Uchaguzi Malawi: Utabiri wa Wataalamu wa Mambo Wageuka Batili

Wakati uchaguzi umekwisha na rais aliye madarakani Bingu wa Mutharika ameshaapishwa kwa muhula wake wa pili na wa mwisho, wanablogu wa Malawi (mabloga) bado wanashangaa kuona maendeleo kinyume na utabiri wa wengi, haswa ule watalaamu wa mambo. Utabiri wa kwanza ulikuwa kwamba ushindani ungelikuwa wa karibu sana. Haukuwa. Pili kulikuwa na mtazamo kwamba Wamalawi wangepiga kura kwa kufuata mistari ya ukabila. Hawakufanya hivyo. Masuala mengine ya uchaguzi ambayo yalikuwa yakijadiliwa na wanablogu au “Mabloga” yalijumuisha namna ambavyo redio za kwenye mtandao wa intaneti zingeweza kuwapasha Wamalawi waishio ughaibuni habari kama zinavyotokea, kadhalika jinsi bunge jipya litakavyokuwa, je nini watakachofanya wabunge wengi wapya ambao wana shahada za za uprofesa wa chuo kikuu pamoja na kazi za kimataifa, wenye shada za falsafa, kadhalika shahada nyingine za juu.

Blogu ya Chingwe’s Hole inatoa maoni juu ya utabiri ambao haukutokea, kisha anachambua orodha ya mambo sita ambayo yameufanya uchaguzi wa mwezi Mei 2009 kuwa wa kihistoria. Kwa mujibu wa Chingwe’s Hole, miundo mikuu ya taasisi za Malawi ilifanya kazi nzuri. Na pia kuhusu uwezekano wa mwisho wa shughuli za kisiasa kwa kiongozi wa chama cha Malawi Congress Party (MCP) mwenye umri wa miaka 77, Bwana John Tembo, uchaguzi huu pia ulihitimisha zama za viongozi wa kiuzalendo ambao wametawala Malawi kuanzia mwaka 1964, jambo ambalo Paul Tiyambe Zeleza pia ameling’amua. Imedaiwa kwamba Bwana Tembo amependekezwa kuwa mgombea wa MCP katika uchaguzi ujao wa 2014, kwa mujibu wa Chris Banda kwenye mtandao wa Malawitalk. Suala la tatu analozungumzia Chingwe’s Hole ni kuwa namna ya upigaji kura ilisukumwa na masuala ya maendeleo dhidi ya wajihi wa wagombea, kadhalika dhidi ya ukabila. Suala la nne na la tano la kihistoria kuhusu uchaguzi huu kwa mujibu wa Chingwe’s Hole. Suala la mwisho linazungumzia jinsi wataalamu wa mambo walivyokisia vibaya uwezo wa mpinzani mkuu, John Tembo, haswa matokeo ya mseto alioingia na chama cha United Democratic Front (UDF). Kuhusiana na suala hili Chingwe’s Hole anakosoa:

Na hatimaye uchaguzi umeonyesha utupu wa wataalamu wa mambo ya kisiasa nchini Malawi. Wataalamu wetu wa kisiasa wanaonukuliwa sana hawajui ni nini wanachokizungumzia… wanashupalia kuchambua siasa kwa mitazamo ilei le ya kizamani na walionekana kusimamisha maono yao kwa hulka badala ya utafiti na tabaruku. Ungewasikiliza ‘wataalamu wetu wa mambo ya siasa’ mseto wa vyamba vya upinzani ulipaswa kushinda kwa kishindo kikuu; uchaguzi ungekuwa wa ushundani wa karibu”. Bingu alifanya makosa makubwa kwa kumchagua mtu kutoka kusini kuwa mgombea mwenza; kukua kwa uchumi hakujawanufaisha Wamalawi n.k….

Kama mmoja wa wachambuzi wa mambo amabye alitabiri ushindi wa MCP/UDF na mgombea wake John Tembo, Boniface Dulani anakiri wakati kura zilipokuwa bado zinahesabiwa wakati ilipodhihirika kwamba Bingu wa Mutharika anageuza yale yaliyokuwa yakitarajiwa:

Lazima nikiri kuwa sikutegemea ushindi unaoanza kudhihirika kutokana na matokeo ya upigaji kura ambayo yanatangazwa hivi sasa. Kwa kila hali, inaonekana kuwa Mutharika anaelekea kuibuka na ushindi mithili maporomoko ya ardhi. Wakati Bingu anafanya vizuri kwenye majimbo ya kaskazini kama ilivyotabiriwa, kadhalika nafanya vizuri katika majimbo ya kati na kusini.

Kwa mwanablogu Greenwell Matchaya, ushindi wa rais aliye madarakani nchini kote unaweza ukawa unaashiria mwisho wa siasa za kikabila:

Kwanza, ushindi mkubwa wa Bingu mbele ya mseto wa nguvu wa upinzani ni ushindi wa kwanza kuusikia katika Afrika. Zaidi ya hapo, ukweli kwamba hapakuwepo na tuhuma zozote za wizi wa kura, kunaufanya ushindi wake uwe wa haki na wa kuvutia. Chama cha Bingu, DDP, kimeshinda uchaguzi wa rais kwa kura takriban 2,730,630 wakati mseto wa MCP/UDF uliambulia kura 1,270,057, kura takriban 200, 000 pungufu ya zile za Bingu […]. Ujumbe mkuu unaotolewa na takwimu hizi ni kuwa Bingu alichaguliwa na taifa zima, na unazua wazo kuwa pengine uongozi bora unaweza kutokomeza sarakani ya ukabila ambayo wengi wetu tulidhani ilikuwa bado inazengea kutafuna siasa na maisha yetu.

Clement Nyirenda pia anatoa maoni kuhusu jinsi ambavyo wachambuzi wa mambo walivyokosea kutabiri, na anadhani kuwa upigaji kura uliompa ushindi rais aliye madarakani ulikuwa ni wa kihistoria:

[…] Wataalamu wa mambo walidhani kuwa john Tembo angepata kura nyingi kwenye majimbo ya kusini wakati angemshinda kabisa Mutharika kwenye majimbo ya kati, ambayo ni ngome ya MCP. Mutharika alitarajiwa kupata ushindi katika majimbo yenye watu wachache ya kaskazini.

Mwisho wa yote, wataalamu wa mambo wamedhihirika kuwa wamekosea kwa sababu Dr. Mutharika alitangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura. Tangu kuanza kwa mfumo wa demokrasi ya vyama vingi, sijawahi kuona kuona mgombea urais akipata kura kutokea kona zote za nchi kama hivi.

Na maneno ya kuhimidi yanaendelea na Cryton Chikoko ambaye anaandika katika nafsi ya tatu kwa kutumia jina la bandia la “Rambler”:

Rambler anakiri kuwa alikuwa hatarajii Wamalawi kupiga kura kwa kufuata sifa za mgombea. Rambler alifikiria kwa makosa kwamba kama livyokuwa katika chaguzi zilizopita siasa za majimbo zingetawala. Uchaguzi wa 2009 umekuwa ni staajabu ya kuvutia. Upepo mpya katika siasa yetu.

Victor Kaonga anaienzi kazi ambayo idhaa za redio ziliifanya katika kuwapasha watu habari za matokeo wakati wa kusubiri Tume ya Uchaguzi ya Malawi (kutangaza matokeo). Katika mtandao wa Malawian Internet listserv, inashukuriwa kazi ambayo redio ilifanya hasa stesheni ya Zodiak Broadcasting, ambayo inatangaza katika Malawi yote, na hivi karibuni ilianza kutangaza moja moja kwenye mtandao wa intaneti. Listserv pia imejadili namna ambavyo bunge jipya litakavyokuwa, hasa ikizingatiwa kwamba kuna idadi kubwa ya wasomi wa kimalawi ambao wamechaguliwa kuingia bungeni, jambo ambalo pia lilijadiliwa na Chingwe’ Hole. KAtika mtandao wa Nyasanet, swali la ni nani atakayechaguliwa kwenye baraza la mawaziri linajadiliwa katika msingi wa wasomi waliochaguliwa kuingia kwenye baraza la wawakilishi, ambalo linafananishwa na kongamano la wasomi. Mwanablogu Kondwani Munthali ameshatoa baraza lake la kufikirika la Mawaziri.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.