Tajiri Wa Kimisri Ahukumiwa Kifo

Wamisri walishuhudia hukumu isiyotarajiwa katika historia ya vyombo vya sheria nchini humo: Bilionea Hesham Talaat Moustafa, pamoja na mamluki wake (mpiga risasi wa kukodi) Mohsen El Sokari wamehukumiwa adhabu ya kifo kutokana na kuhusika kwao katika mauaji ya mwimbaji wa Kilebanoni Suzanne Tameem. Mauaji hayo ya kinyama yalitokea huko Dubai, UAE, na hukumu iliyotolewa Alhamisi imesababisha mshtuko na mshangao wakati wanablogu walipojaribu kukubaliana na yaliyotukia.

Mwanablogu anayeandika sana wa Kimisri, Zeinobia alitangaza habari:

Mnamo tarehe 21 Mei, Hakimu Muhammadi Qunsuwa alitangaza kuwa kesi hiyo itapelekwa kwa Mufti Mkuu Ali Gomaa, Kiongozi wa juu zaidi wa Kidini nchini humo, ambaye angetoa hukumu ya kifo kwa Moustafa siku ya tarehe 25 Juni.

Kama ilivyomstaajabisha kila mmoja, hukumu hiyo pia ilimuacha mshtakiwa akiwa na mshangao. Mwanahabari Ahmed El Desouky alikuwa ni mmojawapo wa watu wa kwanza kuandika maoni ya watu mahakamani kwa ajili ya jamii ya Wamisri katika mtandao wa intaneti, alisema:

Kulikuwa na ulalamishi mahakamani baada ya sentesi kusomwa na wale waliohusika walionyesha hasira kali na mshangao wakieleza kuwa hukumu ile ilikuwa ni kali kupita kiasi. Maoni yalitofautiana nje ya jumba la mahakama, ambapo watu wengi waliiona ile adhabu ni stahiki kwa mtu ambaye aliyatumia mamlaka, ushawishi na pesa zake vibaya, akifikiri kwamba alikuwa yuko juu ya sheria.

Maoni yalikuwa yakipishana, kati ya kukubali na kuiunga mkono ile hukumu na huruma pamoja na huzuni. Katika makala yake, Desert Cat alishangazwa na ukweli kwamba Moustafa na El Sokary walipewa hukumu inayofanana:

Kwa masikitiko hukumu imetolewa leo kinyume na vile kila mmoja alivyokuwa akitarajia na kesi hiyo hivi sasa inapelekwa kwa Mufti Mkuu. Baada ya kusomwa kwa hukumu, mushkeli ulizuka mahakamani, huku wanafamilia wa Mohsen na Hesham wakipiga mayowe kadhalika wafanyakazi wa kundi la Talaat Moustafa, ambao hawakuamini kile walichokisikia. Wakati huo huo Hesham na Mohsen walikuwa kimya kabisa. Binafsi, sikuamini kwa sababu kosa la Hisham lilikuwa ni kuchochea mauaji wakati Mohsen ndiye aliyeua. Iweje adhabu zao ziwe sawasawa?

Ahmed Shokeir alijibu swali hilo katika sehemu ya maoni ya ujumbe ule kwa kusema:

Katika sheria nyingi, adhabu ya wale waliotoa wazo la jinai ni sawasawa na ile ya watekelezaji. Katika baadhi ya sheria, adhabu huwa kali zaidi kwa mchochezi kuliko kwa mtekelezaji.

Wanaomuunga mkono mfanyabiashara huyu tajiri wa majengo nchini Misri kwenye huduma ya Facebook, waliijibu hukumu ile kwa kuanzisha kundi la “Muachieni Heshaam Talaat Moustafa.”

Ashraf Elmanwaty alisema:

Bado nina matumaini kuwa HTM ataachiwa huru… Hii ni hukumu iliyovuka mipaka

Wakati Miral El Ramlawy aliandika:

Asilimia 90 ya Wamisri hawaamini kuwa alifanya na mahakama inapaswa kuwaeleza Wamisri msingi wa hukumu hii!!! Simu ambazo hazionyeshi ujumbe ulio wazi siyo USHAHIDI… tunasubiri ufafanuzi!

Baada ya mshtuko, uchambuzi ulianza kuchukua nafasi. Zeinobia alifafanua:

Ikiwa Hakimu anasema kuwa mafaili ya mkosefu yatapelekwa kwa Mufti Mkuu kwa ajili ya ushauri inamaanisha katika mazingira mengi kwamba mkosefu atakutana na adhabu ya kifo. Adhabu ya kifo inahitaji maoni ya Mufti Mkuu ili kuiunga mkono kutokana na mtazamo wa kidini, mtazamo wa Sharia ili kuitimiza hukumu. Siyo kila siku watu hutoa adhabu ya kifo kwa yeyote.
Katika kesi nyingi, kama siyo zote Mufti Mkuu hukubali na kuunga mkono hukumu ya hakimu.

Na anaendelea:

Pili katika kesi ya Hisham na Sokary, hakimu atatangaza hukumu ya mwisho tarehe 25 Juni 2009, karibu mwezi mmoja na siku 5, naamini ni muda mrefu kusubiri adhabu ya kifo.
Tatu, wakati ambapo hakimu atatangaza hukumu ya mwisho, mawakili wa mtuhumiwa watakuwa na haki ya kukata rufaa.

Kwa hiyo panaweza kuwa na duru la pili, jambo ambalo tutalifahamu siku ya tarehe 25 Juni.

Wakati huo huo, kuna maswali na mashaka juu ya biashara ya majengo ya Hisham. Blogu ya Middle East Intitute inaripoti:

Kundi la Talaat Mustafa (TMG), ubia mkubwa wa biashara ya majengo ambao Mustafa alitengeneza mabilioni, hautaki wadau wahofu kwa sababu tu mwenye kampuni amehukumiwa adhabu ya kifo. Kundi la TMG limewahakikishia wawekezaji:
Sawaftah alisema kwamba muundo wa kiufanisi wa TMG utakinga athari zitakazotokana na ‘kutokuwepo kwa mtu mmoja’.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.