Haiti: Madhira ya Tetemeko la Ardhi

Mpaka sasa taarifa za majeruhi wanaotokana na tetemeko la ardhi lililoikumba Haiti zimejikita kwenye takwimu za kutisha, lakini ni majina machache tu ndiyo yameambatanishwa kwenye namba hizo. Kwa bahati mbaya, leo hii (14.01.10), mwanablogu maarufu wa kutoka Dominika, Guillermo Peña, alithibitisha kwamba amefiwa na baba yake aliyeitwa Guillermo Peña Sr. kutokana na janga hilo. Baba mtu Peña alikuwa akifanya kazi katika mji wa Port au Prince kama mhandisi katika kampuni ya ujenzi ya Santo Domingo Mera, Muñoz & Fondeur. Mfanyakazi mwenzake na Mzee Pena pia alifariki. Mfanyakazi mwingine wa tatu waliyekuwa naye amejeruhiwa vibaya lakini amekwishaokolewa na kupelekwa katika hospitali ya Plaza de Salud huko Santo Domingo kwa ajili ya matibabu. Tayari wanablogu wengi wa Ki-Dominika na wale wanaozungumza Kihispania wamekwishatoa salamu zao za rambirambi kwa Guillermo Peña, Jr. ambaye naye anatuma fikra zake kupitia Twita.

Jamhuri ya Dominika inaonja adha ya baada ya tetemeko la ardhi kwa njia nyinginezo. Mwanablogu wa Ki-Dominika, Jose Sille, anaeleza, pia kupitia Twita, kwamba CESFRONT, kitengo cha kulinda mpaka wa Dominika, kimeanza kukabiliana na mmiminiko wa raia wa Haiti wanaojaribu kuikimbia nchi yao.

se jodio la vaina, confimado eso de que se perdio el control en la frontera por mi hermana que esta por esos lados

Kila kitu kimekwenda mrama, imethibitishwa kwamba udhibiti umekosekana huko mpakani, hiyo ni kwa mujibu wa dada yangu aliye kwenye eneo hilo.

Minong'ono ya watu walionusurika kujaribu kuvuka mpaka bado haijathibishwa, lakini serikali ya Dominika imetangaza kwamba maeneo ya kuvukia mpaka yalikuwa wazi kama kawaida. Hospitali zilizopo katika mji wa Barahona, nchini Dominika, na zile zinazomilikiwa na vikosi vya jeshi ziko wazi kuwapokea raia wa Haiti wanaohitaji huduma za matibabu, vilevile vituo vya misaada vimefunguliwa huko Verón,Bávaro, mkaazi mmoja maarufu ambaye pia ni mtalii amefungua kituo cha kukusanyia misaada katika hoteli inayojulikana kwa jina la Luna del Caribe na ataisafirisha mpaka kwenye mji wa mpakani wa Jimaní. Ubalozi wa Haiti katika jiji la Santo Domingo umeripotiwa kutoa huduma za usafiri kwa raia wa Haiti wanaotaka kwenda nchini mwao.

Mfumo wa simu za mezani umeripotiwa kuwa bado upo kwenye matata: mfumo wa simu za mkononi ndiyo ambao una nafuu. Kampuni ya Large carrier Voila’ ilipatwa na uharibifu lakini bado inaendelea kufanya kazi, hiyo ni kwa mujibu wa kampuni mama ya Voila, Trilogy International Partners of Seattle, ya huko Washington, Marekani.

Eddyson Volcimé, anayeishi katika mji wa Nantes, Ufaransa, anasema aliweza kuzungumza na mama yake aliyeko katika jiji la Port au Prince muda mfupi baada ya tetemeko la ardhi. Alifanyiwa mahojiano na kituo cha kurushia matangazo cha mahali anapoishi:

Haiti : après le séisme, témoignage d'un Nantais
Imepandishwa na presseoceanHabari kwa picha za video kutoka mahali mbalimbali duniani.

EV:….Mama yangu hajambo. Hata hivyo hana taarifa za wanafamilia wengine…hasa ukizingatia kwamba hakuna mfumo wa usafiri unaofanya kazi, kila mmoja anatembea kwa miguu, kwa hiyo kuna taabu kweli ya kuwasiliana.

Mwandishi: Na mama yako alikuwa upande upi wa kisiwa hicho wakati wa tukio?

EV: Alikuwa palepale jijini Port-au Prince, palepale kwenye kitovu cha tetemeko hilo.

Mwandishi: Je, alikueleza yale yaliyotokea kwenye simu?

EV: Alinieleza yale yaliyomkuta yeye, hatuwezi kujua sehemu nyingine mambo yalikuwaje.

Yeye alikuwa kwenye mgahawa wakati tetemeko la ardhi lilipotokea, kwa hiyo kulikuwa na kuhamaki kwingi. Baadhi ya watu walifia kwenye mgahawa huo baada ya kuporomokea ndani. Yeye aliwahi kukimbilia nje.

Tangia hapo … kwa kusema kweli, tangia hapo, watu wapo mitaani…wale walioshindwa walikuwa na majeraha mabaya sana kwa vyovyote vile.

Mwandishi: Vipi, una hofu kuhusu usalama huko nyumbani?

EV: Kwa upande wa mama – kusema ukweli, yeye yuko salama, kila kitu ni shwari sasa.

Kwa wanafamilia wengine…kwa sasa hivi hatujui kitu, hatujasikia chochote…tunasubiri kupata habari. Kumekuwa na wahanga, wengi wamejeruhiwa…

Mwandishi: Kwa upande wa kisaikolojia, hali ya mama yako ikoje?

EV: Mungu wangu! Kwa umri wake ameona mambo mengi, lakini yeye hajambo, hana tatizo.

Huko jijini Port au Prince, wengine bado wanajaribu kujikusanya. Bw Jean Francois Labadie, mmoja wa walionusurika alituma taarifa alizokusanya kuhusu janga hilo muda mfupi baada ya usiku wa manane leo hii alfajiri:

13/01/2010 00:25

Tetemeko la kwanza, mtikisiko wa kumi na nne
Saa 6:30 mchana : Kwa kweli tungetamani sana kama lingekuwa la mwisho …Ama kwa hakika, huwezi kuishi mara mbili…
Kuelekea saa 10:45 mchana, tukiwa na dereva wetu, tunaenda kuegesha gari katika eneo la Karibeani, Soko kubwa la Pétion-ville. Kama kawaida, kasi inapunguzwa na msongamano wa kawaida wa Delmas. Tulipokuwa tunaliingiza gari mahali pa maegesho, gari letu linaanza kucheza. Niliona kama wavulana watatu au wanne wakiwa kwenye sehemu ya mbele ya gari wakilitingisha kwa nguvu. Kwa mbele yetu, eneo la maegesho lilianza kucheza na kufanya mawimbi makubwa kama katika eneo la bahari la Wahoo. Jengo la Karibeani lilianza kucheza na katika muda wa sekunde tatu tu likaporomoka lote. Wingu jeupe liligubika eneo lote la maegesho na mtu ungeweza kuona mazimwi meupe yakiibuka kutoka kwenye vumbi, kila mmoja akiwa katika mhamaniko mkubwa.
Mara vumbi limetulia tena – ingawa awamu hiyo bado ni mapema – yaelekea lundo la zege kutoka kwenye jengo la ghorofa 4 halikuacha mtu akiwa hai. Watu wameingiwa na ukichaa, wanajaribu kukimbilia sehemu ya Patroo huku walinzi – akiwemo mmoja aliyejeruhiwa vibaya – wakijaribu kufunga lango lililo nyuma yetu. Dereva ambaye alielewa mapema zaidi yangu kuhusu kilichokuwa kikitokea, anajitahidi kuomba dua kwa nguvu zake zote. Anapaaza sauti za kuomba kwake huku mikono ameinyanyua juu kuelekea mawinguni. Licha ya kunipigia kelele kali kwenye ngoma za masikio yangu, ananisaidia kupata utulivu. Anafanya mkanganyiko huu wa ajabu unaotokea mbele ya macho yetu uanze kueleweka. Baada ya kitu kama dakika tano hivi za vurugu, waendesha magari wachache wanaweza kuendesha magari yao ili kurudi nyumbani baada ya kuwaamuru walinzi kufungua lango lenye urefu wa futi 15. Mwonekano wa eneo la Delmas ni wa kusikitisha, unaogofya. Tuliendelea kuendesha kwa muda wa saa moja tukipita katika majengo yaliyoporomoka, watu wakikimbia hovyo, wengine wakilia na kuliitia jina la Yesu, wengine wakimwita kwa ishara za mikono, vichwa vikiwa vimejaa vumbi jeupe, wakitazama huku na huko pasipo kuamini yaliyotokea, majeruhi, maiti au vipande vya miili ya watu… Jean-clause anaendelea kwa nguvu zake zote kuonyesha imani yake katika kipindi chote cha safari hiyo. Kutoamini kwangu Mungu kunafunikwa na imani ya mwenzangu iliyo motomoto. Matukio yalitokea kama vile ni sinema ambayo mtu ameitazama hata mara elfu moja. Ninafaulu hata kuimiliki hali yangu ya kuwa na wasiwasi hasa baada ya kushindwa kufika kwa Jehanne baada ya kuona kwamba jengo fulani la ghorofa moja lilionesha mitikisiko. Nitamkumbatia kabla hajaelewa juu ya ukubwa wa janga, maana hali ilikuwa tofauti katika mji anakoishi. Tunajiandaa kwenda kulala huku tukihofia mitikisiko zaidi ambayo iliigubika jioni yote. Tunamwaminia kabisa fundi sanifu mwenye nyumba wetu. Mpaka baadaye.

Mpaka kufika mchana huu ndege zenye kuleta misaada zimeripotiwa kuwa tayari zimekiwishafika katika uwanja mkubwa wa ndege wa Haiti.

Rocio Diaz aliripoti kutoka Santo Domingo. Tafsiri za Kifaransa zimefanywa na Suzanne Lehn na Katharine Ganly.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.