Wamalawi wanapiga kura katika uchaguzi wa Raisi na Bunge. Kikundi cha wanablogu kilipewa mafunzo na PenPlus Bytes, Taasisi ya kimataifa ya Uandishi wa TEKNOHAMA kwa ushirikiano na New Media Insitute kwa lengo la kuangalia na kutoa maoni yao kuhusu uchaguzi huo kwa kutumia blogu, teknolojia ya twita na simu za viganjani.
Hebu na tuziangalie blogu zao, ambazo zimehifadhiwa katika Potal ya chaguzi za Afrika. Poto hii hutoa taarifa za kutosha kuhusu chaguzi mbalimbali katika nchi za kiafrika.
Kwa mujibu wa mwanablogu Eric Chilenje, uchaguzi wa 2009 nchini Malawi utakuwa na ushindani mzito:
Uchaguzi Mkuu wa 2009 utakuwa kati ya chaguzi zile zinazoonekana kuwa na ushindani mzito. Kwa kuanzia tu, tumemwona Kiongozi wa nchi mstaafu Dr. Bakili Muluzi, akizuiliwa na Tume ya Uchaguzi ya Malawi kugombea kwa mara ya tatu kama Rais. Hili lilifanywa na kwa mujibu wa katiba ya Malawi inayoelekeza kwamba Rais atakuwa madarakani kwa vipindi viwili mfululizo peke yake. Suala jingine linalovutia katika Uchaguzi Mkuu wa 2009 ni kwamba tumeona chama cha UDF kinachoongozwa na Dr. Bakili Muluzi kikiunda ‘muungano’ na kile cha MCP cha John Tembo.
Norman Fulatira ana maoni yanayofanana na hayo:
Uchaguzi wa 2009 katika Malawi unaonekana kuwa wa kwanza tangu nchi iingie katika demokrasia ya vyama vingi. Matangazo yanayowanadi wagombea yanaweza kutubashiria ushindani ni mkubwa wakati huu.
Natambua kuwa uchaguzi wa 2009 katika Malawi unabainisha suala la ulafi wa watawala. Hakuna mtawala anayetaja mfumo rasmi wa kiutawala atakaoufuata akiisha kuchaguliwa kushika madaraka ukimwacha labda Bw. James Nyondo mgombea binafsi wa Urais.
McDonald Bamusi anatoa hoja kwamba uamuzi wa vyama viwili vya siasa vya UDF na MCP, kumwuunga mkono mgombea mmoja umefanya mbio hizo za uchaguzi ziwe kali kweli kweli:
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu katika Malawi umekuwa mmoja ya chaguzi zenye ushindani wa karibu sana. Imekuwa hivi hasa kwa sababu ya makubaliano ya UDF na MCP kumwunga mgombea anafahamika kwa jina la John Zenus Ungapake Tembo.
Michael anaonesha kwamba wapiga kura wa vijijini hawawezi kutegemewa katika uchaguzi wa mwaka huu:
Mbio za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zitakuwa zito. Vyama vikuu vya siasa vinaweka mkazo wa kampeni zao katika maeneo ya vijijini. Hawa ndio watu walio wengi. Watu hawa wa vijijini hawatatumika vibaya mwaka huu kwa sababu wanatambua vyema kiongozi mzuri ni nani.
Vyama vya kiraia, Vyombo vya habari na Taasisi za kidini vinafanya wajibu wake muhimu katika kuhakikisha kuwa Wapiga kura wanazo taarifa sahihi kuhusiana na uchaguzi. Hii itasaidia umma kufanya maamuzi yanayotokana na ufahamu wa kutosha kuhusu nani wa kumchagua ifikapo Mei 19.
Wesysylas anaarifu kwamba basi la chama cha DPP kilitwangwa mawe katika Wilaya ya Machinga:
Kama siku moja baada ya matukio yasiyo ya kiungwana kutokea katika mkutano ulioandaliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa UDF Dk. Bakili Muluzi huko Goliati wilayani Thyolo, tukio hilo lilichukua sura mpya pale basi la chama cha DPP kutwangwa mawe wilayani Machinga siku ya Jumatano.
Habari njema ni kwamba, kwa mujibu wa Kamati ya Ushauri wa Haki za Binadamu, kiwango cha matumizi ya nguvu katika kipindi cha kampeni yamepungua ukilinganisha na yale ya uchaguzi wa mwaka 2004:
Kamati ya Ushauri wa Haki za Binadamu (HRCC) imesema viwango vya matumizi ya nguvu katika kampeni cha kampeni za kuelekea maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 19 Mei yamepungua ukilinganisha yale yaliyoshuhudiwa mwaka 2004.
Kipindi cha kampeni kimehitimishwa leo saa 12 asubuhi. Naibu Mratibu wa Taifa wa HRCC Cecilia Mussa amesema mafanikio haya ni uthibitisho tosha kwamba wa –Malawi wameelewa kuwa nguvu si silaha ya kuingiza ajenda binafsi.
Uchaguzi wa 2009 kwa mujibu wa Nicolas Mbonela ni wa aina yake:
Uchaguzi ujao wa tarehe 19 Mei 2009 utakuwa ni wa aina yake tukizingatia maendeleo ya kisiasa ambayo yanatukia nchini.
Washindani katika siasa wanachabangana ili tu kuhakikisha kwamba wanawavutia wapiga kura wa Kimalawi ambao hawana elimu ambao ndiyo sehemu kubwa ya watu na wapiga kura.
Taarifa za hivi Punde za uchaguzi wa Malawi zinaripoti kwamba wamiliki mali wa Malawi wanadai fedha kwa ajili ya mabango yaliyobandikwa katika maeneo yao.
Baadhi ya wamiliki wadogo wa mali hizo huko Blantyre wanadai kama Kwacha 500 kwa mabango waliyowekwa katika maeneo yao ya biashara ama kazi, imegundulika.
Maendeleo hayo yamewashawishi baadhi ya wamiliki kuzitangaza wazi sehemu zao, kama vile bango moja kubwa lililoko kwenye mji mkongwe wa Blatyre lilivyoashiria jumapili asubuhi.
Mojawapo ya maeneo ambayo wanasiasa wanasemekana kuyalipia ni Kituo cha Curios, karibu na jengo la Benki ya Akiba ya Malawi huko Blantyre.
Mmoja wa wauzaji wa kituo hicho alibainisha katika mahojiano kwamba mabango yanayojiuza yenyewe kwenye eneo hilo yalilipiwa, na kwamba kila moja liling’arimu Kwacha 500 kwa vyama vya siasa vilivyoonyeshwa. Mabango hayo yanajumuisha sura za Bingu wa Mutharika na nyingine ya John tembo, anayebeba mwenge wa chama wa MCP katika uchaguzi wa Mei 19.
Jessie Puwapuwa anasema kwamba mwaka 1994 wa –Malawi walipiga kura ili kumuondoa Kamuzu Banda aliyekuwa ametawala Malawi kwa miaka 30:
Kwa jinsi ilivyo, uchaguzi ni wakati ambapo watu hupiga kura zao ili kuwaweka ama kuwatimua watu katika nafasi zao.
Hii ni mara ya tatu wa –Malawi watakuwa wanaenda kupiga kura kumchagua anayegusa mioyo yao. Mwaka 1994 wa –Malawi walikuwa na ari ya kwenda kupiga kura ili tu kukitosa chama tawala cha MCP ambacho kilikuwa kimetawala kwa miaka 30 chini ya kile kilichoitwa “Udikteta wa Marehemu Mheshimiwa Ngazi Dk. Hastings kamuzu banda”. Huu ulikuwa mwanzo wa kutamalaki kwa demokrasia na Rais wa UDP Dk. Bakili Muluzi alikuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa na kisha kuchaguliwa tena mwaka 1999.
Mwaka 2004 Dk. Bingu Wa Mutharika alichaguliwa kuingia katika ofisi hii inayoheshimika kupitia UDF.
Katika makala yake yenye kichwa cha habari “Malawi: Ni Uchumi tu, mjinga we?”, Mujo anaandika, “ Pamoja na kukumbana na upinzani mkali wa pamoja wa kiongozi mkuu wa upinzani na rais mstaafu, mtawala huyu anatarajiwa kushinda kwa mgongo wa kuuinua uchumi”.
Tarehe 19 Mei, wa –Malawi watakuwa wanaenda kupiga kura kumchagua rais mpya. DPP kimekuwa madarakani kwa miaka minne iliyopita na kimemtengenezea njia Rais Bingu waMutharika kuwa mgombea wake kwa mara nyingine.
Ingawa wapinzani wake wanamlaumu Mutharika kwa kujitengenezea njia ya kuingia Ikulu, anasifiwa kwa kuuboresha uchumi wa Malawi. Tangu atwae madaraka, nchi imeshuhudia uchumi ukikua kwa wastani wa asilimia 7.
“ Alirithi hali mbaya sana kisiasa na uchumi uliodorora…na ilikuwa kazi ngumu kuiendesha nchi, kurudisha imani ya watu muhimu wa nje,” alisema Dimpho Motsamai, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Taasisi ya majadiliano ya Kidunia ya Afrika Kusini anayejikita nchini Malawi.
“Kwa hiyo maono yake yalikuwa kuufufua uchumi, kulinda vyanzo vya kiuchumi –uthibiti wa dhati vya vyanzo vya uchumi –na utakaoshughulika na matabaka ya kijamii na kiuchumi nchini Malawi,” alikiambia kipindi cha Reuters African Journal.
George Kanyange anategemea kuwa uchaguzi wa 2009 utakuwa uchaguzi unaosisimua zaidi katika historia ya Malawi:
Uchaguzi wa mwaka huu unaonyesha bayana kwamba utakuwa wenye msisimuko kuliko kawaida nchini Malawi. Kuna sababu zinazoufanya uchaguzi wetu kuwa wa pekee. Kwanza ni ukweli kwamba mmoja wapo ya vyama muhimu kabisa vya siasa vinavyogombea katika uchaguzi huu ni chama tawala, DPP, ambacho hakikuwahi kamwe kuchaguliwa na wananchi kutwaa madaraka. Na jambo lingine linalovutia ni kwamba chama tawala cha zamani, UDF hakina mgombea wa Urais baada ya kiongozi wake, Bakili Muluzi kukataliwa na Tume ya Uchaguzi, ikikilazimisha kuungana na chama kingine kikubwa cha upinzani, MCP ambacho nacho ni kikongwe kuliko vyote nchini.
Vyombo vya habari havijapewa umuhimu kwenye Ilani za vyama, anaandika Big Up:
Wagombea wote saba, katika uchaguzi mkuu wa Juma lijalo, wameonja joto la jiwe, kwa kutokuingiza jambo lolote linaloonekana, kuhusu vyombo vya habari katika ilani zao. Hawa ni pamoja na John Tembo wa MCP/UDF, Bingu wa Mutharika wa DPP, Dindi Gowa Nyasulu wa afford, Loveness Gondwe wa NARC, Stanley Masauli wa RP, Kamuzu Chibambo wa PETRA na mgombea binafsi James Nyondo. Hii imewafanya baadhi ya waandishi wa habari kuwauliza maofisa wa kisiasa nchini ikiwa wanathamini vyombo vya habari kama Mhimili wa nne ama la, kwa mujibu wa katiba.