Saudi Arabia: Je, mafua ya nguruwe yatatishia Hija?

Kila mwaka mamilioni ya Waislamu husafiri kwenda  Maka kuhiji, moja ya nguzo tano za Uislamu. Je, msimu wa hija ya mwaka huu utatishiwa na homa ya mafua ya nguruwe? Wanablogu wanayo maoni ya kusema.

Kwenye blogu ya CrossRoads Arabia, John Burgess anaeleza:

Mtafiti wa Kisaudi katika sheria za Kiislamu (Sharia) amegundua kuwa kuna uwezekano wa kuwazuia baadhi ya mahujaji (wale ambao walishahiji kabla yaani, mahujaji wa ‘kurudia’) hasa wanaotoka maeneo ambayo kwa sasa yanatishiwa na mlipuko wa mafua ya nguruwe. Nina hisi kwamba wazo hili linakuja sasa kwa sababu ya Haji ambayo itafanyika mwishoni mwa mwezi Novemba. Hija ni wajibu wa msingi, ambao kila Mwislamu hutakiwa kuutimiza angalau mara moja katika maisha yake, inapowezekana.

Hali kama hii ilijitokeza miaka michache iliyopita, ambapo homa ya mafua ya ndege (H5N1) ilikuwa tishio. Msomi mmoja wa Kisaudi alitoa wito wa kuifuta Hija ikiwa mlipuko ungekuwa mkubwa zaidi, lakini pendekezo hilo lilizimwa na wenzake. Hoja ilikuwa kwamba Hija haijawahi kufutwa kwa minajili tu ya kiafya na kwamba kufanya hivyo kungekuwa kuukiuka Uislamu. Badala yake, wale walio wagonjwa, kimaadili hutakiwa kutokuitimiza hija yao.

Magonjwa yaambukizwayo yana historia ndefu na Hija. Zipo kumbukumbu nyingi za milipuko ya magonjwa kama kipindupindu na maafa ya maelfu huko Maka, Madina na Jedah kwa miaka mingi sasa. Ni kuelekea karne ya 19 ndipo ambapo sheria za kutenga wagonjwa zilianza kutumika ili kukomesha ueneaji wa magonjwa katika eneo hilo takatifu, hadi manyumbani mwa mahujaji. Sheria hizo pamoja na kutiliwa mkazo kwa mchujo wa kiafya kwa mahujaji unaelezwa kuweza kusaidia kuwalinda mahujaji. Muda utahitajika kuona ikiwa hili linawezekana. Mafua ya nguruwe, kama ilivyokuwa kwa mafua ya ndege hapo awali, yanaweza kuja kuwa jambo lisilo na uzito unaoonekana hivi sasa. Isipokuwa hivyo, hata hivyo, ni vyema watu wakaanza kulitafakari kuanzia sasa.

Blogu ya Middle East Institute's Editor's Blog inaongeza:

Jambo hili linazidi kuwa jipya kila uchao. Mufti mkuu wa Misri anapendeza wanazuoni wa Kiislamu kutangaza fatwa [tamko la kidini] kuahirisha Hija kwa sababu ya mafua ya nguruwe. Fatwa yenyewe inapatikana hapa kwa Kiarabu. Tilia maanani –ninajua na naendelea kurudia hili –hapajawahi kuwapo suala kama hili katika Misri. Kusema kweli, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maambukizo yaliyothibitishwa katika Mashariki ya Kati yote ni Israel (wagonjwa saba). Na Shirika hilo la Afya Duniani (WHO) linasema “ Shirika halijashauri kusitishwa kwa safari kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya mafua ya nguruwe.” Ndio, na suala jingine: Hija haijafika, ni mpaka mwezi wa Novemba. Hivi kuna kitu nitakuwa nakosea hapa? Je, katika historia ya Uislamu, hivi imewahi kutokea Hija ikaahirishwa kwa sababu tu za kiafya? Sijui, lakini ninatarajia kuwa tungehitaji walau mgonjwa mmoja ili kuhalalisha uamuzi huu. (Si tu kwamba hakuna taarifa za ugonjwa Mashariki ya Kati, isipokuwa Israel, lakini pia hakuna mgonjwa yoyote Indonesia, Malayasia, Pakistani – ndio hata kokote waliko Waislamu)

2 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.