Rwanda: Miaka kumi na tano baada ya mauaji ya Kimbari

Hivi karibuni zilifanyika sherehe za kitaifa nchini Rwanda kuadhimisha kumbukumbu ya kutimiza miaka 15 tangu mauaji ya Kimbari. Mauaji hayo yaliangamiza maisha ya watu wapatao 800,000. Mnamo tarehe 7 Aprili, maadhimisho yalifanyika katika mji mkuu wa Kigali, na pia katika mji wa Nyanza, ambapo watu wapatao 5000 waliuawa kinyama. Katika Uwanja wa Mpira wa Kigali, maelfu ya mishumaa iliwashwa na kupangiliwa katika namna ambayo iliunda neno “Matumaini” katika lugha tatu.

Mwanablogu Mrwanda, Negrita's Chronicles, alitoa mwito kwa wasomaji wake kushiriki katika mkesha wa kitaifa wa kuwasha mishumaa ili kuwakumbuka wahanga wa mauaji. Alifanya hivyo kupitia blogu yake:

Ni miaka 15 sasa tangu Mauaji ya Kimbari yalipopabadilish nyumbani kwangu na watu wangu milele.

Ulimwengu ulikaa kimya wakati ambapo vilio vilipaazwa pasipo kuitikiwa.

Tafadhali unganeni nasi katika tukio la kuwasha mishumaa kwa kumbukumbu ya wale walioporwa maisha yao na kwa matumaini ya mustakabali uliojaa amani, haki na maelewano ya kweli.

Katika makala mfululizo, Negrita, alituma mtandaoni picha ya video ya kampeni ya Mishumaa kwa Rwanda, ambayo iliambatana na wimbo ‘Hali hii isijirudie tena kamwe’ uliotungwa na kuimbwa kwa ajili ya kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari. Wimbo huo ulitungwa na mwimbaji wa nyimbo za Injili wa Rwanda, Jean Paul Samputu. Ulitungwa kwa lugha ya Kinyarwanda, lakini viitikio vilikuwa katika lugha tofauti (Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kirundi na Kiganda) na uliimbwa na wanamuziki wengi maarufu kutoka eneo la Afrika ya Mashariki.

Picha za watoto wahanga wa mauaji ya Kimbari katika Kituo cha Kumbukumbu cha Kigali (Picha na Elia Varela Serra).

Picha za watoto wahanga wa mauaji ya Kimbari katika Kituo cha Kumbukumbu cha Kigali (Picha na Elia Varela Serra).

Martin Leach, ambaye ni mkuu wa Idara ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) nchini Rwanda alishiriki katika kumbukumbu zilizofanyika Nyanza, na anaelezea kwenye blogu yake:

Mamia ya watu walitembea polepole kwa huzuni kubwa kupitia njia ndefu iliyoelekea kwenye kilima kwenda Nyanza, wengi wao walivaa chochote chenye rangi ya zambarau, kitambaa cha begani, kanga, au utepe wa mkononi. Rangi ya zambarau ni alama ya maombolezo nchini Rwanda na jana tarehe 7 Aprili, ilikuwa siku ya kuadhimisha Kumbukumbu ya miaka 15 tangu Mauaji ya Kimbari. Pale juu ya kilima niliungana na umati mkubwa katika Maadhimisho ya Kumbukumbu. Nikiwa nimebanwa katikati ya mabalozi wawili, nilisikiliza maelezo binafsi ya watu walionusurika katika mauaji yaliyotendeka mahali hapo tulipoketi, na hakukuwa na hata mtu mmoja wa kuwatetea dhidi ya mashambulizi ya kinyama ya wanamgambo.

Lakini ilikuwa ni vijana ndiyo walionigusa zaidi: wasichana waliovalia mavazi ya rangi ya zambarau na nyeupe walighani mashairi kwa lugha ya Kinyarwanda, hasa wakihimiza umuhimu wa kuvaa ushujaa kwa ajili ya siku za baadaye licha ya huzuni kubw, na pia kwaya ya vijana waliovalia Tii-sheti zenye maneno ‘Hali hii isijirudie tena kamwe’, maneno hayo pia yalikuwa kwenye vitambaa walivyojifunga kichwani, huku wakiimba kwa hisia kubwa juu ya umuhimu wa kutosahau kamwe mauaji ya kimbari. Na kwa kweli lilikuwa tukio la kuamsha hisia kali kwani hata mawaziri wa serikali waliokuwepo walitiririkwa na machozi, wakikumbuka yaliyotokea kipindi hicho na hasa kwa kuwapoteza watu waliowapenda. Nashindwa kuiaminisha akili yangu – yaani watu milioni moja kuuwawa katika muda wa siku 100: kama alivyosema mwanamama Meya wa Kigali, akiongeza ‘mwovu asiyesemekana’ aliinyakuwa nchi.

Michael Abramowitz anayetoka katika Makumbusho ya Kumbukumbu ya Mauaji ya huko Marekani naye alikuwepo Kigali kwa ajili ya tukio hili. Katika blogu inayoitwa World is Witness, Abramovitz anasimulia ushuhuda wa aliyenusurika kwenye mauaji ya kimbari aliyeitwa Venuste, ambapo ushuhuda wake uliigusa mno hadhira iliyokuwepo wakati wa maadhimisho hayo:

Venuste, aliyeonekana kuwa na umri wa kati ya miaka 50 hadi 60, huku akitembea kwa mwendo wa madaha, aliusimulia umati uliojazana jinsi gani familia yake na majirani zao walivyoamua kukimbilia katika kituo kilichokuwa karibu cha L’Ecole Technique Officielle, wakitumaini kwamba hapo pangekuwa na usalama kwao kwa kuwa kulikuwa na kikosi kidogo cha Wabelgiji chini ya Umaja wa Mataifa. Lakini siku nne baadaye, kwa mshangao mkubwa wa kutisha, kikosi hicho kidogo cha Umoja wa Mataifa, kiliondolewa, huku wakiawaambia watu waliokimbilia pale kwamba “maaskari polisi” (gendarmes) wangekuja kuwaokoa. Askari wa Umoja wa Mataifa walipuuzia kubembeleza kwao ili wasiondoke na kuwaacha mikononi mwa makundi ya askari wa serikali na wanamgambo wenye silaha waliokuwa wamewazingira nje ya milango ya shule walipokimbilia.
Mara tu baada ya askari wa Umoja wa Mataifa kuondoka, Venuste na watu wengine wapatao 5000 waliokuwa kwenye viwanja vya shule hiyo walilazimishwa kutembea chini ya ulinzi wa wanamgambo wa Kihutu waliokuwa wakiwadhihaki, pia walikuwepo askari na raia waliobeba mapanga, bunduki na silaha nyingine. Baadhi ya wale waliookoka kufa walieleza matembezi hayo kama “Matembezi ya kifo”. Venuste alipoteza mkono wake wa kulia ambao ulikatwa na mmoja wa watesaji. Mateka hao walitembea mpaka kwenye kilele cha kilima hiki ambapo walizingirwa na genge la wauaji na kisha kushambuliwa kwa mabomu, mapanga na marungu. Katika muda mfupi tu, anasimulia Venuste, “Tulikuwa tumelala kwenye madimbwi ya damu”.
Kati ya watu wapatao 5000 walioomba ulinzi kutoka kikosi cha Umoja wa Mataifa, ni takribani 100 tu ndiyo walionusurika kufa, ndivyo alivyosimulia Venuste. Yeye anasema alipona kwa sababu alijilaza kimya chini ya maiti kadhaa, wakati huo huo wauaji waliendelea kuzagaa pale ili kuona kama kuna aliyekuwa hai bado.

Akiguswa na maendeleo ya uchumi yaliyofanywa na nchi ya Rwanda, Abramowitz haoni kama kuna dalili yoyote inayoonyesha kuwa kuliwahi kutokea mauaji ya kimbari miaka 15 iliyopita:

Kama mtu ambaye ndiyo mara yake ya kwanza kwenda Rwanda, ni vigumu mtu kutoshangazwa na kutoshabihiana kati ya matukio ya kutisha sana yaliyotokea miaka 15 iliyopita na hali inayoonekana kuwa ya utulivu mkubwa na ustawi wa aina yake inayotawala sasa nchini humo, ambapo nchi hiyo inaonekana kuwa kiini cha uchumi unashamiri kwa kasi wa Afrika ya Mashariki. Tulipokuwa tukisafiri kwa gari kutoka katikati ya mji kwenda katika moja ya makanisa ambapo mtu unaweza kuona mafuvu na mali za Watutsi waliouwawa, tuliwapita wafanyakazi fulani waliokuwa wakichimba mitaro kandokando ya barabara maalumu kwa ajili ya kutandaza nyaya za mawasiliano ya Intaneti. Kwa mtu mgeni ni rahisi kujiuliza: Inawezekanaje kwamba nchi hii ya kupendeza, ambayo mara nyingi watu wengi barani Afrika huichukulia kama ya kupigiwa mfano kwa namna yake bora ya uendeshaji, inakuwaje kwamba iliingia katika unyama huo mkubwa usiosimulika?

Wavuvi wa Uganda wakiopoa miili kutoka Ziwa Victoria baada ya kusafirishwa mamia ya maili kutoka Rwanda (Picha na Dave Blumenkrantz, una ruhusa ya kutumia chini ya utaratibu wa leseni za Ubunifu wa Pamoja)

Wavuvi wa Uganda wakiopoa miili kutoka Ziwa Victoria baada ya kusafirishwa mamia ya maili kutoka Rwanda (Picha na Dave Blumenkrantz, una ruhusa ya kutumia chini ya utaratibu wa leseni za Ubunifu wa Pamoja)

Colette Braeckman [Fr], ambaye ni mwandishi wa habari wa Ubelgiji na mwandishi wa vitabu kadhaa kuhusu Afrika ya Kati, naye pia alikuwepo kwenye maadhimisho hayo kule Kigali, naye anaandika:

Kutoka katika umati uliokusanyika mbele ya “Bustani ya Kumbukumbu” na ilipo kumbukumbu ya mauaji ya kimbari, vilio vinasikika huku na kule, hivyo kukatisha hotuba rasmi zilizokuwa zikitolewa. Wakati wote, watu waliozimia au kupoteza fahamu walinyanyuliwa na kukimbizwa hospitali kwa kutumia magari ya wagonjwa. Wakati Venuste Kasirika aliposimama jukwaani na kusimulia yale yaliyomipata, simulizi lake lilisindikizwa na vilio vya chini kwa chini kutoka kwenye hadhira iliyokuwepo.

Akipita huku na huko katika Kigali ya leo, Braeckman anasimulia mambo yanayofanana na yale aliyosimulia Abromowitz kuhusu kutofautiana kukubwa na zamani ya kutisha:

Katika jiji hili la kisasa, lenye kuleta matumaini, ambapo makazi ya walalahoi yamevunjiliwa mbali na wakazi wake kuhamishiwa mbali zaidi; katikati ya majengo marefu yenye mabenki, maduka na ofisi, unapotazama bustani nzuri za maua zinazotunzwa vizuri na maeneo ya kijani kama zile Bustani za Uingereza, tunawezaje kuamini kwamba miaka kumi na tano tu iliyopita, magari ya taka yalikuwa yakikusanya maiti makundi kwa makundi mitaani na kuzimwaga mbele ya hospitali kama takataka? Mtu unapoona watu hawa waliovalia vizuri, wakiwa wamevaa viatu safi (maana kutembea pekupeku ni marufuku hapa), tunawezaje kuvuta kumbukumbu za wauaji katili kama vichaa, tena waliolewa, waliojaa hasira na chuki, wamejizungushia hirizi, wakipepesapepesa bunduki huku na huko pamoja na mapanga na walikuwa wakiwinda, yaani kama unavyowinda wanyama, wenzao wa kabila la Kitutsi ambao kwa woga walikimbilia kujificha darini, kwenye mitaro na kwenye vichaka?

Yves Zihindula, mwanablogu wa Kikongo anayeishi Goma, anakumbuka mauaji ya kimbari kama hali ilivyokuwa upande wa pili wa mpaka:

Miaka 15 kamili iliyopita mamia ya maelfu ya wakimbizi walimiminika kuja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tarehe hii inaleta kumbukumbu za kutisha za akina mama na watoto waliochoka kwa njaa waliomiminikia kwenye mitaa ya Goma. Nakumbuka kuona maiti za watu kwenye Ziwa Kivu, upande wa Rwanda wa ziwa na ambazo zilisogezwa polepole kuja upande wa Kongo na mawimbi. Wakati huo niliona magari ya kubebea taka yakiwa yamesheheni maiti za watu na kwenda kuzitupa kwenye makaburi ya halaiki.

Ama kwa hakika hizi si kumbukumbu nzuri hata kidogo. Bado inashangaza kuona msiba huo. Binadamu wakiuwana wao kwa wao. Hata miongoni mwa wanyama jambo hili ni nadra sana kutokea. Ninatumaini tu kwamba jambo hili halitatokea tena na kwamba Afrika (na dunia nzima) nzima imejifunza somo.

Ili kusoma taarifa ya kina zaidi kuhusu historia ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda, tazama

makala hizi: Stop Genocide blog: False History, Real Genocide: The Use and Abuse of Identity in Rwanda na Genocide in Rwanda: “A Distinctly Modern Tragedy”.

3 maoni

 • Dusabemungu ANGE DE LA VICTOIRE

  Nashukuru sana kwa ushahidi huu,nami inanibidi nitumiye muda huu kwa kutoa masikitiko yangu makubwa yanayosababishwa na namna hali ya uchumi unavyoendelea kupaa baada ya mauaji ya kinyama ya mwaka1994 nchini RWANDA.Ukuaji huwo unasababishwa na uongozi bora ambao huwenda ukaboresha kilimo na ufugaji na matanda akawa ni afya nzu ri kwa jamii ya wanyarwanda.Pia na watakia waafurika wote kuiga mfano Rwanda wakati wa kufumua uchumi wa nchi zao.Ni kweli kwamba mtu anaweza kupata ahueni,baada ya kupita katika hali mbaya.Mauaji kama yale hatuyataki tena kutokea duniani.Nawashukuru,ahsanteni

 • Ndugu Dusabemungu

  Umesema kweli. Afrika ina mambo mengi sana ya kujifunza kutoka Rwanda … hasa kwa upande wa uongozi bora wenye visheni ambao ni muhimu katika kuipeleka jamii ya taifa lolote kuondokana na matatizo ya umaskini n.k. Kweli wananchi wa Rwanda na viongozi wake wanastahili pongezi. Tunajifunza kutoka kwetu. Tafadhali endelea kutushirikisha yale yanayotokea nchini humo. Asante.

 • DUSABEMUNGU Ange de la Victoire

  Zikiwa zinasalia siku 30,ili uchaguzi rasmi wa raisi ufanyike nchini humo,waliowokoka mauaji ya harayiki wanaomba serikali kuwalindia usalama pamoja na wanyarwanda wote.Ombi hilo linatokana na magruneti yaliyolipuka mjini KIGALI,na huenda ikawa inshara ya kuzuka vurugu nchini katika siku za uchaguzi utakaofanyika tarehe 9 Agasti 2010.Nilipozungumza na wakazi wa kijiji cha KINYINYA wirayani GASABO waliniambia kwamba wao tayari wameanzisha kikosi cha kulinda usalama kijijini humo katika masaa ya jioni,pia serikali inatangaza kuwa inafanya liwezekanalo ili uchaguzi huwo ufanyike katika usalama wa kutosha.Ikumbukwe kwamba raisi PAUL KAGAME wa chama tawala wa chama cha RPF atagombeaa tena uraisi.Genocide hayitatokea kamwe nchini Rwanda!

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

 • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.