Wanawake na Uchaguzi Nchini India

Makala hii ni moja ya Makala Maalum za Global Voices Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa India wa 2009.

Demokrasi kubwa zaidi duniani, India, itafanya uchaguzi mkuu utakaoanza katika wiki chache zijazo kutoka sasa. Katika nchi yenye watu zaidi ya bilioni, uchaguzi mkuu ni wakati wa “kujenga au kuvunja” kwa makundi yenye maslahi, kwa vyama vya siasa na kwa watu wa kawaida. Kutokana na ukweli kwamba maisha yao kwa miaka mitano ijayo yataamuliwa siku ya uchaguzi.

Upinde wa rangi za akina mama wa vijijini waliokusanyika kama wahamasishaji wa kujitolea kwenye vijiji vyao.

Upinde wa rangi za akina mama wa vijijini waliokusanyika kama wahamasishaji wa kujitolea kwenye vijiji vyao.

Picha na Mtumiaji wa Flickr Mckaysavage na imetumika chini ya hatimiliki huru za jamii.

Wanawake wa India, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinyimwa nafasi yao ya haki majumbani, kazini na katika hatamu za uongozi wana dau kubwa katika uchaguzi ujao. Wanawake wanaojua kusoma na kuandika nchini (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2001) ni asilimia 53 tu ikilinganishwa na asilimia 75 kwa wanaume, hata hivyo wanawake wa India hawajatengwa kabisa kutoka katika mchakato wa kisiasa. Kiwango cha ushiriki wao kinaongezeka na vyama vingine mashuhuri vina viongozi wanawake.

Japokuwa wanawake wengi wanaanza kuwa na ufahamu wa haki zao za kupiga kura na wanashiriki katika siasa kwenye ngazi za chini, ripoti hii inaeleza kwamba inavyoelekea mwaka huu ni wanawake wachache zaidi watakaochaguliwa katika bunge la nchi.

“Kuwasilishwa kwa Muswada wa Viti Maalum vya Wanawake katika kikao cha 14 cha Baraza la Wawakilishi (Lok Sabha) kumewafanya wanawake waanze kuwania tiketi kwenye vyama vikubwa, lakini uteuzi wa wagombea kwenye vyama hivyo unaonyesha kwamba siasa za uchaguzi nchini India bado ni hifadhi ya wanaume.

Pamoja na mkuu wa chama Sonia Gandhi, ni wanawake tisa tu katika orodha ya wagombea 90-na-ushee wa Baraza la Wawakilishi waliotangazwa na chama cha Congress mpaka hivi sasa na katika orodha ya wagombea 232 wa chama cha BJP kuna wanawake 21 tu.

Chama cha Mrengo wa Kushoto, ambacho kimevishutumu vyama vya BJP na Congress kwa kutokuwa na nia ya kisiasa kuhusiana na sheria ya viti maalum vya wanawake, imewateua wagombea wawili tu wanawake kati ya wagombea 42 kwenye ngome yao ya jimbo la Bengali ya Mashariki, idadi hii ni ya chini zaidi ya wale watano ambao kiliwasimasha katika uchaguzi wa mwaka 2004.”

Samiya Anwar, mpiga kura wa kike, anaandika kuhusu uchaguzi ujao, na anauangalia kwa makini mji anaotoka wa Hyderabad:

“Kuna masuala mengi yanayowahusu wanawake zaidi ya yale yanayowahusu wanaume ambayo yanapaswa kuangaliwa. Au siyo? Kwanza, ni usalama wa wanawake katika jamii wanamoishi. Wanawake wengi katika mji mkongwe (wa Hyderabad) hawawaamini polisi. Wanapitia mateso ya ndani ya nyumba pamoja na kupigwa bila ya kulalamika. Tunahitaji mfumo ambao utawafanya wanawake waweze kuongea na mapolisi bila ya woga. Masuala kama vile ukosefu wa maji, kukatika kwa umeme kila mara, ajali za barabarani na unyanyasaji dhidi ya wanawake makazini ni lazima yapewe kipaumbele.”

Utamaduni wa matabaka ni suala kubwa wakati wa uchaguzi nchini India. Kama alivyowahi kusema mtu mmoja “Wahindi hawapigi kura bali wanapigia kura matabaka”, siasa za kuwatenganisha watu kwa kadri ya matabaka yao na kuwatumia kama “benki za kura” ni utaratibu wa kawaida.

Joshua Meah akiblogu kuhusu utamaduni huo wa matabaka na wanawake katika siasa kwenye blogu ya Washington Note anasema:

“Nchini India ambako kinyume cha kila kitu huwa ndio ukweli. Hii ni nchi ambayo imetengeneza wanawake kadhaa wanasiasa wenye nguvu kubwa, kitambo kirefu kabla hata Marekani haijaanza kulitaja somo hilo – Indira Gandhi ni mfano mmojawapo. Hata hivi sasa, Mkuu wa Uttar Pradesh, Jimbo lenye watu wengi zaidi nchini India na makazi ya watu milioni 130 linaongozwa na mwanamke anayetokea kwenye tabaka la Dalit (tabaka la chini kabisa). Maendeleo ya demokrasi nchini India katika maana ya kuelekea usawa wa jamii kwa namna fulani yamekuwa ni ya kuvutisha pumzi na kadhalika kukatisha tamaa.”

Vinod Sharma pia analijadili suala la “benki ya kura” kwa kutumia majadiliano ya kubuni kati ya wanawake watatu wenye nguvu – Mayawati (Waziri Mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh) ambaye ni wa tabaka la “Dalit” (tabaka la chini), Maneka Gandhi (mkwe wa Indira Gandhi) ambaye ni mwanaharakati za haki jamii, haki za binaadamu na za wanyama na Sonia Gandhi (wifi aliyetengwa wa Maneka) ambaye pia ni mkuu wa chama cha Congress. Ifuatayo ni nukuu:

“Sonia: Chama cha Congress ni chama cha kitaifa chenye historia tukufu.

Mayawati: Na kisicho na mustakabali.

Sonia: Usiseme hivyo. Tafadhali. Inaumiza. Tunao uwezo wa kuchukua madaraka tena peke yetu (bila kuingia kwenye mseto na vyama vingine).

Mayawati: Kweli? Angalia, Sijali ikiwa kuna mtu katokea kwenye familia ya Gandhi au raja au maharaja. Kama wewe au mwanao akitishia benki yangu ya kura kwa njia yoyote ile, nitawatupa nyote jela.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.