Urusi: Jinsi Abiria wa “Nevsky Express” Walivyoeleza Habari Kupitia Vyombo Vya Habari Vya Kijamii

Mamlaka nchini Urusi yanaendelea kuchunguza ajali ya treni la “Nevsky Express” [ENG] ambayo ilitokea kati ya Moscow na St Petersburg usiku wa Ijumaa. Kwa mujibu wa maofisa, dhahama hiyo iliyochukua maisha ya angalau abiria 25 ilikuwa ni shambulio la kigaidi. Ajali hiyo imezua maswali mengi. Watu wengi wanauliza ni nini kilichotokea katika masaa ya mwanzo baada ya ajali na ni kwa nini ilichukua muda mrefu kuanza kutoa taarifa za ajali hiyo.

Kwa kuwa dhahama hiyo ilitokea mbali na maeneo yenye makazi ya watu, ilichukua muda mrefu kwa wanahabari kuwasili kwenye eneo la ajali. Na ndipo picha za kwanza na video zilipoanza kuonekana kila mahali. Je nini kilichoyatokea majukwaa ya uanahabari wa kijamii ambayo yalitaarifu vilivyo kuhusu ajali ya ndege mjini Perm [ENG] mwezi Septemba 2008.

Abira pekee ambaye alitoa taarifa mara moja kuhusu ajali ya “Nevsky Express” alikuwa mtumiaji wa Twita Lazy Frog. Aliandika mara 12 kuhusu ajali hiyo kabla ya kuwasili nyumbani. Haya ndio aliyoandika:

Nipo hai. Lakini nitaeleza kuhusu (ajali) baadaye. Kama mtu ataeleza chochote kwenye habari, tafadhali niandikie. Hawatuambii kila kitu hapa.

Baadaye, abiria wengi kutoka mabehewa ya kwanza – ni mabehewa ya mwisho ambayo yaliteguliwa kutoka kwenye reli –walisema kuwa kwa saa zima baada ya ajali hawakufahamu chochote. Lazy frog alituma habari mpya za nyongeza:

Tumepanda treni jingine. Nilifanya kila nilichoweza.

Hivi sasa tupo SAPSAN (treni mpya ambyo iliwachukua abiria kwenda St. Petersburg – G.A). Natamani ingekuwa inakwenda polepole.

Wametangaza sasa hivi kuwa watu walitayarishwa rasmi wangetulaki kwenye kituo cha treni.

Siku iliyofuata baada ya dhahama, Lazy Frog aliandika muhtasari wa uzoefu wake:

Nilizihisi hisia za kwanza kuhusu kilichotokea wakati tulipofika karibu na Piter (St. Petersburg G.A). Sikuwa na wasiwasi nilipokuwa katika eneo la ajali. Nilikuwa na hofu kidogo na viatu vyangu – kulikuwa na tope kila mahali na mawe yenye ncha.

Jumamosi habari nyingi zilijitokeza wakati abiria walipoanza kublogu kuhusu yaliyowakuta. Makala ya blogu maarufu zaidi inayohusiana na mada hii iliandikwa na mtumiaji wa LJ paltus_mk [RUS] ambaye alikuwemo ndani ya mabehewa ya mwisho yaliharibiwa vibaya na mlipuko. Aliandika [RUS]:

Yote yanatokea ndani ya sekunde 10 wakati unapofahamu ni nini kitakachotokea. Nilikuwa na muda wa kutosha kuutayarisha mwili wangu. Lakini hakuna linaloweza kusaidia dhidi ya kanuni za Newton wakati dazeni za tani za vyuma zinaposimama mara moja wakati zikiwa katika mwendo wa kasi – ni bahati tu… kwa hiyo nilikuwa na bahati tu. Kaka yangu alikuwa na bahati, pia, ukiachilia mbali ukweli kuwa majeraha yake yalikuwa yanatisha kuliko yangu.
[…]

Kila kitu ambacho kilikwenda mrama hadi kusimama kabisa kulichukua kama sekunde 30 hivi. Ilikuwa giza na kimya. Watu walioumia walianza kulia. Nilikuwa sakafuni, nimekandamizwa na miili mingine. Niliisogeza ile miili. Niliona kuwa nimelowana na damu lakini damu ile haikuwa yangu. Niliona kuwa ni mzima na miguu yangu na mikono vuinafanya kazi. Kichwani nilikuwa na jeraha linalovuja damu. Ilinibidi ninyanyuke na kusubiri kwa muda kiasi kabla ya watu wenye majeraha mado waliposafisha njia ya kutoka.
[…]
Mateso yalikuwepo kila mahali. Tulikuwa tumeketi mwishoni mwa behewa na mikoba yote ilipaa ikituelekea. Watu wengi waliojeruhiwa. Katika dakika chahce baada ya ajali, behewa lilikuwa ni kama fungu la miili, viti na sehemu za treni ambazo zilikuwa zimesambaa sawia kila mahali.

Paltus_mk anasimulia habari za uokoaji zenye maelezo ya kina kuanzia dakika za mwanzo baada ya ajali, lakini wakati huo huo anaepuka ufafanuzi ambao ungeweza kuwastua wasomaji. Anaandika kuwa abiria walianza kupeana huduma ya kwanza kwa ushujaa bila kuogopa. Anasema haikuwezekana kuhesabu ni wagtu wangapi waliofariki. Waokoaji waliwasili saa moja na nusu baada ya ajali. Paltus_mk na kaka yake hatimaye waliokolewa na kupelekwa kwenye hospitali jirani na baadaye aliwasili mjini St. Petersburg.

Hadithi nyingine ya kunusurika ilichapishwa na mwanablogu pancakyes katika huduma nyingine ya kublogu ya Kirusi Ya.Ru. behewa lake halikuharibiwa na mlipuko. Alichapisha makala yake ya kwanza saa 4:11 za usiku – nusu saa baada ya ajali – pale pale kwenye eneo la ajali. Aliandika kuwa treni ilisimama kutokana na ajali ya namna fulani, mabehewa machache yaliteguliwa na kwamba angewasili nyumbani kwa uchelevu kuliko ilivyotarajiwa. Karibu saa zima baadaye, aliongeza kuwa kulikuwa na waathirika katika mabehewa mawili ya mwisho. Jumamosi, pancakyes alichapisha habari nzima kuhusu ajali [RUS] kama alivyoshudia mwenyewe:

Tulihisi mitetemo michache ambayo ilikuwa ikiongezeka nguvu. Vitu vilianza kuanguka kutoka mezani. Haikuwa wazi ni nini kilichotokea. Hapakuwa na matangazo. Kwanza tulidhani kuwa halikuwa jambo lenye uzito. Pengine kuna mtu aliyesimamisha treni kwa makosa. Lakini makondakta wenye sura zenye hofu walianza kukimbia kila mahali wakikusanya magodoro, vitambaa vya mezani na maji. Walitutaka tusiondoke kwenye viti vyetu isipokuwa kama ni madaktari. Tulisikia mambo mabaya kutoka kwenye redio zao. Uvumi ulianza kusambaa. Hatukuamini kuwa mabehewa mawili yalikuwa yametengana na yalikuwa mbali sana. Baadaye tuligundua kuwa ilikuwa kweli.

Tulitoka nje na tulitaka kusaidia. Tulikwenda mpaka behewa la tatu. […] hatukutaka kuwa waduwazi ambao wanaongeza wingi wa watu bila fursa yoyote ya kusaidia. Pia hatukutaka kuona yale ambayo watu waliotoka huko walikwishatueleza.

Mara baada ya ajali, majukwaa ya uanahabari wa kijamii yalikuwa sehemu ya kwanza ambayo wanahabari wa Kirusi walikuwa wakitafuta habari. Mwandishi kutoka Shirika la Habari la RIA-Novosty aliacha maoni kwenye blogu ya pancakyes na kumtaka mwanablogu huyo ampigie simu mara moja. Tatyana Landa (mtumiaji wa LJ mwenye jina la Elada) aliandika kwenye blogu yake [RUS] kuhusu rafiki aliyenusurika ambaye alikuwemo kwenye treni. Mara moja wanahabari wawili waliacha maoni ya kumtaka awasiliane nao. Baadaye Tatyana alichapisha makala ya hasira [RUS] ambamo alisema kuwa mwanahabari kutoka “Komsomolskaya pravda” (gazeti la udaku la Kirusi) alikuwa akijaribu kumpata kwa simu mara kadhaa usiku huo. Makala hiyo iligeukia mahali ambapo watu walianza kujadili kama wanahabari wanaweza kuwatumia wanablogu kama chanzo cha taarifa zinazohusu hii ajali ya treni. Wanahabari pia walijaribu kuwasiliana na mwanablogu ambaye aliandika [RUS] kuwa aliamua kutopanda treni la “Nevsky Express” katika dakika ya mwisho.

Baadhi ya wanablogu walieza kughafirika kwao [RUS] na ukweli kuwa ni watu wachache mno kutoka kwenye treni walitumia vyombo vya habari vya kijamii kutoa taarifa za kile kilichokuwa kinatokea., Na, inavyoonekana, kuna fafanuzi kadhaa zinazoelea ni kwa nini uanahabari wa kijamii haukuchukua nafasi kubwa katika upashaji wa habari za ajali ya “Nevsky express”.

Twita, jukwaa zuri la kublogu moja kwa moja, si maarufu nchini Urusi. Kwa mujibu wa twitRU [RUS], kuna watumiaji wa Twita 2,700 tu ambao wanaandika kwa lugha ya Kirusi. Wakati huo huo, majukwaa maarufu ya kublogu nchini Urusi kama vile Livejournal.com au ya.ru yangeweza kutumika ili kublogu moja kwa moja lakini, kama ilivyojadiliwa hapo juu, kuna mifano michache tu ya matumizi hayo.

Ufafanuzi wa pili unahusiana na nafasi ya zana za mkononi na uunganishaji. Zana za mkononi zinaongezeka nchini. Warusi zaidi na zaidi wanaweza kutumia mtandao wa intaneti na zana nyingine za mtandaoni. Tabia hii ina nguvu katika maeneo ya Moscow na St. Petersburg. Lakini ajali ilitokea mbali na maeneo ya mjini ambako, kama mashihidi walivyotaarifu, uwezo wa kupatikana kwa mawasiliano ya simu za mkononi ulikuwa mdogo. Mwanablogu pancakyes anasimulia tatizo la mawasiliano:

Mawasilian ya simu yalikuwa mabaya sana. Inawezekana kuwa kila mtu alijaribu kupiga simu kwa wakati mmoja na mtandao ulielemewa. Nilianza kupata jumba za maandishi pale tu nilipokuwa kwenye treni la pili (treni ambalo liliwachukua abiria kwenda Saint- Petersburg G.A.). Ningeliweza kutumia mtandao wa intaneti, lakini ilikuwa ni vigumu mno.

Hii ni tofauti, ajali ya ndege kule Perm mwaka jana ambayo ilitoa fursa nyingi kwa uanahabari wa kiraia:

1. Ndege ilianguka ndani ya mipaka ya mji ambako watu wengi waliweza kuona ni nini kilichokuwa kinatokea kutokea madirishani. Ajali ya “Nevsky express”, kama ilivyoelezwa awali, ilitokea sehemu za vijijini.

2.Habari zilizoandikwa kwa uanahabari wa kijamii kule Perm zilitokana na maelezo ya walioishuhudia ajali ambao hawakuwamo katika ajali (kwa bahati mbaya, hapakuwa na walionusurika kutoka katika ile ndege). Mashahidi wote wa tukio la “Nevsky Express” walikuwa ni abiria katika treni.

3. Watu wengi walituma habari mpya juu ya ajali ya ndege kule Perm kwa kutumia tarakilishi za nyumbani. Walionusurika kwenye “Nevsky Express” walitegemea zana za mikononi.

Tofauti hizi zinabainisha kwa nini vyombo vya habari vya kiraia vilikuwa mbele katika ajali ya ndege na vilikaribia kutokuwepo kwenye tukio la “Nevsky Express.”

Pia inawezekana kudai kuwa urusi bado haijaendeleza utamaduni wa utoaji taarifa kupitia uanahabari wa kiraia. Na ndiyo sababu abiria wawili tu walikuwa na msukumo wakutosha kwenda kwenye mtandao na kujipa kazi ya uanahabari wa kijamii. Na pia inaweza kufafanua upinzani wa abiria na wanablogu kwa wanahabari ambao walikuwa wanatafuta taarifa za ajali kwenye vyombo vya habari vya kijamii.

Inaonekana kana kwamba ulimwengu wa blogu wa Kirusi bado uko mbali na kuwa chanzo kikuuu cha kutangaza habari mpya. Bado unabaki kuwa sehemu ya usambazaji wa habari na mijadala mipana inayohusu nini kilichotokea.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.