Misri: Haki ya Kijerumani kwa Marwa El Sherbini

Hatimaye, haki imetolewa katika shauri la Marwa El-Sherbini, mwanamke wa Kimisri aliyeuwawa kwa kuchomwa visu na muhamiaji mwenye asili ya Urusi-na-Ujerumani ndani ya mahakama huko Ujerumani. Baada ya karibu miezi mine na nusu, Alex Wiens amehukumiwa kifungo cha maisha, bila ya matarajio ya kuachiwa mapema kabla ya kifungo kumalizika.

Bikya Misr ameandika kuhusu kesi hiyo:

Baada ya karibu miezi mine na nusu, mkasa wa Marwa el-Sherbini umefikia hitimisho la namna Fulani baada ya mahakama ya Ujerumani kumhukumu kifungo cha maisha bila uwezekano wa kuachiwa mapema mtu aliyemchoma visu “shahidi aliyevaa shela” mara 17 ndani ya mahakama mnamo mwezi Julai. Wamisri, Waarabu na kadhalika Wajerumani wameikaribisha hukumu hiyo na wanatumaini kuwa Ulaya na Mashariki ya Kati zitaanza kupona majeraha ya mauaji hayo na kusonga mbele “kuelekea mustakabali bora zaidi.”

Hicham Maged ameandika jinsi alivyoridhika na hukumu, na kuwa ana imani na mfumo wa sheria wa Ujerumani:

Hakimu alikuwa anazitambua mbinu kadhaa za timu ya utetezi ya muuaji na hapa ninanukuu maneno kwa mujibu wa makala hii: “Aliua… si kutokana na hofu bali kutokana na kisasi. Kwa makusudi alitumia nia njema na udhaifu wake (marehemu). “Ninakubaliana na hili na usisahau kuwa alijaribu pia kumuua mume wake.
Ninafarijika kuwa chumba cha mahakama ambamo usaliti huo ulitokea kimeoshwa kwa mikono na kimaadili kwa kutumia haki. Baada ya hayo, imani yangu kwa mfumo wa sheria wa Ujerumani haupaswi kuelezwa kwani kosa hili lilikuwa ni la kustusha kwetu sote na si kwa Wajerumani pekee. Kwa hivyo basi, ni leo hii Marwa na mwanawe ambaye alikuwa hajazaliwa wanaweza kupumzika kwa amani baada ya malipo kwa muuaji.

Zeinobia aliifurahia hukumu, naye pia aliandika kuwajibu wale ambao waliamini kuwa hukumu ile ilikuwa ni ya kisiasa, na kuwa mahakama ya Ujerumani ilitoa hukumu inayomnufaisha Marwa ili kuwaridhisha Wamisri na Waarabu:

Sasa nataka kusema jambo, baadhi ya wabaguzi “na si wachache duniani hivi sasa”, watasema kwamba uamuzi huu ni wa kisiasa; ambao mahakama ilibidi iuchukue ili kushinda mioyo na fikra za Waislamu duniani na kuokoa maslahi ya Ujerumani katika ulimwengu wa Kiislamu.
Naam, kwa heshima yangu yote nilikwishasema hapo awali na nitasema tena; usimfikirie Marwa kama mwanamke wa Kiislamu; mfikirie kama mwanamke mjamzito na mama ambaye kwa yakini alichomwa visu mara 18 mbele ya mwanawe mdogo wa kiume. Aliua roho mbili, roho zisizo na hatia kwa sababu ya chuki isiyoona pamoja na ubaguzi. Anastahili kuwa jela kwa maisha yake yote yaliyobaki kwa kutoa maisha ya roho zisizo na hatia na kuota uhai wa mama kutoka kwa mwanawe.

Aam Mina kwa upande mwingine aliandika makala, ya kuwakebehi wale wanaoamini katika nadharia za njama na waliokuwa wakitarajia Wajerumani kufanya uamuzi utakaompendelea muuaji:

مش عارف ليه من ساعة الجكم مش سامعين صوت الناس اللي فلقتنا وقت الحادث عن عنصرية الألمان و كرههم للعرب و المسلمين و عن إن القضية هتتظبط و الراجل هياخدله سنة أو سنتين و خلاص و انه الحل الوحيد هو الجهاد و محاربة الغرب الصهيوني الفاسد العلماني الكافر

Sijui kwa nini, tangu kutangazwa kwa uamuzi, sijamsikia yeyote kati ya wale waliokuwa wakiongelea juu Wajerumani na jinsi walivyo wabaguzi, na kuwa wanawachukia Waarabu na Waislamu. Pia walidai kuwa mahakama ingetoa uamuzi uanompendelea muuaji na kuwa atafungwa kwa mwaka mmoja au miwili tu, na kuwa tumaini letu pekee ni kutangaza vita takatifu dhidi ya utawala usio na dini, uliooza, Wakizayonisti, na Wamagharibi makafiri.

Kisha aliandika kuhusu mafundisho mengi ambayo tunapaswa kujifunza kutokana na tukio hili:

دي بعض الدروس المستفادة من الغرب الكافر
١- سرعة العدالة.. جريمة القتل تمت في يوليو ٢٠٠٩ يعني من حوالي ٤ شهور.. ماحتاجناش ٢٠ سنة دراسة للقضية زي ما بيحصل عندنا
٢- عدالة الحكم.. تم تطبيق أقصي عقوبة علي المتهم و هي المؤبد (عقوبة الإعدام غير معمول بيها في القانون الألماني) من دون التمييز ما بين مسلم و مسيحي أو عربي و ألماني.. الكل سواسية أمام القانون

Haya ni baadhi ya mafundisho tunayotakiwa kujifunza kutoka kwa makafiri wa Magharibi:
1. Toeni haki haraka: Mauaji yalitokea mwezi Julai 2009, yaani, takriban miezi 4 iliyopita, na haikuwachukua miaka 20 kulichambua shauri, kama ambavyo hufanyika hapa.
2. Haki yenyewe: Muuaji amepokea adhabu ya juu – adhabu ya kifo haimo kwenye sheria ya ujerumani – bila ya kubagua kati ya Muislamu, Mkiristu, Mwarabu au Mjerumani. Wote wako sawa mbele ya sheria.

Na mwisho, Hicham Maged aliandika:

Kilichotokea kwa Marwa kiwe ni mbiu ya ‘kuamsha’ ambayo itawafanya watu wafanye kazi ili kufanikisha, kwa kukosoa vitendo vilivyozidi mipaka ambavyo vinafanywa dhidi ya watu kutokana na imani zao au rangi na kuelewa tofauti zetu na hii inamaanisha kuzizima imani potofu kutoka kwa yeyote dhidi ya yeyote.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.