Kenya inakabiliwa na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa. Ukame huu umeathiri nchi nzima, lakini athari zake zimeonekana zaidi katika jamii ya Kimasai ambayo chanzo zhake cha kwanza cha maisha ni mifugo.
Wakikabiliwa na hatari ya kupoteza mifugo yao wanayoithamini, Wamasai, jamii ya yenye utamaduni wa kuhama-hama inayopatikana kusini mwa Kenya na kaskazini mwa Tanzania, wanaswaga mifugo yao kuelekea kwenye maeneo ya wanyama pori –na hata mijini- katika kutafuta malisho. Jambo hili limeongeza mgogoro kati ya binadamu na wanyama pori kwa kuwa ng’ombe waliodhoofu hujikuta wakishambuliwa na simba pamoja na wanyama wengine walao nyama.
Blogu ya Lion Guardians inaarifu kwamba hapajakuwepo mvua ya maana katika miaka miwili:
Ukame unazidi kuwa mbaya siku hadi siku. Mvua haijanyesha kwa miaka miwili mfululizo, na jamii ya wafugaji wa Kimasai wanaoishi katika ranchi ya jamii ya [Mbirikani] wamehamisha mifugo yao kwa mielekeo mitatu wakitafuta malisho mabichi. Ng’ombe wote wanakondeana mno, na wengine wanakufa.
Predator Aware, kikundi kinachofanya kazi ya utunzaji wa wanyama wala nyama, kinataarifu pia hali mbaya kwenye nyika za Masai Mara na ranchi za Siana sehemu za kusini mwa Kenya. Kwenye blogu ya Predetor Aware wanasema:
Masai Mara na Siana hasa hasa ndizo zinazoishiwa malisho[majani]wakati ambapo haja ya mvua inaendelea. Usiku uliopita kimbunga kidogo kilionekana mahali fulani kwenye hifadhi. Tunategemea kuwa hii ni ishara na mvua zaidi itakuja. Hali hii ya ukame inaongeza mgogoro baina ya mwanadamu na wanayama pori kwa kadri ambavyo utafutaji wa maji na malisho unaelendelea.
Ingawa wanyama pori wana uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na ukame, mifugo inaathiriwa vibaya sana. Wamasai, kwa kuwa kwa asili ni wafugaji wa kuhama hama, watafanya kile walichofanya kwa vizazi na vizazi, watahamisha mifugo yao kutafuta malisho. Imeondokea kwamba maeneo pekee yenye malisho ya wazi ni yale yaliyohifadhiwa kama vile hifadhi na mbuga za taifa. Jambo la kinyume ni kuwa, mbuga nyingi za Kenya zilizo maarufu duniani zilichukuliwa kutoka kwenye maeneo ya asili ya malisho ya Wamasai. Blogu ya Lion Guardians inaelezea mienendo ya makundi ya Wamasaai wanaoishi pembeni tu mwa Hifadhi ya Taifa ya Amboseli:
Kundi la kwanza lilihamisha mifugo yao kwenda Manyara nchini Tanzania. Wengine waliamua kupeleka mifugo yao Hifadhi ya Taifa ya Tsavo-Magharibi, lakini wawamekuwa wakikabiliana na mapambano makali kutoka kwa mamlaka za hifadhi, zinazojaribu kuzuia malisho yaliyopo kwenye hifadhi yasiliwe na mifugo, na kuiacha hifadhi ikiwa tupu.
Baadhi ya wafugaji hao wamesafiri na mifugo yao kwa zaidi ya kilomita 400 wakitafuta malisho na maji. Wengine wameenda kaskazini kuelekea Jiji la Nairobi baada ya kusikia kuwa mvua kidogo ilinyesha majuma machache yaliyopita, wakati wengine wameelekea kusini kuingia Tanzania.
Ukali wa madhara ya ukame huo unaweza kusikika katika maneno ya Ole Lentura, mwanablogu muhimu wa blogu ya Predator Aware. ‘Siku huwa na jua kali na upepo mwingi’, anasema ole Lentura anayeripoti kwamba wanyama pori ambao kiasili ni wala majani wanalazimika kuvamia miti na vichaka wakijaribu kupambana na ukosefu wa majani.
“Wazee katika ranchi ya kikundi wanauelezea ukame huu kama ni mbaya kuliko ukame mwingine wowote, na wakati bei za bidhaa zinapaa, huku bei za kuuza mifugo na bidhaa nyinginezo za nyumbani zinashuka, hali hii inasababisha janga kubwa la chakula” inasema blogu ya Lion Guardians.
Kuhusu Mgogoro wa binadamu na wanyama pori ole Lentura wa blogu ya Predator Aware anasema “Hakuna matukio ya kutaarifu kuhusu mashambulio ya wanyama pori lakini mwanaume mmoja wa Kimasai aliuawa na mbogo mwishoni mwa juma lililopita. Mgogoro huu wa binadamu na wanyama pori hautapungua mpaka hapo tutakapopata mvua ya kutosha.”