Naijeria: Wanablogu Wajadili Sifa Mbaya ya Naijeria

Inajulikana vyema kuwa Naijeria ina tatizo la muonekano – utapeli wa 419 kwenye intaneti, rushwa, uharamia wa mafuta katika jimbo la Delta – kwa watu wengi, huu ndio uhusiano unaokuja akilini wakati nchi yenye watu wengi zaidi Afrika inapotajwa. Hata hivyo, mwaka uliopita umekuwa mgumu kwa watu wa Najeria walio ughaibuni: katika miezi michache iliyopita, mfululizo wa matukio yanayoionyesha Naijeria katika mwanga wa utata ulizua majadiliano kwenye ulimwengu wa blogu.

Mwezi Septemba, Sony ilitoa tangazo la mchezo wa Playstation 3 ambalo lilikuwa na mstari unaosema, “Usiamini kila kitu unachosoma kwenye intaneti – vinginevyo, ningekuwa milionea wa Kinaijeria hivi sasa.” Tangazo hilo lilikumbana na mawazo ya kuchanganyikiwa kutoka kwa Wanaijeria wengi, na Serikali ya Shirikisho iliitaka Sony kuomba radhi (Sony iliomba msamaha na baadaye ikaliondoa tangazo).

Katika wakati huo huolilikuja toleo la filamu ya District 9 – filamu ya kisayansi ambayo ilipokewa kwa mapitio mazuri lakini yaliyowakasirisha Wanaijeria. Serikali ya Naijeria ilichukizwa na jinsi filamu hiyo ilivyowaonyesha Wanaijeria kama wahalifu na wala watu, na iliipiga marufuku ndani ya Naijeria na kulitaka Baraza la Udhibiti kuikamata kutoka kwenye majumba ya sinema. Kwenye mtandao, filamu hiyo ilisababisha maoni yaliyopishana, huku baadhi ya watu wakichukua mtizamo kuwa filamu ina mtizamo wa kibaguzi dhidi ya Wanaijeria, wakati wengine waliitetea kama wakilisho la kubuni lenye chembe ndogo ya ukweli.

Adamu Waziri katika EVCL anasema kuwa mara nyingi jinsi Wanaijeria wanavyoonyeshwa na Wanaijeria pia huwa hakufurahishi:

Nollywood, kiwanda cha filamu cha wazawa, kimetuonyesha katika mwanga mbaya zaidi kwa wote, watazamaji wa kitaifa na wale wa kimataifa. Kuna wakati usingeweza kupata filamu ya Nollywood ambayo haikuwa na haya yafuatayo au mchanganyiko wake: utapeli, uchawi, ujambazi wa kutumia silaha, ngono kati wanandugu, mapenzi nje ya ndoa, kula watu na pia suala tunalolipenda, rushwa. Nollywood imekuwa ikitoa maelfu ya filamu zenye maudhui haya kwa miaka bila pingamizi la kweli kutoka kwa umma wa kawaida au wizara.
… kupiga marufuku filamu kunaanzisha mfano mbaya; na kunaweza kuwa hatari. Tuachieni sisi umma tujadili hili suala. Tumekomaa vya kutosha kufanya hivyo. Kwa kweli, waziri wetu amefanikiwa kuipatia filamu hiyo matangazo zaidi jambo ambalo nina hakika hakulikusudia.

Nicole Stamp anatoa maoni kuhusu masuala ya rangi katika District 9:

Jambo ambalo linanikera ni kuwa watu wengi wanaoiangalia filamu hii hawaulizi, au hata hawaoni, muonekano huu usioaminika wa kibaguzi…. Kwa nini Wanaijeria wasiweze kuwa watu wenye kutaka vitu vyenye mantiki kama vile pesa na silaha? Kwa nini wanaenda nje ya njia zao na kuwa washenzi wa ki-ooga-booga?… haiwezekani kutojali jinsi Wanaijeria wanavyoonyeshwa ambavyo kukiangaliwa katika muktadha mpana, kumepita hali ya kuumiza au kudhalilisha lakini ni hali ya hatari.

Unaweza kusoma zaidi mjadala huu kwenye tovuti ya Nigerianstalk.org au tafuta kwenye google kwa kutumia maneno haya “district 9 race”.

Katika siku za karibuni zaidi, gazeti la Time lilichapisha onyesho la picha na mpiga picha wa Afrika Kusini Pieter Hugo ambazo zilionyesha picha kutoka kwenye kiwanda cha sinema cha “Nollywood” huko Naijeria. Japokuwa halikuwa onyesho tata kama ilivyokuwa District 9 au tangazo la Playstation, mpiga picha huyo hata hivyo alichochea mdahalo katika ulimwengu wa blogu, na mjadala kuhusu kama uonyeshwaji huo wa Wanaijeria uko chini ya fungu la uhuru wa kisanii au upendeleo wa kitamaduni.

Solomon Sydelle kwenye blogu ya Nigerian Curiosity anaandika:

Ninaelewa fika haja ya kusogeza mipaka, kwani shauku hiyo imepelekea kupatikana kwa ubunifu wa kazi za hali juu sana na mafanikio ya wakati wote. Hata hivyo, kwa picha hizi, ninahangaika kuzithamini pamoja na kile kinachoonyeshwa na ninaamini kuwa bila ulazima wowote zilitegemea upendeleo ambao unathibitisha imani fulani potofu za kadamnasi ya Hugo ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya Magharibi.

Matukio haya yametukia katika wakati mbaya kwani yanawiana na mpango mpya uliozinduliwa mwanzoni mwa mwaka huu wa “kutengeneza chapa mpya ya Naijeria” (Re-brand Nigeria). Mpango huo unadhaminiwa na Dk. Dora Akunyili, Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Naijeria, na ambao umekumbana na yote mawili, sifa na kukosolewa (angalia hapa ili kusoma mjadala huo kwenye Global Voices)

Bunmi Oloruntoba katika blogu ya A Bombastic Element anajadili kampeni ya kutengeneza chapa mpya katika muktadha wa mjadala wa hivi karibuni kwenye BBC juu ya suala hilo:

Waziri alikuwa na shauri zuri aliposema kuwa Naijeria haiyatazami mengi yaliyo chanya, haielezi simulizi zake na inafanya makosa ya kuiachia dunia kufafanua taswira yake inayoelemea kwenye sifa zake mbaya pekee. Na anayo mifano mizuri ya mambo chanya. Lakini BBC ilitafuta maafisa uhusiano na wataalamu wa chapa wachache ambao wanapinga kwa kusema, kama nchi inataka kujitengenezea chapa mpya, inapaswa kuipatia timu yoyote ya mahusiano nyenzo zaidi. Wale waliohojiwa walisema, ugavi wa umeme wa uhakika na mwisho wa uchumi unaotegemea mashjine za jenereta kutaizifanya jitihada za kutengeneza chapa mpya ya Naijeria kuwa “rahisi.” Na kuthibitisha maneno yao, dakika 13:40 baada ya kipindi kuanza… naam, haupaswi kuwa Mnaijeria kujua ni nini kilichotokea.

Sehemu angavu ya mjadala wa taswira ya Naijeria ilikuwa ni video iliyosambazwa sana ya mwandishi wa Kinaijeria Chimamanda Ngozi Adichie akiongelea juu ya “Hatari ya simulizi moja.” Adichie anatoa maoni juu ya mitegoya taswira kubwa ya Afrika kama sehemu ya majanga; anatahadharisha kuwa kujekea upeo wa “simuli moja” kunasiliba uzoefu na kutengeneza imani potofu. Kwa wanablogu wengi, maneno ya Adichie yalitoa mwangwi wa kughafirika kwao na taswira ya Naijeria iliyozoeleka nje ya nchi.

Mwanablogu Shade NonConformist anaandika kuhusu uhusiano wa rissala ya Adichie na taswira ya Naijeria:

Ninaamini kuwa hivi ndivyo Adichie alivyomaanisha katika hotuba ya Hatari ya Simulizi Moja aliyoitoa kwenye TED. Inageuka kuwa tatizo pale sura pekee ya Afrika tunayoiona ni ile inayohusisha wanyama waliokufa, umaskini, majanga, vifo, ufisadi, watu mashuhuri wanaasili watoto… unafahamu yadi zote tisa. Sasa sisemim kuwa Afrika haina mambo hayo. Wote tunaweza tukaafikiana kuwa tunayo. Ninachosema ni kuwa mambo hayo si ya nchi za Kiafrika peke yake.
…Mimi/sisi hatutasikoma kukosoa taswira za Afrika ambazo hazina mizani na zenye ubaguzi. Kuonyesha taswira zenye mizani iliyolingana ni jambo muhimu. Kama Waafrika pia tunapaswa kiujifanya kuwa kama vyombo ambavyo viko radhi kutumika katika mabadiliko tunayotakja kuyaona (ambayo tutayaona) katika bala letu tunalolienzi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.