Karibu wakazi milioni 20 wa Cameroon wanakabiliwa na kiwango kinachoongezeka cha unyang’anyi. Majambazi wameweza hata kuyavamia makao makuu ya taifa ya polisi na Wizara ya Mambo ya Nje katika mji mkuu wa Yaounde.
Mwanablogu wa PNT Attitude alitoa uzoefu wake kuhusu jinai katika makala ya hivi karibuni akielezea jinsi mkoba wake ulivyoibwa kutoka kwenye gari yake:
…niliegesha pembeni (gari) ili kununua maembe. Maembe yaliponunuliwa,, nikafungua mlango wa gari ili kuweka maembe kwenye kiti cha nyuma. Hapo hapo ndipo nilipomwona jamaa huyu akishangaa shangaa kwenye upande mwingine wa gari.
Sikumjali. Ghafla alifungua mlango wa abiria, akaupokonya mkoba wangu uliokuwa kwenye kiti cha mbele, na akakimbilia sokoni. Mwanzoni nilifikiri anataka kuteka gari, au alitaka kunifanya nijisikie wasiwasi kwa kuingia kwenye gari? Inawezekana alikuwa na matatizo ya akili? Nilipiga kelele ‘mwizi’ na kumkimbiza nikiwa na maembe, ambayo nilimrushia kabla hajakata kona, na hivyo kunipotea machoni. Ndio, unaweza kudhani sikuwa makini kwa kuacha mkoba wangu pale, kwa taarifa yako, ulikuwa umefichwa chini ya kiti kile kile mpaka nilipofikiri kuwa nimemaliza manunuzi!’
Lakini jambo zuri kwenye habari yake ni kwamba wezi wengine mjini Yaounde wanaweza kuwa ‘wakarimu’. Hata polisi wanajua kwamba kama mtu ana bahati wanaweza kumrudishia vitu vyake binafsi kwa kutembelea sehemu ambayo aliibiwa (kwapuliwa). Kwa hiyo akaendesha mpaka pale:
Niliambiwa kwamba jamaa mwenye mkoba mwekundu alikuja dakika kadhaa baada ya mimi kuondoka na kuuliza “yuko wapi mwanamke ambaye mkoba wake ulikwapuliwa”. Kwa sababu hawakuniona, waliuchukua.
Mimi na rafiki yangu tulimtafuta maeneo ya njia aliyotorokea kwa muda mchache na mtu mwingine akashauri tujaribu kituo jirani cha redio. Tulienda na wahudumu wa mapokezi wakasema: “ndio tulipokea mkoba huu asubuhi ya leo na vitu vilivyomo kwa jina la…Ntemgwa…!” na hvyo ndivyo ilivyokuwa, nilijisikia AHUENI kwamba nimeupata mkoba wangu, akauleta, nikapekua vilivyomo na nikasema kila kitu kilikuwa kama kilivyokuwa timamu, isipokuwa bila shaka fedha na hawala ya kununulia mafuta. Akaongeza “frs 10.000, gharama ya kuutoa”. Nilijaribu kubembeleza punguzo na baadae nikafahamu kuwa kilichokuwa kwenye mkoba kilikuwa na thamani kuliko gharama hiyo iliyoombwa. Hata hivyo niliomba punguzo mpaka frs 5.000 na nikaupata mkoba, nikarudi nyumbani, kwa furaha.”
Baada ya tukio hilo hapa kuna mafunzo aliyojifunza PNT:
-Si wezi wote wana nia mbaya, wengine ni wabahatishaji wenye njaa tu;
-Kuna mtandao ulijpanga wa ujambazi (uchwara) kwenye soko la Mokolo, uwe makini na chochote unachofanya kila mara unapojikuta pale, (mtandao) uliojipanga kwa sababu wanachohitaji zaidi ni fedha zako, na kila mmoja aliye kwenye maeneo hayo anajua wapi unaweza kuupata mkoba wako baada ya tukio, nani ajuye kama kuna zaidi kwenye mpango mzima kuliko kinachoonekana?
-Ni kawaida kushambuliwa kwenye masoko kama haya yenye msongamano wa watu, polisi hawakuutilia maanani mchezo mzima, wakishangaa kwa nini nilikuwa najisikia vibaya, ndio hakuna huduma za kuhudumia waliotharika katika vituo vya polisi kwa sababu ni ‘kawaida’ kuathirika kwa namna hiyo… haggle
-Ninayakumbuka kwa hamu yale maembe na sina lolote dhidi yake;”
Akizungumzia ununuzi wa matunda mjini Yaounde, mfanyakazi wa kujitolea wa shirika la kujitolea la Marekani (U.S. Peace Corps ) anayeblogu kwenye Adventures of Aubrey inaelekea amekuwa akibishana kidogo juu ya bei ya matofaa. Mazungumzo na wauza matofaa kwa hakika yanaibua mengi kuhusu mitizamo inayoambatana na rangi ya mtu ambayo ina mkanganyiko:
Wakati wa safari yangu ya Yaounde juma hili nilienda kununua matofaa mara mbili. Mara ya kwanza nilikuwa nikitembea mtaani na kumwona mtu mwenye mkokoteni wenye matunda. Nikamwuliza bei na nikamwambia hiyo ilikuwa ni bei kwa mzungu na kwamba matunda hayo yalipaswa kugharimu kiasi hiki na kwamba nilitaka kununua matunda mawili kwa kiasi hiki. Akacheka na kushusha bei lakini si sana. Tukazungumza kwa kuvutana dakika chache na mwishowe akataka CFA50 zaidi (kama senti 10) na sikuweza kulipa na ndipo nikachukua mfuko wangu na kupakia matunda yangu na kuacha hela kwenye mkokoteni wake wakati sote tukicheka na kuondoka huku nikisema asante na kwamba ningerudi wakati mwingine (hii ni namna iliyozoeleka ya kumaliza mazungumzo nchini Cameroon –kusema asante, wakati mwingine).”
…Nilimuona mtu mwingine akiwa na mkokoteni wa matofaa nje ya duka la mzungu kwenye mtaa mwingine mjini Yaounde (hilo lilikuwa kosa la kwanza, kujaribu nje ya duka la mzungu). Nikamuuliza matunda hayo yalikuwa yanauzwa bei gani, tukaingia dukani pamoja na rafiki yangu na mama yake, tukarudi na nikaamua ninayahitaji matunda hayo na kuanza kuomba kupunguziwa bei. Akawa na hasira na akaanza kunipigia kelele kwamba kwa nini nilifikiri bei ingepungua –aliniambia bei na alitegemea ningetakiwa kuikubali na blah blah blah. Basi nikacheka nikimwambia, hii ni Cameroon unaomba punguzo kwa kila bei na nikajaribu kuomba anipunguzie. Akakasirika tena. Ndipo, na mimi nikawa mkali. Nikamwambia alikuwa si muungwana na kwamba sijali matunda yake yalikuwa ni bei gani sasa sikuwa na mpango wa kununua kwake tena. Akanikemea kwamba nilikuwa si muungwana kujaribu kuomba kupunguziwa bei wakati nilikuwa tajiri (yaani mzungu). Nikarudia kwamba alikuwa si muungwana na kwamba asingeipata fedha yangu leo na hata siku nyingine na kuondoka. Mwaka mmoja uliopita hali hiyo ingenikasirisha sana lakini sasa ninakimbia kwa urahisi kwenda kukutana na rafiki yangu na mama yake na kusimulia tukio hilo huku nikicheka na kusema kwamba kwamba nilidhani haikuwa siku yangu ya matofaa.”
Badala ya kukimbilia kwenye matatizo ya kupatana bei, labda Aubrey (au yeyote anayepanga kukaa Cameroon) anapaswa kutumia huduma ya simu za mkononi ya kununua vocha za kulipia-kadri-ya-matumizi za simu ya mkononi kama malipo halali. Inaelekea kuwa ni njia rahisi zaidi ya kununua vitu bila fedha taslimu kama mtu atafuata maneno ya PNT Attitude:
Nilikuwa karibu ya kumaliza kununua bidhaa kwenye orodha yangu nilipoamua kwenda kwenye duka la nguo za ndani kutafuta bidhaa iliyokuwa kwenye orodha yangu ya manunuzi kwa muda mrefu: sidiria isiyokiwa na pindo wala waya.
Nilikuwa na bahati sana kuikuta kwenye duka hilo, na kama nilivyokuwa nimeandikiwa, ilikuwa ni ya mwisho iliyobaki na sikuwa nimeiona kwenye duka lingine lolote. Muuzaji akasema iligharimu CFA 4,500. Tazama nilikuwa na CFA 3,500 tu mfukoni! Nilijaribu kuomba kupunguziwa mpaka bei niliyokuwa nayo, bila mafanikio. Nikafikiri kutembea mwendo unaotisha kuelekea kwenye gari na pia uwezekano wa kuwalipa kidogo kidogo kwa kutumia huduma ya kuhamisha salio kwa simu. Chaguo la pili lilionekana kuwa linawezekana zaidi.
Kwa hiyo nikamuuliza kama alikuwa na simu ya MTN ili niweze kumalizia malipo kwa kupitia huduma ya kuhamisha salio kwa simu. Akasema hapana, alikuwa na Simu ya mtandao wa Orange. Hata hivyo akaongeza, “nina rafiki mwenye mtandao wa MTN unaweza kutuma kiasi kilichobaki kwake (CFA 1000). Tatizo limetatuliwa, nikaondoka na sidiria niliyokuwa nimeitafuta sana, nikitabasamu wakati nikiondoka”