Kutambulisha Sauti Zinazotishwa


Haijawahi kutokea hapo kabla kwamba watu wengi kiasi hicho wametishwa au kutupwa gerezani kwa sababu ya maneno wanayoandika kwenye mtandao.

Kwa kuwa wanaharakati wengi na raia wa kawaida wameongeza sana utumiaji wa Intaneti ili kutoa maoni yao na kuwasiliana na wengine, serikali nyingi pia zimeongeza ufuatiliaji wa kichunguzi, kujipenyeza, uchukuaji wa hatua za kisheria na unyanyasaji. Matokeo mabaya zaidi ya vitendo hivyo yanapata hasa msukumo wa kisiasa na hivyo kusababisha ukamataji wa wanablogu na waandishi wengine wa mtandaoni kutokana na shughuli zao za mtandaoni na nje ya mtandao, katika baadhi ya matukio ya kusikitisha hata vifo vimetokea. Waandishi wa habari wa mtandaoni na wanablogu wanawakilisha asilimia 45 ya wanahabari walio magerezani duniani kote.

Leo, kitengo cha utetezi cha Global Voices, kinazindua tovuti mpya inayoitwa Threatened Voices, yaani, Sauti Zinazotishwa ili kusaidia kufuatilia unyamazishaji wa uhuru wa kujieleza wa mtandaoni. Inaonyesha ramani ya dunia na mwingiliano wa saa unaosaidia kuonyesha taarifa za vitisho na ukamataji unaofanywa dhidi ya wanablogu duniani kote, na ni mhimili mkuu wa kukusanyia taarifa kutoka katika asasi na wanaharakati walioamua kujitoa muhanga kwelikweli, zikiwemo Committee to Protect Bloggers (Kamati ya Kuwalinda Wanablogu), The Arabic Network for Human Rights Information (Mtandao wa Kiarabu wa Haki za Binadamu kwa Taarifa), Wanahabari Wasio na Mipaka, Shrika la Kuchunguza Haki za Binadamu, Blogu ya Sherika za Mitandao, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari, Kitengo cha Utetezi cha Global Voices.

Mwanablogu yupi, wapi?

Kupata taarifa sahihi kuhusu wanablogu na waandishi wa mitandaoni waliokamatwa ni jambo gumu kwa sababu mbalimbali.

Kwanza, usiri unaotawala udhibiti wa mtandaoni na ukandamizaji unafanya taarifa sahihi liwe jambo gumu sana. Hakuna wiki inayopita bila kuwepo habari za kukamwatwa kwa mwandishi au mwanaharakati mwingine wa mtandaoni katika nchi kama vile Misri au Irani, lakini undani na sababu mara nyingi hugubikwa na utata usioelezeka.

Pili, bado kuna mkanganyiko kuhusu ufafanuzi wa “Mwanablogu” ni nani. Wanahabari mahiri wanazidi kuhamia katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni na blogu ili kutafuta uhuru zaidi, hivyo kufanya ufafanuzi uliokuwepo hapo kabla kuingia ukungu. Na wengi kati ya wale wanaoitwa watukutu wa mitandaoni huko Uchina, Tunisia, Vietinamu, au Irani, hawana blogu zao binafsi. Katika nyakati nyingine, wanablogu hukamatwa kwa sababu ya shughuli zao zilizo nje ya mtandao, kuliko yale waliyoyachapishwa kwenye mtandao.

Mkanganyiko huu mara nyingine umefanya iwe vigumu kwa watetezi wa uhuru wa kujieleza wa mtandaoni kuja na mkakati na ushirikiano wa kuwatetea wanablogu na wanaharakati wa mtandaoni, lakini haikutokea kuwa ni muhimu zaidi kujaribu.

Tushirikiane

Katika Global Voices tunawashirikisha waandishi, wahariri, na watafsiri, ambao hutufahamisha kuhusu ukiukwaji wa uhuru wa kujieleza na haki za binadamu. Kwa kuanzisha Threatened Voices tunakusudia kufungua mchakato wa kutolea taarifa hata kwa mtu mwingine zaidi aliye na taarifa fulani.

Tunatoa wito kwa wale wote ambao rafiki, ndugu, wenzao, au wapiganaji wenzao wametishwa kwa namna moja au nyingine ili kusaidia kutengeneza na kutoa taarifa mpya kuhusu wale waliopotea au waliokamatwa, ili kwamba tutafute vyanzo zaidi ili kuthibitisha na kuunganisha na kampeni za mtandaoni zinazolenga kuhakikisha wanaachiwa huru.

Katika mchakato, tunataraji kujifunza zaidi kuhusu ni lini, wapi na kwa kiasi gani wanablogu wanatendewa vibaya katika nchi mbalimbali, ili tuweze kuwashirikisha taarifa hizi waandishi wa habari, watafiti, na wanaharakati, na kujaribu kupigania uwepo wa Intaneti ambamo kila mmoja anaweza kutumia uhuru wake wa kujieleza, na mahali ambapo wanablogu walio magerezani hawasahauliwi.

Saidia kueneza neno. Twiti, blogu na toa taarifa mpya kwenye facebook kuhusu Sauti Zinazotishwa!

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.