Saudia Arabia: Ambako Kuiga Kazi Kinyume cha Haki Miliki ni Kosa la Jinai

Wanablogu wa Kisaudia wanaungana ili kumuunga mkono mwanablogu mwenzao anayelituhumu gazeti moja kuwa limetumia picha na kuzinakili kutoka mwenye blogu yake bila ruhusa.

Saudi Jeans‘ Ahmed Al Omran anazo sifa kiduchu mno kwa gazeti hilo linalotuhumiwa kwa kitendo cha kutumia kazi za wengine kinyume cha haki miliki:

Ingawa gazeti la al – Yaum, kwa muda mrefu limefurahia nafasi kubwa katika Jimbo la Mashariki, (EP) linabaki kuwa kati ya machapicho duni zaidi nchini. Nilizaliwa na kukuzwa katika Jimbo la Mashariki, na nilizoea kusoma magazeti ya Ashraq al-Awsat, al-Hayat na al-Watan lakini sio al-Yaum.

Kutofurahishwa kwa Al Omran kulichochewa zaidi baada ya Saudi Aggie, mwanafunzi mwenye jina la Nathan wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mfalme Abdulla (KAUST) kilichofunguliwa hivi karibuni alipoleta malalamiko kwamba gazeti hilo limetumia picha zake pamoja na uchambuzi wake kuhusu uchaguzi wa wanafunzi hivi majuzi. Ameweka nakala ya habari hizo kutoka gazetini na kuwauliza wasomaji wake:

Siwezi kuamini hili! Angalia makala hii iliyochapishwa hivi majuzi kwenye gazeti maarufu la Saudi Arabia, Al Yaum. Je, picha hizi zinaonekana kana kwamba zinafahamika? Vipi kuhusu maneno? Kama huwezi kusoma Kiarabu, hii ilichukuliwa karibu neno kwa neno kutoka kwenye makala ya blogu yangu niliyoipa jina la ‘uchaguzi’ na kuichapa Oktoba 5, 2009. Hii haiwezi kuwa sahihi kisheria, hata hapa Saudi Arabia!

Mwanafuzi huyo wa Kimarekani anaongeza:

Kama ningekuwa Marekani ningefungua kesi ya haki miliki ya utaaluma dhidi ya Al Yaum. Kama lingekuwa ni Gazeti la New York Times limetumia kazi yangu bila ruhusa, ningekuwa tajiri sasa hivi. Hivi haki miliki za utaaluma kwa mawazo na picha zilizochapishwa zina thamani yoyote hapa?

Al Omran anazingatia:

Nathan anafikiria kuwashitaki, jambo ambalo nadhani litakuwa zuri sana, lakini labda wameshajitia aibu vilivyo wao wenyewe.

Watoa maoni kwenye blogu ya Nathan wanaguswa na yaliyompata mwanablogu:

Mazoo anaandika:

Ninasikitika kuona hili linatokea kwako…
Lakini, hili ni jambo lililozoeleka hapa Saudi Arabia…

Nimesikia kesi nyingi ambazo kazi za marafiki zangu (maandiko ya blogu, picha na mawazo) yameibwa na waandishi habari wavivu. Walilalamikia hali hii na wengine waliaandikia wahariri wakuu –wengine wao huandika taarifa za kuomba msamaha na wengine wao humfukuza kazi mtu aliyeiba maudhui

Al Hanouf, anayejielezea mwenyewe kuwa ni mwanafunzi wa sheria, anataka haki itendeke:

Kama kitendo hiki kikiangaliwa chini ya makosa ya jinai yanayohusiana na kompyuta, basi huyu – mwana habari – inatakiwa awe jela kwa zaidi ya miezi sita na kukulipa si chini ya fedha ya Riyali za Saudia 250,000.
Unapaswa uende kwa mwanasheria, na tafadhali usilimalize hili kwa kuliandikia gazeti barua pepe! Kuna sheria, na (gazeti) halitaweza kurekebisha makosa yake kama tutalimaliza suala hili kwa njia zatu za kizembe!

Na Chiara anashauri:

Nami ninashiriki katika kuchefuka na uvunjifu huu wa sheria ya haki miliki, na njia iliyozoeleka ya kutafsiri na ‘kuiba’ kazi za wengine si nafuu. Unaweza kuweka blogu yako nzima chini ya haki miliki kama ambavyo wanablogu wengine wamefanya, na kufanya namna ambayo jina lako litaonekana kwenye picha.

Kwenye makala fuatilizi, Nathan anaandika:

Nchini Saudi Arabia, umbea huenea kama vile ugonjwa wa mlipuko. Blogu hii imepokea makumi elfu ya watembeleaji wapya katika juma moja tu

[…]

Nilikuja Saudia kujenga madaraja (ushirikiano), sio kutengeneza maadui. Nilikuja kusoma na kutafiti katika Chuo kikuu ambacho kinajitahidi kwa nguvu zote kuwa moja wapo ya vyuo vikuu bora vya utafiti duniani, na sio kupata fedha kutoka kwa watu ama mashirika.

Ninataka uwajibikaji. Ilichokifanya Al Yaum kilikuwa ni makosa, lakini mwenendo wa mjadala pia una makosa.

Na maneno yake ya mwisho kwa wasomaji wake ni:

Kama unataka kuazima kitu kutoka kwenye blogu yangu, tafadhali omba kwanza. Hakuna mtu, nikijijumuisha na mimi, anayependa kutokuelewana.

Kwa kutumia kifaa cha kutafsiri, mwandishi husika anamwandikia Nathan akilielezea vyema suala lake.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.