- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Palestina/Gaza: Matayarisho ya Maandamano ya Uhuru Gaza

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Israel, Misri, Palestina, Haki za Binadamu, Maandamano, Vita na Migogoro, Vyombo na Uandishi wa Habari, Wakimbizi


Tarehe 31 Desemba, Maandamano ya Uhuru Gaza yatafanyika kuadhimisha mwaka tangu Operesheni Tandaza Chuma [1], au Shaumbulio la Israeli mjini Gaza.

Muungano wa Kimataifa wa Kukomesha Vikwazo Haramu Vinavyoizingira Gaza unaandaa kikundi cha kimataifa kitakachoandamana bega kwa bega na watu wa Gaza, katika onyesho la amani la mshikamano ambalo lina matumaini ya kumaliza vikwazo huko Gaza.

Wengi wa waandamanaji wameshawasili mjini Cairo kwa ajili ya maandalizi.


Maandamano ya Uhuru yanashirikisha watu wengi wenye uzito, pamoja na Alice Walker, muigizaji wa ki-Syria na mkurugenzi Duraid Lahlan, Roger Waters wa Pink Floyd, na kundi la muziki wa kufoka la Kifaransa MAP, kati yaw engine wengi.
Mmoja wa washiriki ni muhanga wa Mauaji ya Wayahudi yaliyofanywa na ma-NAZI (Holocaust) Hedy Epstein.

Hedy Epstein amekuwa akielimisha na kuoneza utambuzi kuhusu maandamano hayo. Mnamo Desemba 1, 2009, pamoja na J’Ann Allen, mke wa ofisa wa jeshi mstaafu na Sandra Mansour, mkimbizi wa Kipalestina, alitangaza hadharani mwalikowa kwenda Gaza kwa mwanaharakati wa siasa, Mshindi wa Tuzo ya Nobeli na muhanga wa mauaji ya halaiki ya Wayahudi Elie Wiesel.

Ushiriki wa Hedy Epstein katika maandamano umepokelewa kwa furaha:

Desertpeace anashangilia ushiriki wake [2]:

Kumuona aliyenusurika katika matukio ya kutisha [Holocaust] akipambana dhidi ya maovu ya leo kwa kweli ni jambo la kutia moyo. Ninamuongelea Hedy Epstein, ambaye wakati ninaandika, yumo njiani kuelekea Gaza kushiriki katika Maandamano ya Uhuru Gaza. Hiki ndicho mauaji ya Wayahudi yangetengeneza kama nyanja, nyanja ambayo hairuhu kurudiwa tena kwa yaliyopita…. ISITOKEE TENA KAMWE!

Maandalizi ya maandamano hayo hata hivyo, hayajatukia bila vikwazo, na waandalizi Muungano wa Kimataifa wa Kukomesha Vikwazo Haramu Vinavyoizingira Gaza, hawako mbali na kukosolewa.

Norman Finkelstein, mwandishi wa The Holocaust Industry na ‘aliyeyaota’ maandamano mwanzoni alikuwa mwanachama hai wa wa muungano huo, lakini amejiuzulu. Kukarahika kwake kulitokana na tamko lililojadiliwa sana la muungano huo. Tamko la asili lilikuwa kuandamana ili kuvunja vikwazo vinavyoizingira Gaza kwa mujibu wa kanuni za amani zilizojikita katika sheria za kimataifa. Tamko hilo lilibadilishwa ili kujumuisha ‘muktadha wa siasa,’ ambao Finkelstein aliuona kuwa unaleta utengano kwani ulileta masuala tata yasiyo ya lazima kwa dhana ya asili ya maandamano. Wakati hayaweki wazi mabadiliko ambayo anayapinga, anatoa maoni katika makala Kwa nini nilijiuzilu kutoka kwenye Muungano wa Maandamano ya Uhuru Gaza [3]:

Pengine inapaswa isisitizwe kuwa sehemu tuliyotengana haikuwa iwapo mtu binafsi aliunga mkono haki fulani ya Wapalestina au mkakati wa kukomesha kukaliwa kwa mabavu. Sehemu hiyo ilikuwa iwapo kulikuwa na ulazima wa kujumuishwa kwa haki fulani au mkakati hata kama havihusiani na lengo lililopo la kuvunja vikwazo na kupunguza matarajio ya maandamano ya kweli ya umma.

Kuondoka kwa mtu huyu mwenye sifa kubwa kulifuatiwa na kujitoa idadi ya wanachama hai wengine. Max kwenye Jewbonics [4] alieleza kujitoa kwake kwenye wimbi hilo kwa masikitiko. Kama muandalizi wa maandamano alitoa maoni kuhusu hofu kwamba wengine wangeliacha wimbi hilo, alitaarifu:

Nafikiri ni salama kusema kuwa idadi iliyopotea itaonekana ndogo kwa idadi itakayoonezeka, ikiwa nilichikiona binafsi na kwenye mtandao kinaashiria chochote

Bila kujali wasiwasi juu ya idadi inayokubaliana na maandamano, haya kwa kweli ni maandamano ya halaiki, na itakuwa mara ya kwanza kwa Wapalestina kukusanyika pamoja kwa idadi kubwa pamoja na waunga mkono wa kimataifa: kuna takriban washiriki 1,300 wa kimataifa watakaoshiriki, ambao watakutana mjini Cairo na kuandamana bega kwa bega na wakazi wanaokadiriwa kufikia 50,000 pindi watakapoingia gaza kupitia Rafah.

Kwenye Electronic Intifada, Rami Almeghari anataarifu [5] kuwa:

Katika miezi ya karibuni, watu wa Gaza wanaamini kuwa jumuiya ya kimataifa imeanza kuelekeza macho yake sehemu nyingine, na kutotilia maanani vikwazo vinavyoizingira Gaza. Vyombo vichache vya habari vya kimataifa vinatilia maanani hali ilivyo hapa.

Maandamano haya yanatarajia kubadili hali hiyo. Mustafa al-Kayali, mratibu wa kamati ya maandalizi ya maandamano ya Uhuru Gaza, anataarifu:

Tunawataka watu wa mataifa wanaokuja hapa kutochukulia ziara yao kama utalii. Badala yake, wafikishe ujumbe wa kweli kutoka hapa kwa watu wao, mashirika au serikali…
Wengi wa vijana niliiongea nao juu ya Maandamano ya Uhuru Gaza walielezea msisimko na hamu ya kushiriki. Wana hamu ya kutuma ujumbe kwa dunia ya nje kuwa wat wa Palestina wapo na kwamba binadamu wanapaswa waungane kwa ajili ya uhuru.

Habari zaidi kuhusu Maandamano ya Uhuru Gaza, washiriki, madhumuni, na matayarisho yanayoendelea vinaweza kupatikana hapa [6].