- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Ofisa Aweka Wazi Ufisadi wa Polisi kupitia Mtandao

Mada za Habari: Urusi, Habari za Hivi Punde, Haki za Binadamu, Harakati za Mtandaoni, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza

Mnamo tarehe 6 Novemba, afisa wa polisi katika Idara ya Mambo ya Ndani huko Novorossiysk [1] alitumia tovuti yake binafsi kuwasiliana na Waziri Mkuu Vladimir Putin na kuzungumzia matatizo lukuki yanayowakabili maafisa wa polisi nchini Urusi.

Kwenye ujumbe wake wa video unaopotakina katika anwani hii ya mtandaoni www.dymovskiy.ru [2] na YouTube (sehemu ya I [3] na sehemu ya II [4] [RUS]), Aleksey Dymovskiy anaonekana kuwa mtulivu na anayejieleza kwa usahihi mkubwa. Anazungumzia juu ya kushuka kwa hadhi ya polisi, rushwa, ufisadi na jinsi gani malipo duni yanavyokuwa kama sumu inayowala maafisa wengi wa polisi nchini Urusi.

Nafikiri watu wengi watanielewa. Nataka kuchapa kazi, lakini nimechoshwa na mipango ya kingano ambapo tunalazimishwa kupeleleza jinai ambazo hazipo. Nimechoshwa na mipango ya kutunga ambapo tunaambiwa tuwafunge watu fulani. Nimechoshwa na jinai za kutunga zinazoandaliwa ili kuwatupa watu fulani gerezani.

Akiendelea kuweka wazi mambo mbalimbali, Dymovskiy anakiri kumtupa mtu asiye na hatia gerezani kwa sababu ya kulazimishwa na mkubwa wake kazini:

Mkurugenzi wa Idara ya mambo ya Ndani alinitunukia cheo cha Meja, ambacho nilikipata mwezi Mei, kwa sababu tu nilimwahidi kutumpa mtu asiye na hatia gerezani. Siogopi kueleza jambo hili. Naelewa kuwa naweza kuadhibiwa kwa sababu hii. Lakini ni ukweli nami ninaukiri.

Dymovsky pia anamwomba Waziri Mkuu Vladimir Putin kupeleleza matatizo hayo na kumalizia mbali tatizo la ufisadi katika jeshi la polisi.
Video yake hiyo ilipata watembeleaji wengi sana muda mfupi tu tangu ichapishwe na vilevile maelfu waliibofya kwenye YouTube. Ilichukuliwa pia sana na kuchapishwa na vyombo vikuu vya habari za Urusi na kujadiliwa sana katika blogu nyingi. Ni mfano mmoja kati ya kadhaa ya kwanza ambapo raia wa Urusi wanafaulu vema kabisa kutumia miundo mipya ya majukwa ya habari ili kuwasiliana na serikali hasa kuhusu masuala nyeti yanayoikabili nchi.

Upekee wa “hotuba za kiraia kwa njia ya video” nchini Urusi inaelezwa vema zaidi kwa maoni yenye tahadhari kutoka katika moja ya blogu maarufu zaidi nchini inayoitwa dolboeb [5]:

Risala yenye nguvu ya pekee. Sitashangaa kama itageuka kuwa mbinu ambukizi ya utafutaji masoko. Mhusika mkuu anaonekana kama mtu wa kutoka sayari nyingine.

Mwanablogu mwingine marchenk [6] anaandika:

Hakuna hata mmoja wetu aliye malaika… simhusudu [Dymovskiy] kama askari mwaminifu na mpenda ukweli (mwenyewe amekiri kwamba alitunukiwa cheo cha Meja kwa kumfunga mtu asiye na hatia gerezani). […] Hata hivyo, nampa heshima kwa ajili ya ujasiri wake wa kuwa mkweli. Kwa hiyo, kumbe kuna maafisa wengine wa polisi walio waaminifu. Kwa sababu yao, ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo na mabadiliko katika jeshi la polisi.

Ninamwombea Mungu ili kwamba uwekaji wake wazi huu wa mambo umpe kinga na atendewe haki katika hali yake.

Siku ya Jumapili, tarehe 8 Novemba, Rashid Nurgaliev, Waziri wa Urusi wa Mambo ya Ndani, alitangaza ukaguzi wa jeshi la polisi huko Novorossiysk. Wakati huohuo, Dymovskiy amefukuzwa kazi kwa sababu ya “uzushi na vitendo ambavyo vinaharibu sifa” ya polisi.

Katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Urusi, “Ekho Moskvy [7],” Dymovskiy alisema kwamba amekuwa akifuatiliwa na kwa hiyo alikuwa akifikiria kuhamishia familia yake jijini Moscow kwa sababu za kiusalama.