Serikali ya Sri Lanka imetangaza kwa kupitia vyombo vya habari vya taifa pamoja na ujumbe wa simu za mkononi mchana leo (Jumatatu, 18 Mei, 2009) kwamba kiongozi wa Kundi linalotaka kujitenga la Wa-Tamil, the Liberation Tigers of Tamil Eelam (LTTE), Vellupillai Prabhakaran, amefariki. Vyombo vya habari vinaripoti kwamba Prabhakaran, ambaye alikuwa kwenye uongozi wa moja ya maasi ya kikatili zaidi duniani, aliuwawa kwa kombora wakati alipokuwa kwenye basi dogo na mkuu wa jeshi la majini la LTTE, Soosai, pamoja na mkuu wa upelelezi, Pottu Amman. Mwili wa kiongozi huyo wa waasi utafanyiwa uchunguzi zaidi wa DNA ili kuthibitisha utambuzi wake. Kadri ya wanachama 250 wa waasi wa Chui wa Kitamil waliuwawa kwenye mapambano ya mwisho ya vita vilivyodumu kwa miaka 26.
Salamu za rambirambi zinaashiria kwamba alikuwa shujaa kwa baadhi ya watu kadhalika alichukuliwa kama muuaji katili kwa wengine. Chombo cha habari cha BBC kimeandika, “kwa wafuasi wake, Vellupillai Prabhakaran alikuwa ni mpigania uhuru kwa ajili ya ukombozi wa Watamil. Kwa maadui zake alikuwa ni mtu msiri anayependa kutawala na asiyejali kabisa maisha ya wanaadamu wengine.” Gazeti la The Hindu nchini India linasema, Mpigania uhuru kwa wafuasi wake na gaidi wa kuogopwa kwa wengine, Prabhakaran alikuwa anatafutwa na Chombo cha Polisi cha Kimataifa, Interpol, pamoja na mashirika mengine mengi tangu mwaka 1990 kwa makosa ya ugaidi, mauaji na jinai. “kabla dunia haijamsikia Osama Bin Laden au Al-Qaeda, Prabhakaran alianza kutumia mbinu mpya ya vita, mabomu ya kujilipua kwa kujitoa muhanga. Makala hii kwenye gazeti la Tehelka inatoa mwanga kuhusu kiongozi huyu wa vita.
Mwanablogu wa Beyond the Skin anafafanua hivi:
Hisia za mwanzo: WHAAA! [vipele vya baridi, kushuka tama na hisia mchanganyiko za hjofu na ahueni.]
Hisia zilizofuata: Sasa nini? Baada ya miaka 26 ya mapambano, baada ya kuua mamia ya maelfu, baada ya kuwanyamazisha wale walioipinga serikali na waasi wa LTTE kwa kuwaua, mateso na watu kupotea, sasa itakuwaje kwa watu wa Tamil?
Kada wa chama cha United National Party Ajith P. Perera ameandika salamu za rambirambi kwa Prabhakaran katika blogu yake, akitaka kuwa tofauti na wengine: “alikuwa muuaji, bila ya shaka, lakini Prabhakaran anastahili salamu za rambirambi, hata kama ni katika lugha ambayo alikuwa haielewi,”
Je alifanikisha lolote la maana kwa ajili ya jamii yake? Jibu ni HAPANA. Watamil wazawa (Jaffna) wako pabaya zaidi ya pale walipokuwa katika miaka ya 1970. Zaidi ya nusu ya Watamil wamehama moja kwa moja. Watamil Wazawa, kundi kubwa la walio wachache nchini Sri Lanka wakati ule, hivi sasa wapungua na kuchukua nafasi ya tatu baada ya Waislamu na Watamil wanaotokea India. Jaffna, jiji la pili kimaendeleo nchini Sri Lanka, na mfumo wake maarufu wa elimu, hivi sasa iko nyuma sana. Kama jamii, Watamil, wale walio na bahati mbaya ya kubaki, wamerudi nyuma miaka kumi au ishirini. Walitambuliwa kama magaidi duniani kote. Kaskazini na mashariki pamekuwa tegemezi kwa Colombo kiuchumi. Kwa miaka michache ijayo, mpaka hapo serikali ya UNP itakapotekeleza sera zake kisiasa, watakuwa wanaendeshwa kutokea Colombo. Yote haya ni shukrani kwa Prabhakaran.
Mwanaharakati wa Kitamil na mwanachama wa zamani wa waasi wa LTTE Nirmala Rajasingam anafafanua katika makala kwenye gazeti la Independent kwamba dada yake aliuwawa na waasi wa LTTE miaka 20 iliyopita.
Kwa sababu hiyo, habari za maangamizi ya uongozi wa juu wa LTTE – ambao uliamuru kuuwawa kwake pamoja na Watamil wengine wengi waliowapinga – kumeleta ahueni kubwa sana. Vita na ukatili hatimaye vimesitishwa na kumwagika kwa damu za Watamil kumefikia mwisho.
Hata hivyo anaonya:
Pingamizi linaloendela la kutoruhusu mashirika ya misaada ya kibinaadamu kuingia halisaidii kupunguza mashaka juu ya nia ya serikali kwa wakimbizi na makada wa LTTE ambao wamesalimu amri. Katika miaka mitatu iliyopita kumekuwa na matukio mengi ya utekaji, mauaji na kutoweka kwa watu, kulikolenga jamii ya Watamil wakati ambapo serikali ya Sri Lanka ilipokuwa ikitekeleza kampeni yake ya kijeshi. Kushamiri kwa uongozi wa kijeshi kitaifa na kwenye jamii kumefanikisha ukandamizwaji wa maoni mbadala kusini mwa nchi, na kumewezesha mashambulizi dhidi ya wanahabari. Tunasuburi ili tuone kama serikali itageuza mwelekeo huu mbaya wa utawala wa kidemokrasi.
Akiwa safarini, mwanablogu na mwandishi wa makala Indi Sumarajiya ametumia zana ya Twita kujadili kifo cha Prabhakaran. Alituma jumbe kadhaa kwenye ukurasa wake wa Twita jumatatu mchana:
Nipo Hambantota. Fataki. Pengine Prabhakan amefariki. Hakuna utukufu kwenye kifo, lakini, ni vyema. Tunaomba Sri Lanka ijijenge upya#fb
Wanawasha baruti karibu kabisa na ghala ya mitungi ya gesi. Wauza samaki wanahimizwa kurejea kazini.
Mji wa Hambantota una Waislamu wengi, kazi inaendelea. Misafara ya bendera katika Ambalantota. Vita vimekwisha, Prabha amekufa. Idumu Sri Lanka #fb
Mwanablogu aliyeko mjini Chennai, India, Prahalathan KK, anasema kuwa kushangilia kifo cha Prabhakaran ni utovu wa heshima kwa raia waliouwawa katika harakati za kuwezesha maangamizi ya LTTE.
“Kwa hiyo Prabhakaran gaidi ameuwawa. Mmefurahi? Mnashangilia? Je mmeweza kuwafikiria maelfu ya Watamil wasio na hatia ambao waliuwawa kutokana na matumizi ya jumla ya makombora na silaha za sumu yaliyofanywa na jeshi la Sri Lanka wakati wa vita hivi vya kimbari?
Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya ulinzi, karibu ya raia 150,000 ambao walikimbia uwanja wa vita wanatunzwa na na jeshi. Lakini Kamati ya Kimataifa ya Hilali Nyekundu (ICRC), shirika huru pekee ambalo liliweza kuwafikia raia katika eneo la mgogoro, liliita hali iliyokuwepo kama “si jingine zaidi ya balaa.” Leo hii, wamesema katika taarifa yao kwa vyombo vya habari kwamba hawajaweza kuwafikia raia walioko kaskazini-mashariki kwa siku tisa. “Hii ni dharura kwani hakuna msaada wowote wa kibinaadamu ambo umeweza kuwafikia wale wanaouhitaji kwa zaidi ya wiki moja’” alisema mkurugenzi wa mipango, Pierre Krähenbühl. Selvarasa Pathmanathan, mkuu wa kitengo cha Diplomasia cha LTTE, alitoa tamko Jumapili kuwa Chui “tutanyamazisha bunduki zetu ili kuwanusuru watu wetu.” Alisema kuwa raia 3,000 walifariki na wengine 25,000 walijeruhiwa.
Blogu maarufu ya Waasia wa Kusini Ughaibuni Sepia Mutiny inaripoti maandamano yanayoendelea nchini Kanada. Katika makala inayohusu maandamano huko Winnipeg, Melvin anaandika:
Walibeba mishumaa, mabango, bendera nyeusi na picha za watotot ambao wanawachukulia kama waathirika wa mashambulizi ya serikali ya Sri Lanka dhidi ya raia. Wakati ambapo watu jijini Colombo walikuwa wakisherehekea mwisho wa miaka 25 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, wale waliokuwa kwenye maandamano walikuwa wanaomboleza vifo vya raia wasio na hatia huku wakijiuliza, ni nini, kuma kuna chochote, kilichopatiwa ufumbuzi. “haijasuluhisha lolote,” alisema Singaraja. “Kero za wananchi hazitaisha. Serikali ni katili mno. Hawataki kutupatia haki zetu. Na kama ni hivyo, matatizo yataendelea.”
Maandamano yamekuwa yakiendelea jijini London, katika sehemu nyingi za Canada na hivi karibuni nchini Australia. Mwanaharakati Rajasingham anaonya kwenye jarida la Foreign Policy kwamba Watamil walio ughaibuni wamechukulia vibaya ujumbe wake:
Wakati mgogoro wa kibinaadamu unavyojitokeza nchini Sri Lanka, jumuia ya kimataifa inabidi itoe tamko wazi na la moja kwa moja. Kwamba waasi na Watamil wanawaunga mkono ambao wanaishi ughaibuni hawana hati miliki ya kuwa “wawakili pekee” wa Watamil wote. Na kujitenga siyo suluhisho pekee. Njia nyingine yoyote isipokuwa mapambano imara kungetumiwa na waunga mkono wa LTTE walio nchi za magharibi – na kuwachochea wazalendo wa Ki-Sinhala nchini Sri Lanka. Ni ujumbe huu imara pekee ambao utapelekea amani na demokrasia.
Kwenye tovuti ya Moving Images, Moving People! Mwanablogu Nalaka Gunawardene anasema kuwa angependa kuamini, kwa hakika, kuwa vita vimekwisha:
Hakuna vidhibitisho huru – vimekuwa ni vita visivyokuwa na shahidi kwa miaka michache iliyopita. Lakini nipo tayari kuwa na imani isiyo ya kawaida, ikiwa kama ni hilo tu linalohitajika ili kukaribisha amani iliyotuchenga kwa muda mrefu. Nitakwenda mpaka mwisho wa dunia, ili kusimamisha kutoamini kwangu, ili kupokea kurejea kwa amani na amani yenye maana.
Rais Mahinda Rajapaksa anategemewa kulihutubia Bunge na taifa jumanne asubuhi.