Ghana: Siku ya Kublogu mwaka 2009

Siku ya Kublogu, iliyoitwa kwa jina maalum la #bad09 na wanateknolojia pamoja na waliobobea kwenye fani, ni tukio la kila mwaka linalowaunganisha wanablogu wote ulimwenguni kwa kutundika habari zinazozungumzia suala moja katika siku hiyo. Kusudi la tukio hilo ni kuongeza ufahamu na kuanzisha mijadala ya kidunia katika siku hiyo. Siku ya Kublogu mwaka huu ilifanyika Oktoba 15, ambapo wanablogu kote duniani waliandika kuhusu mada ya mabadiliko ya hali ya hewa. Hapa chini ni mkusanyiko wa makala kadhaa zilizotundikwa na wanachama wa Kikundi cha Wanablogu wa Ghana siku hiyo ya Kublogu.

Gameli Adzaho, mwandishi wa Blogu ya The Gamelian World, alitoa makala inayohusu Sauti 5 kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa. Katika makala hiyo alitomasa maoni ya viongozi watano duniani. Katika maoni yake ya kufungua, alizungumzia umuhimu wa Siku ya Kublogu Duniani na jinsi “matukio ya hali ya hewa yalivyoweza kukamata hisia na kupewa uzito ulimwenguni kote katika muongo huu uliopita, kuanzisha mijadala ya sayansi, siasa, biashara na teknolojia.” Viongozi watano wa kidunia aliowajadili walikuwa Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Al Gore, Mshindi wa Tuzo ya Nobeli Wangari Maathai, Rais wa Marekani Barack Obama, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, Rais wa zamani wa Cuba Fidel Castro.

Gameli alihitimisha makala yake na mlolongo wa maswali –“Una maoni gani kuhusu mabadiliko ya Hali ya hewa? Je, mabadiliko haya ni ya kweli? Je, ni ya kusadikika tu? Kwa njia gani unadhani dunia inaweza kutumia raslimali zake kwa uendelevu zaidi? Je, nchi zinazoendelea zinaweza kuchangia katika kubadili mwelekeo wa mabadiliko haya?” – akitegemea kupata majibu mapema.

Makala iliyofuata wakati wa Siku ya Kublogu Kwa Vitendo Duniani ilikuwa ni Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa Afrika (AWDF) ambao wachangiaji ni Bisi na Roselyn wa AWDF. Makala yao ilihusiana na “Mabadiliko ya Hali ya hewa na wanawake”. AWDF ni mfuko wa Afrika nzima wa kutoa misaada kwa wanawake wa ki-Afrika. Maono ya AWDF ni kwa wanawake wa Afrika kuishi katika dunia yenye haki za kijamii, usawa na heshima kwa haki za binadamu za wanawake.

Walianza makala yao kwa kuyapembua maneno yaliyosemwa na Arun Agrawal katika mada yake kuhusu Mitizamo ya kijamii ya Mabadiliko ya dunia, iliyoandaliwa kwa ajili ya Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Benki ya Dunia, Washington, tarehe 5 mpaka 6, mwezi Machi 2008. Katika mada yake hiyo, Agrawal alisema kwamba “mabadiliko ya hali ya hewa yatakuwa nguzo muhimu katika kufafanua upya dhana ya maendeleo katika karne ya ishirini na moja. Jinsi gani mataifa, jamii, jumuiya na familia zitakavyochukua hatua dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na namna mbalimbali ambazo dunia tayari imeshajihusisha nazo kwa namna nyingi zitatapelekea matarajio yao katika mafanikio ukuaji, usawa na uendelevu”.

AWDF inayatazama mabadiliko ya hali ya hewa kama mabadiliko ya mazingira, ambayo yanaharakishwa pia na binadamu –kimsingi likiwa tatizo la mwanadamu. Athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinatarajiwa kuathiri vibaya zaidi (na pasipo uwiano) mwenendo wa maisha, afya, na fursa za kielimu kwa watu wanaoishi kwenye ufukara. AWDF ilitoa maoni yake machache ya namna ya kukabiliana na tatizo.

Kajsa Hallberg Adu, mwanzilishi mshiriki wa Ghana Blogging Group na mwandishi wa blogu ya Rain In Africa, alikuwa na mengi ya kusema katika Siku ya Kublogu Duniani, lakini alistushwa na “namna ambavyo mada hii isivyokuwa na umuhimu katika wakati uliopo nchini Ghana”. Kajsa analalamikia kutokuwepo kwa Ghana kwenye wavuti ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa unaohusu Mabadiliko ya Hali ya hewa na kuuliza: “Kweli, lini mara ya mwisho umesikia mtu akijadili mabadiliko ya hali ya hewa hapa?”

Hata hivyo Ghana ilipewa sifa maalumu na Kasja:

Njia ya kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa ni kuhakikisha tunasafiri kwa usafiri wa umma badala ya kutumia usafiri binafsi kwenye magari yetu. Leo, Waghana wengi wanasafiri kwa usafiri wa umma, taxi za kuchangia au “mabasi vya Kufour ” na hivyo hawatoi sana hewa ya ukaa. Je, tunaweza kusema hivi hivi pia kwa nchi za Kaskazini na Magharibi? Lakini kwa kadri Waghana wanavyokuwa matajiri –lengo letu likiwa kuwa nchi ya kipato cha kati mapema iwezekanavyo –Waghana wengi wanaweza pia kumudu kuwa na magari yao wenyewe.

Kwa maoni yangu tatizo linalojitokeza katika mjadala kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ni kwamba wakati nchi zilizoendelea zinafanya bidii kuwa endelevu, nchi zinazoendelea tayari zipo klimatsmarta, sio kwa kuchagua. Ila “uelewa wa kimazingira” ama maisha endelevu unasababishwa na mada ya mwaka jana; umasikini.

Mwisho, Edward Tagoe, mwandishi wa Blogu ya Tagoe ambaye pia ni mshairi na mtengeneza nyenzo pepe, aliamua kuwashirikisha wasomaji wake wavuti yake nzuri iitwayo YOURENEW.COM. Kwa mujibu wa Edward, wavuti hiyo “ni sehemu muafaka ya kubadilisha ama kuuza simu, kicheza mziki cha mp3, kamera za dijitali na tarakilishi. Unaweza pia kuharibu na kuuza kompyuta za mapajani, michezo ya kompyuta, nyenzo ngumu za kompyuta na DVD. Kama huwezi kupata kifaa chako kwenye orodha ama hatuwezi kukilipia, unaweza kukituma bure na sisi tutakiharibu kw ausalama. Kwa hivyo angalia kifaa chako leo, kuwa kijani na uwe kijani! Kwa hiyo angalia kifaa unachotumia na kuwa kijani!”

Pia zingatia, Oktoba 24, 2009 ni siku iliyopewa jina la Siku ya Dunia ya Kuchukua hatua za Hali ya Hewa na wavuti ya 350.org.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.