Mwezi huu, vyombo vya habari na majukwaa ya habari za mtandaoni nchini China yalijazwa na habari za ushindi wa tuzo ya Nobel katika Fizikia ya Charles Kao. Hiyo ni mara nyingine tena kwamba mwanasayansi wa Kichina anayeishi ng'ambo amejishindia tuzo hiyo yenye kuheshimiwa sana duniani, hata hivyo, furaha hiyo ya muda inaamsha swali la msingi kwamba: Ni lini hasa Uchina itajipatia mshindi wake wa kwanza anayeishi nchini humo wa Tuzo hiyo ya Nobel?
Maoni yaliyotolewa kupitia Xinhua yanaeleza hali hiyo ya kisaikolojia:
Kila mwaka, wakati wa kutangaza mshindi wa Tuzo ya Nobel unapowadia, Wachina hugubikwa na hamasa fulani hivi. Endapo mshindi ni yule wa asili ya Uchina, basi wao hufurahi sana. Lakini mara baada ya kupita siku chache, furaha hiyo huanza kupoa au hata kugeuka na kuwa simanzi. Mwaka unaofuata wakati unapowadia tena, hali hujirudia tena kama hapo awali.
詹晟 alituma swali kwenye blogu ya ifeng:
Baadhi ya watu wamesema ni aina fulani ya ubaguzi dhidi ya Wachina – hakuna tuzo ya Nobel itakayotunukiwa kwa Mchina, itaendelea tu kutolewa kwa watu wenye uraia fulani. Kwa hiyo, sharti la Mchina kushinda tuzo hiyo ni yeye kuchukua uraia wa Marekani. Hivi, kwa nini Wachina wanaweza kushinda tuzo hiyo mara baada ya kubadili uraia wao?
Swali hilo linatoa mwangwi kwenye makala iliyo kwenye blogu ya 青青草香’s sina:
Tunapozungumzia “Mwamerika mwenye asili ya Uchina”, neno la msingi hapo si “Mwamerika” bali ni “Mchina”. Baada ya vyombo vya habari kurusha habari motomoto, tunapata ndoto kwamba Wachina wote tuna nafasi katika tuzo hiyo ya Nobel. Mioyo yetu iliyo laini inapata faraja.
Charles Kao ni Mchina wa nane kushinda tuzo ya Nobel. Ingawa tunajivunia hilo, je, tujiulize swali la kufedhehesha: hivi kwa nini Wachina wanashinda zawadi ya Nobel wanapokuwa katika nchi ya kigeni na si katika nchi yao wenyewe?
Maoni ya 丁果 katika the Southern Metropolitan Weekend yaliainisha baadhi ya matatizo ya kimsingi katika mazingira ya kielimu ya Uchina:
China bado inakosa mazingira huru ya kitaaluma, jambo linalofanya iwe vigumu kukuza na kulea vipaji; China inakosa suhula za kisasa za kufanyia utafiti, jambo linalofanya iwe vigumu kuvutia Wachina kurejea nyumbani kwao; China inakosa mazingira ya kijamii yanayoweza kusaidia kulea fikra makini za kipekee na pia haitoi jumuiya mwafaka ambamo kwamo wanasayansi bora wanaweza kukaa kwa vipindi virefu.
詹晟 na 青青草香 pia walijadili masuala mengine yasiyopendeza.
詹晟 alisema:
Tazama jinsi ufisadi ulivyojikita katika mazingira ya kitaalamu ya Uchina. Wapo wanaoitwa wenye shahada za udaktari wa falsafa vitabu kwa vitabu, kila mmoja akiwa na kati ya vichache mpaka dazeni kadhaa kwa mwaka. Serikali za mitaa zinapenda kuajiri washauri wa kigeni kwa kuwa wanaona kuwa huo ndiyo “mtindo”.
Kama hakuna mazingira madhubuti ya kitaaluma na mfumo wenye ufanisi wa kutambua mchango wa mtu, hata ule utakufu wa kuwa “Mwalimu wa Watu”, wanataaluma wengi watajitoa kwenye ulimwengu huo na kujiunga na ule wa kibiashara.
Tunaweza kulaumu upepo wa mabadiliko nchini China au wimbi la kupenda mali kama sababu za hali hii isiyopendeza. Lakini, je, hali hii haina uhusiano na tamaduni na mitazamo yetu?
青青草香 aling'aka:
China iko makini kutumia namba. Idadi ya tafiti zilizochapishwa vitabu hutumika kuonyesha uwezo wa mtu kitaaluma, au kuamua kama mwanafunzi wa tafiti anaweza kuendelea kufikia ngazi ya kutetea utafiti wake. Katika mfumo huu, walimu na wanafunzi kadhalika hawana budi kuchapisha idadi kubwa ya kazi zao, unaoambatana na matokeo ya uharamia mkubwa wa maarifa yaliyoandikwa na wengine. Wakati ambapo Uchina inaendelea kuwa mzalishaji nambari moja wa tafiti za kitaalamu, huenda pia ni mzalishaji nambari moja wa taka za kitaalamu.
Katika mfumo wa sasa wa elimu na utafiti, ni vigumu kwa Uchina kulelea wanasayansi wabunifu, walio huru na wasiobanwa na chochote. Kuja kutoa mshindi mzawa wa Tuzo ya Nobel ni jambo litakalochukua muda.
Katika blogu ya Kiingereza ijulikanayo kama the Fool's Mountain, nako pia kuna mjadala wa moto kuhusu “Kile kilicho kati ya waandishi wa Kichina na Tuzo ya Nobel”.
[Picha imechukuliwa kutoka nobelprize.org]