Marekani: Mauaji ya Fort Hood Yasababisha Kumulikwa kwa Waislamu Walio Jeshini

Shambulizi la upigaji risasi la kushtukiza lililofanywa na mwanajeshi wa Jeshi la Marekani, Meja Nidal Malik Hassan, na kusababisha vifo vya watu 13 na kujeruhi wengine 31 katika kambi ya kijeshi ya Fort Hood, jimbo la Texas, kwa mara nyingine limesababisha Waislamu nchini Marekani kumulikwa – hasa wale wanaolitumikia jeshi.

Kitambo kifupi baada ya Meja Hassan kutangazwa kama mfyatuaji aliyetuhumiwa, kulikuwa na kukosa raha kuliko wazi kabisa miongoni mwa warusha habari na watoa maoni kuhusu usuli wake wa kidini na asili yake. Iliripotiwa pia kwa wingi kwamba wanajeshi wengine wa Kiislamu mara nyingine walikabiliana na mashambulizi kutoka kwa wanajeshi wenzao.

Howard M. Friedman, Profesa Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Toledo, anasema katika blogu yake ijulikanayo kama ReligionClause:

“Jeshi limekuwa likiandikisha Waislamu walio na ujuzi wa lugha na welewa wa utamaduni, vitu vinavyohitajika ili kupigana vita huko Iraki na Afganistani. Hata hivyo, Waislamu walio jeshini sasa wanatiliwa shaka na baadhi ya maofisa wao.”

Bila kujali mashaka dhidi ya wanajeshi Waislamu yaliyokuwapo kabla ya shambulizi hili, mtu anaweza kuwa na hofu kwamba mashaka hayo yamepata msukumo mpya baada ya mauaji ya watu kule Fort Hood. Maswali bado yanaendelea kuibuliwa endapo Meja Hassan alikuwa mwenye siasa kali na ambaye alifanya mashambulizi hayo kwa msukumo wa itikadi ya kidini au labda tu alikuwa na tatizo la kiakili.

Kule Kanada, mwandishi Gwynne Dyer wa gazeti huru la kila wiki la Vancouver kupitia mtandao wa Straight.com, anabuni kwamba kuelekeza fikra kwenye dini ya muuaji ni kufumbia macho baadhi ya masuala mengine muhimu:

“Baada ya siku chache wakati watoa maoni wakisitasita kutoa maelezo yanayoshindana, vyombo vya habari vinaanza kujikita katika maelezo kwamba ilikuwa ni unyanyasaji wa kirangi/kiasili/kidini ndiko kulikomsukuma Nidal kupata ukichaa. Watu wabaya, wanaofanya vitu kinyume na Wamarekani mwisho wa siku ndiyo wenye kuhusika na msiba huo, na kuna mwisho wake.

Maelezo yanayokwepwa ni kwamba vita vya Wamarekani vinavyoendeshwa ng'ambo katika ardhi za Waislamu vinawajenga Waislamu nyumbani kuchukua msimamo mkali. Usijali sana kwamba magaidi wa Kiislamu waliokuzwa nyumbani walioshambulia mfumo wa usafiri jijini Landani mwaka 2005, na wafanya njama wa Kiislamu kadhaa ambao wamekamatwa katika nchi za Magharibi kabla njama zao hazijazaa matunda, wote wamelaumu uvamizi unaofanywa na mataifa ya Magharibi kwenye nchi za Kiislamu kama kitendo kilichowasukuma wao kuwa na msimamo mkali. Zaidi sana, usijali kwamba kile kilichowafanya kuwa na msimamo mkali ni ukweli kwamba uvamizi huo haukuwa na maana kwa masuala ya usalama wa Magharibi.”

Fox News, ambayo mara nyingi hukosolewa kwa kuelemea kwake upande mmoja katika masuala yanayohusiana na uhamiaji na siasa mgando, inasemekana kuitisha wazo la “uchunguzi kwa Waislamu” walio jeshini. Katika tovuti ya Veterans Today, ofisa mstaafu wa Jeshi la Ulinzi wa Pwani ya Marekani, United States Coast Guard, Tom Barnes, anasema chombo hicho cha habari kinachochea mtazamo uleule wa siku zote kwa kujaribu kujenga imani potofu ya “sisi dhidi ya wao”:

“… chombo hicho cha habari kinazidi kuwa “kisichosaidia”, yaani kwa lugha nyepesi, hasa kama swali hili la msingi linageuka kuwa vita nyingine ya Fox Channel dhidi “yao”. Taarifa kama hizi siyo tu zinazidi kupitwa na wakati bali ni za hatari pia. Hapa ndipo palipo na habari nzima.

Kama nilivyoonyesha hapo kabla, jambo kama hili limewahi kutokea katika Jeshi la Ulinzi la Marekani. Ninazidi kuchoshwa na habari za Fox News zinazoniambia kuwa adui zangu ni akina nani. Kila wakati. Bila kukoma. Sikuwa na habari kwamba “wao” wapo wengi!”

Magazeti mengi hivi sasa yanachunguza ni kwa namna gani vitendo vya Hassan vitawaathiri Waislamu wanaotumikia katika Jeshi la Marekani, na wakazi Waislamu wanaoishi karibu na kambi ya Fort Hood.

Hapa kuna taarifa ya habari ya video ya euroamericannews katika YouTube kuhusu maoni ya Waislamu walio Fort Hood kuhusiana na tukio hilo.

Wakati ambapo uchunguzi wa mauaji hayo unaendelea, bila shaka jicho litaendelea kutupwa wa Waislamu wanaotumikia jeshi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.