambao tayari wana uchungu mkali. Wenye taaluma ya utabibu hawana budi kwasiliana na asasi zenye uwezo wa kuratibu juhudi mbalimbali za uokoaji ili waweze kuja hapa. Haitasaidia sana kwa watu wasio na taaluma ya utabibu kuja tu na kuongeza idadi ya watu wa kulisha na kuwapa mahali pa kulala. Naamini maneno haya hayatachukuliwa kuwa na maana mbaya – lakini huo ndiyo ukweli.

Ushuhuda na picha za kutisha pia ni vitu ambavyo vimekuwa vikimiminika kutoka kwenye tovuti ya wanawezaje kusikia (how can they hear):

Nilipokuwa nataka kutoka ndani, mara niliona meza ya kujipodolea ikitikisika, makabati ya jikoni yakitetemeka huku vitu vilivyo ndani vikidondoka chini, wakati huohuo nyumba ilikuwa ikichezacheza utadhani imetengenezwa kwa kitu laini mfano wa mafuta ya mgando. Sijawahi kamwe kushuhudia kitu cha aina hiyo. Nilikuja kutahamaki kwamba ni tetemeko la ardhi baada ya kuwa nimekwisha toka nje na kuona watu wakikimbia ovyo huku na huko. Wengine wao walikuwa wakipiga mayowe. Wengine wakikimbia mbio tu. Wengine wakiomboleza. Yaani walikuwa walikuwa wakilia kwa kuomboleza kana kwamba kulikuwa na mtu anayewakamua uhai wao.

Blogu hiyo pia imekuwa ikitoa taarifa za njia bora za kutoa msaada katika hali inayochanganya sana, ambayo, kwa kutumia mtazamo wa makala mpya zaidi kwenye blogu hiyo, hali inazidi kuwa mbaya:

Hali ya mambo hapa inazidi kuwa ya kutisha. Tunaona kwamba kiwango cha uharibifu katika eneo la Jacmel ni zaidi kuliko tulivyokadiria mwanzoni. Ndiyo kwanza nimegundua kwamba bado kuna mamia ya watu katika eneo hili la Jacmel ambao bado wamekwama kwenye vifusi. Unaweza kusikia harufu mbaya za maiti waliokufa katika eneo la katikati ya mji ambapo kulikuwa na uharibifu mkubwa zaidi.

Suala lingine ni lile la maji. Je, yatakatika hivi karibuni? Je, wapi pengine tutapata maji safi na salama? Sijui.

Kwa upande wao Pwoje Espwa – Matumaini katika Haiti nao wanablogu kueleza yale wanayoshuhudia.

Hospitali kuu hapa tayari yote imejaa watu waliojeruhiwa huko katika jiji. Kuna madaktari na manesi na si kingine. Hakuna dawa, mashuka, bendeji, na hakuna chakula cha kuwalisha. Wengine wao wanaendelea kuangamia huku wamejilaza kwenye sakafu. Tafadhali mtuombee sisi na wao.

Chapisho la karibuni kabisa kwenye blogu hiyo linazungumzia ukweli kwamba kampuni ya umeme ya “EdH (Electricite d'Haiti) hivi karibuni itaanzisha mgao wa umeme kwa kuwa kiwango cha mafuta kinazidi kupungua”:

Mpango uliopo ni kuwasha umeme nyakati za usiku wa ajili ya masuala ya usalama na kwa saa chache nyakati za mchana. Ni kituo kimoja tu cha mafuta ndiyo kilicho wazi kwa wakati huu na baadhi ya watu wanabashiri kwamba huenda bei itapanda sana.

Nilikutana na mtu mtaani leo asubuhi na yeye alikuwa ametokea eneo la Jacmel ambalo lilipigwa vibaya na tetemeko. Alikuwa akiongea peke yake kwa lugha za Kreyle, Kifaransa na Kihispania huku akitumbukiza Kiingereza. Aliniongelesha, lakini sikuambulia kitu katika aliyosema. Mara ghafla aligeuka na kutokomea kwenye giza. Mtu anaposhuhudia uharibifu mkubwa kupita kiasi na upotevu mkubwa wa maisha kunaweza kumchanganya vibaya mtu yeyote.

katika blogu-tovuti ya Haiti, Familia ya Blesh nayo inatuma taarifa mbalimbali:

Hali ni ya kutisha. Masoko mengi yanayotegemewa kwa chakula yameporomoka. Mfumo wa mabenki haufanyi kazi sawasawa. Kuna huduma kiduchu sana za Intaneti na simu za mkononi.

Ili kukuelewesha upate picha ya hali ilivyo hapa…sijaweza kwenda sambamba na habari za nani anafanya nini lakini ninachoweza kukueleza ni kwamba Haiti iko katika hali mbaya. Miundombinu yote imeharibika.

Hata hivyo, kuwepo kwa huduma ya intaneti, japo kwa kiasi kidogo, katika mazingira magumu kama haya tuliyomo, bado ni kama muujiza fulani hivi mdogo – na kampuni ya Mulitilink ya hapa Haiti inayotoa huduma za intaneti (ISP) imechukua jukumu na kuanza kutuma Twita hivyo inatoa taarifa zinazohitajika sana na kurusha upya twita zinazoomba taarifa za watu waliopotezana.

Mmoja wa watu wanaotumia sana Twita ni mfanyakazi wa Hoteli, Richard Morse, ambaye taarifa zake za tukio zima zimekuwa makini sana.

Kwa upande mwingine, Changing Perspectives, ambaye anaandika makala kutoka nchi jira ya Dominika, anatuma ripoti kutokea katika misheni moja iliyo eneo la karibu na Jeremie huko Haiti:

Bado simu zetu hazifanyi kazi na hakuna jinsi ambayo mtu anaweza kuitumia ili kwenda jijini Port kuona kama ndugu zao wako salama au la, yaani hiyo ni hata kama watu wangetaka kwendahuko. Hakuna boti zinazokuja huku Jeremie na tumesikia kwamba barabara inayokwenda Cayes kupitia milimani imeharibika kiasi cha magari kutoweza kupita. Jambo hili lina maana kwamba watu hawawezi kwenda jijin Port ili kutafuta taarifa za ndugu zao. Jambo hili ni gumu sana, tena sana kwa kila mtu hapa.

Katika makala nyingine aliyotuma baadaye, aliandika kwamba kwa namna ya kushangaza kidogo kuna hospitali ambayo haitumiki sana katika maeneo ya kaskazini ya kisiwa:

Hospitali ya Moyo Mtakatifu (Sacred Heart Hospital) ni hospitali kamili ikiwa na kila kitu kuanzia wafanyakazi, timu za wanaojitolea wa aina zote yaani walio kazini na wale walio tayari kuingia kazini wakati wowote. Tunaweza kupokea hadi “wagonjwa waliojeruhiwa 200″ hata sasa! Tuna vyumba vya upasuaji na vitanda. Tumewaruhusu wagonjwa waliokuwa wamepata nafuu. Tumeondoa kila kitu kutoka kwenye uwanja wa mpira ili kuruhusu helikopta kutua hapo.

Kituo cha Matumaini ya Kweli na Uokoaji cha Haiti (Real Hope For Haiti Rescue Center), nacho kwa upande wake, kinajaribu kutoa msaada wa dawa na kinaandika:

Sijifanyi kuelewa mateso yanayotokea hivi sasa katika nchi hii. Najua tunahisi kwamba tayari tumepitia mengi katika miaka iliyopita. Wafanyakazi wamekuja kufanya kazi. Wanawaombea wale wanaowapenda sana hapa jijini. Wanaweka matumaini kwamba watapata habari wakiamini kwamba ndugu zao hao watawasiliana nao. Akina mama na akina baba wanawalilia watoto wao. Watoto nao wanawalilia wazazi wao waliofariki.

Hali halisi inakuwa ngumu zaidi pale ulimwengu wa nje unapoanza kuwasili, je, nini kifanyike?

Na bado ulimwengu wa nje unataka kupata habari.
Kwa taarifa zaidi kuhusu tetemeko la ardhi lililoipiga nchi ya Haiti, tafadhali tembelea Ukurasa wetu Maalumu wa Taarifa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.