Caribbean: Tafakari Mpya Kuhusu Uchapishaji wa Mtandaoni

Baadhi ya vitabu kutoka na kuhusu Karibea. Picha ilipigwa na Nicholas Laughlin, na ilitumwa kwanza chini ya leseni ya Flick ya Creative Commons.

Baadhi ya vitabu kutoka na kuhusu Karibea. Picha ilipigwa na Nicholas Laughlin, na ilitumwa kwanza chini ya leseni ya Flick ya Creative Commons.


Kundi dogo lenye nguvu na linaloendesha blogu za kiuandishi la wanaozungumza Kiingereza huko Karibea limeng'amua uwepo wa mgeni mpya katika mijadala yake. Blogu ya Vitabu ya Karibea iliyoanzishwa na mwandishi wa habari kutoka St. Lucian, Tony Williams, ina lengo la “kuwahabarisha waandishi wa vitabu na wasomaji kuhusu maendeleo ya hivi karibuni katika biashara ya kimataifa ya vitabu na jinsi gani maendeleo hayo yanaweza kuathiri jumuiya za usomaji katika ukanda wa Karibea na visiwa dola vingine vidogovidogo.” Tangu ilipoanzishwa rasmi tarehe 11 Oktoba 2009, Caribbean Book Blog (Blogu ya Karibea ya Vitabu) imeshapandisha mfululizo wa insha zinazotafakarisha na zilizosheheni takwimu kuhusu masuala yanayowakabili wachapishaji, waandishi na wasomaji waishio Karibea, hasa katika kipindi hiki ambapo uchapishaji wa fasihi mahali pengi duniani unahangaika kutokana na matatizo ya kifedha na mabadiliko ya kiteknolojia. Makala za William zimeamsha fikra na mijadala katika sehemu ya kutolea maoni ya blogu hiyo na kwingineko.

Blogu hiyo ya Vitabu ya Karibea ilianza na insha iliyoitwa “Kuvunja pingu”, ambapo ilichambua hali ya uchapishaji katika Karibea na masoko ya vitabu vya Karibea.

… ukizungumza na wapenzi wa vitabu katika Karibea na nje ya Karibea, au ukiduru kwenye kurasa mbalimbali za mitandaoni ambamo mijadala ni fasihi ya Karibea, utakuta watu wakilalama jinsi ilivyo vigumu kupata vitabu vizuri vilivyoandikwa na Wakaribea, yaani iwe katika eneo hili lenyewe au hata katika masoko ya majiji ya nchi zilizoendelea.

… ipo haja ya mabadiliko – mabadiliko makubwa. Vinginevyo, tutajikuta tukikabiliana na hali ambayo malenga wetu wataishia kupoteza hadhi na kuingia katika hali ya uduni na kukosa maana. Ili kukwepa hali hii hawana budi kutafuta njia mpya za kujifufua pamoja na kazi zao.

Katika insha yake ya pili, “Wakati ni huu“, Williams anapendekeza kwamba “kundi la wasomi, wahariri na wasanifu wenye visheni … wanaosukumwa na roho chipukizi na ya kijasiriamali” hawana budi “kuchukua changamoto ya kuunda mahali katika mtandao patapotumiwa na waandishi na washairi wetu wanaohangaika ili kuwasaidia waweze kusimama kwa miguu yao ili kwa upande wao nao pia walete maarifa na msisimko mpya.”

Waandishi kadhaa waishio Karibea wamejiunga kwenye mjadala huo kwa kuacha maoni yao. Mtunzi wa hadithi wa Ki-Antigua, Joanne C. Hillhouse anaandika:

Hiyo inapunguza muda na nguvu ambazo ningewekeza katika kazi yangu ya kuandika, bado najaribu kutafuta mizani, lakini imefika wakati nimekubaliana na ukweli kwamba kujiuza (japo ni neno baya) ni sehemu ya mchakato na kwamba Intaneti inafanya kazi kubwa ya kusawazisha uwanja wa mapambano.

Mshairi wa Kijamaika Tanya Shirley anatoa maelezo yanayounga mkono hoja hiyo hapo juu:

Nafikiri kama Waandishi wa Kikaribea sasa tunaishi katika zama ambapo hatuna budi tuwe mstari wa mbele katika mchakato wa kutafuta masoko kwa kazi zetu na kutumia chochote kile tulichonacho kinachoweza kutusaidia.

Mwandishi wa ki-Jamaika anayeishi Miami, Geoffrey Philp, ambaye pia ni mmoja wa wanablogu wanaondika sana fasihi katika Karibea, anajibu kupitia kwenye blogu yake mwenyewe, akija na pendekezo:

Kinachotakiwa ni tovuti itakayotumia muda wake wote kushughulikia uandishi wa Kikaribea. Jinsi ninavyoitazama tovuti hiyo ni kwamba, itakuwa ni kama nyumba ya kupitisha vitabu vilivyochapishwa na waandishi wa Kikaribea. Wachapishaji wataleta huko katalogi zao, waandishi watapandisha picha zao na tarehe zao za usomaji, wakati ambapo wasomaji wataweza kujiandikisha kupitia RSS, majarida, au barua pepe.

Philp pia anaorodhesha zaidi ya dazeni nzima ya majarida ya mtandaoni kuhusu Usomaji wa Kikaribea, baadhi yake yakiwa ni majarida yaliyopigwa chapa na ambayo yanaendesha kurasa zao za mitandaoni, baadhi yakiwa ni ya mtandaoni pekee. Pamoja na baadhi ya wanablogu wachache waliojitolea na waandishi-wanaoblogu, tovuti hizi, ndivyo anavyopendekeza Philp, huenda zitagetuka na kuwa kiini cha baadaye cha jumuiya ya uchapishaji ya Kikaribea iliyo ya mtandaoni.

Katika miaka mitatu na nusu tangu Global Voices ilipofanya taftishi ya kina na kamilifu kuhusu Usomaji wa Kikaribea katika ulimwengu wa blogu, majarida kadhaa yameibuka, yakiwa ni ya mtandaoni na mara nyingi yakitumia zana za kublogu ili kuchapisha kwa haraka na pasipo gharama. Moja wapo ni tongues of the ocean, ambalo hushughulika na mashairi na huchapishwa kutokea Bahamas kwa kutumia WordPress, lilizunduliwa mapema mwaka 2009, lilipofikia toleo la tatu lilichapisha pia hadithi fupifupi. Mhariri Nicolette Bethel (ambaye pia anaandika katika blogu yake binafsi) alielezea katika mahojiano aliyofanya na Antilles, blogu ya Kikaribea inayopitia vitabu, kwamba alihamasishwa na majarida ya mtandaoni yanayochapishwa kutoka katika pande mbalimbali za dunia:

Nilivutiwa na mfungamano wa vyombo vya habari na majarida haya katika kile yalichotoa, jambo ambalo liliyafanya yawe tofauti sana, yawe na mshawasha zaidi, yaani tofauti na yale yaliyopigwa chapa kwenye karatasi.

Je, nini kilikosekana miongoni mwao? Ni jarida la mtandaoni la Kikaribea kwa ajili ya waandishi wa Kikaribea ambalo litakuwa na rekodi ya kutengeneza na kuchapisha kwa haraka, kitu ambacho kilikuwepo kwenye majarida haya mengine.

Katikati ya mwaka 2009, mradi wa gazeti lingine la mtandaoni ulizinduliwa: Zafra Lit, hili hutafsiri hadithi fupifupi zilizoandikwa na waandishi WaCuba kwenda katika Kiingereza. Gazeti linahaririwa na David Iaconangelo, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Baltimore, huku likiendeshwa katika zana ya Blogger,Zafra Lit linategemea juhudi za wafasiri wanafunzi ambao wanajitolea muda na ustadi wao. Kingine kipya kuingia na kilichozinduliwa mwezi Oktoba 2009 ni Town. Inachapishwa kutokea Trinidad na huchapisha mashairi mafupimafupi na hadithi kwenye mtandao na vilevile mabango maalumu ambayo wasomaji wanaweza kushusha katika muundo wa PDF na kupiga chapa wakiwa nyumbani.

Wanablogu wengine wamejitokeza na kueleza upungufu au kutokuwepo kwa makala makini kuhusu usomaji na utamaduni katika vyombo vya habari vya Kikaribea na hivyo kuzigeuza blogu zao ziwe magazeti ya kuperuzi. Kwenye Tallawah, makala za mwandishi wa habari wa Kijamaika Tyrone S. Reid huwa juu ya mapitio na makala za vitabu, muziki, sanaa na filamu, huku akiwa na lengo la “kushajiisha uwepo wa mijadala inayojenga.” Mwalimu wa fasihi anayeishi New Jersey, Charmaine Valere, anapitia fasihi ya Kikaribea, hasa ile ya KiGuyana kwenye , Signifyin’ Guyana – ambapo katika makala yake ya hivi karibuni alishughulikia swali la “Kwa nini mapitio?” Wakati huohuo, PLEASURE, blogu mpya ya mwandishi wa KiTrinidadi, Andre Bagoo (ambaye pia ana blogu yake binafsi, Tattoo), inashughulikia “sanaa katika miundo yake yote”, ambapo hivi karibuni ilijumuisha mfululizo wa mahojiano yaliyoanza na M-Trinidad mshairi anayeishi Uingereza, Vahni Capildeo.

Pengine ingizo jingine jipya na lenye nguvu katika uwanda wa usomaji wa Kikaribea mtandaoni ni Repeating Islands, blogu ya sanaa na utamaduni inayoendeshwa na wasomi wawili wa fasihi wenye mizizi huko Puerto Rico, Ivette Romero-Cesareo na Lisa Paravisini-Gebert. Jarida hilo linashughulikia fasihi, sanaa ya maonyesho, muziki, sanaa za kuchora, stadi za kitamaduni, na mengine mengi. Repeating Islands hupandisha kati ya makala sita hadi saba kila siku: viungo vya makala na mahojiano, taarifa kuhusu vitabu na maonyesho, and mambo mengine mengi ya kuvutia. Pia linatumia lugha zote zinazotumika katika eneo la Karibea – Kiingereza, Kihispania, Kifaransa, Kiholanzi – kwa kweli blogu hii inafanya kazi ya maana sana ya kusambaza taarifa na fikra. Aina ya mtandao wa uandishi na uchapishaji wa mtandaoni ambao Blogu ya Kikaribea ya Vitabu na Geoffrey Philp wanawazia utahitaji aina hii ya umotomoto na umahiri.

1 maoni

Sitisha majibu

jiunge na Mazungumzo -> Amos Nyambane

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.