Ujauzito na Magereza: Afya na Haki za Wanawake Magerezani

Je, wanawake wote wajawazito wanastahili haki sawa za binadamu, au wanawake wajawazito walio jela huziacha haki hizo?

Kuna maswali machache yanayokuja akilini kuhusu haki ya mwanamke mjamzito kuishi na kumlea mwanae anapokuwa kapatikana na hatia kwa kosa la jinai la namna fulani:
• Inakuwaje kwao wanapokuwa wajawazito na kupata mtoto wakiwa gerezani?
• Je, wanapaswa kuwa kipaumbele wakati kuna wanawake wengine nje ya vyuo vya mafunzo bila msaada wa kitabibu?
• Je, ujauzito unapaswa kuwa juu ya hali nyinginezo za kisheria kumhakikishia mwanamke mjamzito haki zake za kibinadamu?

Marekani: wanawake walio kwenye uchungu wa kuzaa hawatafungwa tena minyororo.

Je unaweza kufikira mwanamke akijifungua huku mikono yake ikiwa kwenye pingu na miguu yake ikiwa imefungwa na minyororo kwenye kitanda? Malika Saada Saar, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Rabecca kwa Haki za Binadamu, anatuelezea kuhusu kitendo hiki ambacho bado kinatokea nchini Marekani, ambapo wanawake wajazito wanaotumikia kifungo wamekuwa wakifungwa minyororo wakati wa uchungu na kujifungua na kuwa hiki ni kitendo kilichozoeleka katika baadhi ya magereza (ya kurekebishia tabia), ingawa ni hatari kwa afya ya mama na mtoto. Ifuatayo ni video ya mahojiano yaliyoambatanishwa kwenye makala iliyoandikwa kwa ajili ya mradi wa RH Reality Check, jamii ya mtandaoni kuhusu afya na haki ya uzazi na jinsia inatupa taarifa na uchambuzi kwa afya ya uzazi:Kitu gani hutokea kwa mtoto mchanga wa wa mfungwa baada ya kuzaliwa?

Nchi mbalimbali zina kanuni tofauti kuhusiana na watoto magerezani. Kwa mfano, nchini Argentina, kwa mujibu wa Ajintem, chombo cha mawasiliano cha taarifa za uhamamiaji, sheria ilipitishwa mwaka uliopita ikifafanua kwamba wanawake wajawazito, wanawake wenye watoto wadogo chini ya miaka mitano na wale wenye watoto walemavu wangenufaika na mpango wa kutumikia kifungo chao makwao chini ya ulinzi wa nyumbani. Sheria hii ingewanufaisha si tu akina mama, ambao kwa kuwa gerezani wasingepata huduma za afya wakati wa ujauzito, lakini pia (ingemnufaisha) mtoto, ambaye angelelewa ama katika mazingira yasiyo salama yanayokosa uhuru na upungufu wa udhibiti wa afya na chakula, au wangelelewa mbali na mama, na hivyo kusababisha mlolongo wa matatizo mengine. Hata hivyo, ujumbe ni kwa ajili ya mahakimu kufuatilia kiini cha sheria na kutoa ruhusa hii kwa wanawake wale ambao hawahusishwi na mashitaka ya jinai ya matumizi ya nguvu, kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya raia iliyobaki haiuchukulii ujauzito kama kadi ya kumtoa mtu jela bure.

Katika visiwa vya Canary, kwa mujibu wa blogu ya Prisiones y penas, ambayo huandika kuhusu habari zinazohusu jela na magereza, wanawake wanaruhusiwa kuishi na watoto wao hadi umri wa miaka mitatu ndani ya selo zao, lakini wakiwa pamoja na wafungwa wenzao, kitu ambacho sio mazingira mazuri sana kwako. Kwa hiyo, wanawake wajawazito au wanawake wenye watoto wenye umri wa chini ya miaka 3 huambiwa kuhusiana na kuingia kwenye magereza kuwa si vizuri kwa mtoto kukualia gerezani, na hupewa uchaguzi wa kumpeleka mtoto kwa wanafamilia wengine. Hali ni hii hii huko Peru na Urusi. Nchini Marekani, kuna magereza mawili tu yenye kuruhusu jambo hili, huko New York na Nebraska, kama ilivyoonyeshwa na mpiga picha maarufu Jane Evelyn Atwood kwenye insha ya picha zake tatu kwa ajili ya Shirika la kimataifa la Amnesty International, inayoitwa Too Much Time, ambapo alitembelea dazani nyingi za magereza kote duniani kurekodi na kuweka kumbukumbu za maisha ya wafungwa.

Kwa nini mfumo wa magereza nchini Marekani hauruhusu, kwa ujumla, wanawake wenye watoto kubaki nao? Atwood anaeleza kwamba kwa sababu ya mazingira ufungwa, hairuhusiwi. Kwenye blogu ya Prison Photography wanaelezea madai haya:

Watoto hawahusishwi kwenye magereza yote isipokuwa mawili tu nchini Marekani. Tishio la usalama linatajwa kama sababu: mtoto ndani ya gereza ni dhaifu na atakuwa shabaha ya malengo maovu siku zote. Madai yanaonekana kuwa hayana maana kwa kiasi fulani kwa unapofananisha na mifumo ya adhabu kwa nchi nyinginezo.

Insha ya Atwood kwenye wavuti ya Amnesty International inaonyesha mambo mawili, sehemu inayohusu taratibu za kujifungua huku umefungwa minyororo kama yalivyoelezwa kwenye Mtoto wa Vanessa na pia inaonyesha jambo jingine kuhusu mfumo wa magereza na umama, kwa kutumia picha za wanawake wakati mpigapicha akisoma insha kuhusu uzoefu wake wa kutembelea magereza huku akipiga picha.

Ujauzito kama zana ya mapatano?

Kwa nini haki za wanawake wajawazito gerezani zinatatanisha? Katika Russia Today, idhaa ya matangazo ya Kirusi, mada hii inatajwa panapojadiliwa suala la watoto kuzaliwa na kulelewa katika mfumo wa magereza wa Kirusi:

Wenye kutilia mashaka (suala hili) wanadhani akina mama wengine hupata ujauzito kwa makusudi ili tu kurahisisha maisha huko gerezani. Ruhusa ya kwenda hospitali, halafu kuwa na ratiba iliyojaa muda mwingi na mwanao –ni afadhali kuliko kukaa kwenye seli ya magereza, wanadai.

Na kuna wanawake ambao wanaona kwamba kuwa na mimba ni njia pekee ya kukwepa hukumu, kama ilivyotokea mwezi Juni, pale mwanamama wa Kiingereza aliwekwa ndani na kuhukumiwa kifo huko Laos kwa sababu ya kusafirisha madawa ya kulevya akapata ujauzito gerezani na akanusurika kunyongwa, kwa sababu serikali ya Laos isingemnyonga mwanamama mjamzito. Madai yaliyotolewa kwa mujibu wa jarida la Kiingereza la Daily Express, ni kwamba alipata ujauzito kwa kupandikiziwa mbegu za kiume ‘ili kupata hukumu nyepesi zaidi”

Kwa maneno yao: Wanawake wanaeleza kuhusu watoto wao na maisha ya gerezani

Geraldin Rodríguez, Mwajentina aliye kwenye jela za Ecuador kwa sababu ya biashara ya madawa ya kulevya anamueleza Marcos Brugiati, mwandishi mshiriki katika chapisho la mtandaoni linalohusiana na masuala ya sanaa liitwalo Plastica-Argentina, masimulizi kuhusu kuigiza na kufanya maonyesho ndani ya jela, kupata ujauzito gerezani na kumpata mwanae. Aliruhusiwa kuwa na mwanae, lakini akaamua kwamba mwanae anahitaji kukua akiwa mtu huru:

“Decidí que salga para vivir, tenía miedo que sufra de grande los traumas que hoy tengo. Se lo llevó al año mi hermano quien se hice cargo con su esposa”.

Niliamua aondoke ili aishi, nilikuwa na wasiwasi angeteswa na msongo wa mawazo nilionao leo. Baada ya mwaka kaka yangu alimchukua na anamtunza kwa kushirikiana wa mke wake.

Juvinete yuko kwenye gereza la Kihispania, na alikuwa mjamzito wakati alipofungwa kwa kusafirisha madawa ya kulevya. Anasimulia habari zake kwenye gazeti la kanda huko Uhispania linaloitwa NorteCastilla. Miaka mitatu baada ya kujifungua mwanae akiwa gerezani, mwanae ilibidi aondoke, na alipelekwa kwa familia ya kufikia. Juvinete humuona mwanae huyo wa kike kila baada ya siku 15 na kila miezi miwili hupata ruhusa ya wiki mbili kukaa na mwanae. Hata hivyo, mambo hayaonekani kuwa mazuri sana: kuna uwezekano kwamba Juvinete atapelekwa Brazil alikozaliwa, na anahofia matokeo ya mabadiliko haya kwa mwanae. Anao ushauri kwa mwanamke yeyote anayeamua kupata ujauzito akiwa jela:

-Intento convencerlas para que no se queden en estado dentro porque ver a un niño privado de libertad es muy duro, es irresponsable. Ellos no tienen que pagar nuestros errores.

Ninajaribu kuwashawishi wasipate ujauzito wakiwa bado ndani kwa sababu kumuona mtoto akikosa uhuru wake ni vigumu sana, ni kutokuwajibika. (Watoto wanaozaliwa jela) wasilipie gharama ya makosa yetu

.

Kwenye wavuti ya Woman and Prison, iliyojikita katika kuyatazama maisha ya wanawake wakiwa kwenye mifumo ya magereza , mfungwa Kebby Warner anaongelea ujauzito wake mwenyewe alipokuwa akitumikia kifungo kwenye gereza la Kimarekani, na jinsi alivyotendewa wakati wa ujauzito wake, utungu na baadae, wakati alipokuja kunyang’anywa mwanae. Hapa ni muhtasari anapoandika kuhusu hatua za kujifungua:

Wakati wa utungu, hakuna mtu anaruhusiwa kuwa kwenye chumba cha kujifungulia. Familia yangu wala haikujua kwamba nilikuwa ninajifungua au nimempata (mwanagu) mpaka nilipokuwa nimetoka hospitali. Wakati huo wa siku tatu baadhi ya walinzi walikuwa ndani ya chumba, lakini muda mwingi, wakati wauguzi walipowaomba kukaa nje ya mlango, walitii. Nimesikia simulizi za kutisha za wanawake wakifungwa kwa mnyororo kwenye kitanda cha uzazi. Ninashukuru kwa kutokukumbana na hali hiyo. Wauguzi wengi walinitendea kama binadamu badala ya mfungwa.

Unaweza kusoma shuhuda zaidi kuhusu kukua na mzazi gerezani na madhara mbalimbali ambayo kufunga wanawake kunaweza kuyawasababisha kwa watoto wao kwenye Wanawake na Magereza.

Kwa hiyo unafikiriaje? Kwa wanawake wajawazito duniani kote kutokupata huduma za afya za namna yoyote, je jitihada zaidi zinahitajika kuwanufaisha wanawake walio gerezani? Je, kuna tofauti kati ya wanawake wanaotumikia kifungo kwenye magereza (ya mafunzo) na wale wanaoishi nje? Je, ni lazima kuwatendea tofauti?

Picha iliyotumika kwenye makala hii ni “17 de noviembre” ya daquella manera.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.