China: Mitizamo Potofu Pamoja na Ubaguzi wa Wa-Han Dhidi ya Wa-Uyghur

Ni mwezi mmoja na zaidi umepita tangu machafuko ya Xinjiang ya Julai 5 na wengi wa wanamtandao wa intaneti wa Kichina bado wanazilaumu nchi za Magharibi pamoja na Rebiya Kadeer kwa kuwatetea wale wanaotaka kujitenga huko Xinjiang. Hata hivyo, kuna sauti za minong’ono zinazochepuka hapa na pale katika intaneti ya Kichina, kama vile hii sentensi moja ya maoni katika tovuti ya BBS of people.com, ambayo inadai kwamba machafuko katika Urumqi yalikuwa ni matokeo ya ukandamizwaji wa muda mrefu:

Hapakuwa na sehemu ya kujieleza baada ya kuonewa tena na tena, ghasia imekuwa jibu la mwisho!

Ubaguzi wa watu wa asili ya Han kwa Wauyghur umekuwa ni chanzo cha mgogoro katika China kwa muda mrefu kabla ya machafuko ya mwezi Julai. Ukutafiti katika majadiliano ya mtandaoni kwenye tovuti ya Tianya Forum, kuna hadithi nyingi za mitizamo potofu ya Wahan dhidi ya Wauighur. Hii ni moja ya hadithi hizo:

Hebu nieleze uzoefu wangu binafsi. Wakati wa miaka yangu katika Chuo Kikuu cha Urumqi, kulikuwa na programu maarufu ya televisheni (ya kamera za siri) iliyoitwa “Special 6+1”. Katika kipindi kimojawapo, mtangazaji alimhoji mtu wa Xinjiang kuhusu ombi lake (maoni ya mfasiri: watu wengi wa kabila la Han huwaita Waughur kwa jina la Wa-Xinjiang). Jibu lake, la kustaajabisha, lilikuwa kwamba angelipendelea kuishi katika hosteli mjini Beijing kwa siku chache. Mtangazaji alishangazwa na akauliza sababu. Aliyekuwa anahojiwa alielezea uzoefu wake wakati wa miaka ya mwanzo ya 1990 wakati alipompeleka mwanae mjini Beijing ili akapate huduma bora za hospitali. Katika safari hiyo, walikataliwa na hosteli zote mjini Beijing kwa sababu tu walikuwa ni watu wa Xinjiang.

Tovuti ya people’s Press pia ina habari kama hiyo iliyotokea mwaka 2006:

Katika mkesha wa Krismasi wa mwaka 2006, nilikuwa mjini Beijing. Japokuwa hapakuwa na mgahawa wowote wa pombe ulioweka kibao kinachosema “Wauighur Hawaruhusiwi” kwenye milango yake, nilichunguzwa na walinzi wa usalama kila wakati.

Ukiacha migongano ya kila siku, wengi wanaghafirika kutokana na kutokuelewa na mitizamo potofu ya Wahan. Mchangiaji anayejiita Looking at cloud and water flow, alipayuka katika tovuti ya Tianya forum kwamba yeye ni mtu wa Xinjiang ili kueleza hasira yake dhidi ya mitazamo hiyo potofu.

Ninataka kupayuka kwa sauti kuu kuwa mimi ni Mu-Uyghur!… Kuna wezi mjini Xinjiang, lakini wezi wapo kila mahali. Je inaweza kufikirika kuwa wezi wote wanatokea Xinjiang? Ni wazi kuwa ni rahisi kumtambua mwizi mwenye maumbile yanayofanana na yale ya watu wa kabila dogo. Halafu unahitimisha kuwa wezi wote ni watu wa Xinjiang. Kwa kweli nimetembelea sehemu nyingi nyingine katika bara na nimegundua kuwa Xinjiang ni sehemu yenye usalama zaidi.

Na hata serikali inataka kurekebisha sera ili kuhifadhi lugha na utamaduni wa Uyghur, Wachina wengi wa Ki-Han hawataki kuiunga mkono (sera hiyo). Mfano wa hivi karibuni ni ule mpango wa Serikali Kuu kuwekeza fedha maradufu (Dola za Kimarekani 121 milioni) kwenye mradi wa elimu ya chekechekea kwa lugha mbili huko Xinjiang. Hata hivyo kuna malalamiko mengi juu ya sera kama hiyo:

Mchangiaji Liar Without draft ana hasira kuhusu sera hiyo:

Hata majimbo mengine hayana shule za chekechea za kutosha, kwa nini serikali yetu haifanyi lolote kuhusu hilo?

Shenqike alijibu:

Watoto wanaolia hepata maziwa! Hakuna watoto wanaolia katika majimbo mengine!

Xwni aliongeza,

Watoto wabaya hupata peremende.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.