- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Msumbiji: Shambulio Dhidi Ya Mgombea Urais

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Msumbiji, Habari za Hivi Punde, Uchaguzi

Wanablogu wa Msumbiji Carlos Serra [1] [kireno] na Paulo Granjo [2] [kireno] waliandika kuhusu shambulio dhidi ya mwanasiasa Daviz Simango lililofanywa kwenye mji wa kaskazini wa bandari ya Nacala. Pamoja na maoni kutoka kwenye ulimwengu wa blogu, chama cha Simango (@mdmwiki [3]), pia kilitumia huduma ya Twita kuandika kuhusu shambulio hilo.

Simango ni Meya wa Beira, na alizindua chama chake kipya cha MDM mapema mwaka huu, baada ya kutofautiana na chama cha upinzani cha RENAMO [4]. Siku chache zilizopita, yeye pamoja na chama chake walithibitisha mipango yao ya kugombea urais na kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwezi Oktoba.
Simango alikuwa anaelekea kwenye mkutano wa chama wakati gari lake lilipotupiwa risasi watu waliokuwa ndani ya umati uliokusanyika ambao walipora silaha za askari polisi.

Alinusurika bila ya kudhurika lakini taarifa za vyombo vya habari zinasema kwamba watu watatu walijeruhiwa, akiwemo polisi. Taarifa za mwanzo kutoka vyombo huru vya habari nchini nMsumbiji zinaashiria kwamba watu waliopiga risasi walikuwa ni wanachama wa RENAMO.