Tunisia: Mwanafunzi Atupwa Gerezani kwa Kuhojiwa na Chombo cha Habari

Mwanafunzi raia wa Tunisia, Mohamed Soudani, 24, alitoweka mnamo tarehe 22 Oktoba 2009 nchini humo baada ya kufanya mahojiano na Redio Monte Carlo International na Redio France International.

Soudani alikuwa ametoweka kwa muda wa siku 18 mpaka pale Polisi wa Tunisia walipowasiliana na familia yake kuwataarifu kwamba kijana huyo alikuwa ametupwa katika gereza la Murnaguiya, kiasi cha kilometa 15 kutoka katika mji mkuu wa Tunis.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, polisi pia waliiarifu familia ya Soudani kwamba alikamatwa na kupelekwa mahakamani na kupatikana na hatia ya kosa la “kuwa na mwenendo mbaya” wakati wa kuwa kwake kizuini pasipo msaada wa mwanasheria na hivyo kuhukumiwa kifungo cha miezi minne gerezani. Familia yake pia walikuja kufahamu baadaye kwamba kijana huyo alikuwa amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Alipopelekwa mahakamani mnamo tarehe 6 Desemba, Soudani alikana mashtaka yaliyotolewa dhidi yake na kueleza kwamba aliteswa vibaya sana wakati alipokuwa ametupwa kizuizini kinyume cha sheria. Wanasheria wake waliomba muda wa kuipitia upya kesi yake na kutaka aachiwe kwa dhamana. Ombi hilo la kuachiwa kwa dhamana lilikataliwa na kesi kuahirishwa mpaka 14 Desemba 2009.

Soudani alihojiwa kuhusu shughuli zake wakati alipokuwa kiongozi wa wanafunzi katika Umoja Unaowaunganisha Wanafunzi wa Tunisia. Mwaka jana alishiriki katika mgomo wa kula uliodumu kwa muda wa siku 56 akiwa na wanafunzi wengine wanne wakidai haki ya kurejeshwa shuleni. Vijana hao pia wameandika makala mbalimbali kwenye blogu kuhusu mgomo wao wa kula wakieleza uzoefu wao wa siku hadi siku, na blogu hiyo imekuwa ikithibitiwa sana nchini Tunisia.

Ukurasa wa Facebook na blogu vimezinduliwa ili kumuunga mkono Mohamed Soudani katika kipindi hiki kigumu anachokipitia.

Nasser Weddady amesaidia kuandika makala hii.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.