Nguvu ya Watu Maarufu Katika uchaguzi wa India

Salman Khan (katikati), muigizaji filamu maarufu wa Bollywood, akipiga kampeni ya kumuunga mkono mgombea wa Chama cha Congress Milind Deora katika mkutano wa hadhara mjini Mumbai

Salman Khan (katikati), muigizaji filamu maarufu wa Bollywood, akipiga kampeni ya kumuunga mkono mgombea wa Chama cha Congress Milind Deora katika mkutano wa hadhara mjini Mumbai

Picha na Al Jazeera English na imetumika chini ya Hati Miliki Huria.

Waigizaji na watengenezaji filamu maarufu nchini India wana ushawishi mkubwa, na ukweli huo ulidhihirishwa na Danny Boyle katika filamu ya Slumdog Millionaire (dokezo: kwenye igizo la chooni). Kujihusisha kwa nyanja ya burudani (hasa Bollywood au Nyanja ya filamu za Kihindi yenye makao mjini Mumbai) katika siasa nchini India kulikuwa ni kwa kiwango kidogo (siku za nyuma) wakati waigizaji wachache na watengenezaji filamu walipokuwa wakijishirikisha kwenye kampeni za uchaguzi. Isipokuwa kwenye jimbo la kusini la Tamil Nadu ambalo ni jimbo la kwanza duniani kutumia nyenzo ya filamu kwa sababu za kisiasa kuanzia wakati wa miaka ya 1940. Mwishoni mwa miaka ya 1960 makutano haya kati ya wanasiasa na nyanja ya filamu za Kitamil Nadu kuliivunia riba nzuri Dravida Munnetra Khazagam (DMK) na kulipelekea kuundwa kwa serikali ya kwanza isiyokuwa ya chama cha Congress jimboni humo. Tangu wakati huo vyama kadhaa vilivyotokana na chama cha DMK vimekuwa vikichukua madaraka jimboni Tamil Nadu. Wakati wa miaka ya 1980 kulikuwa na mtiririko imara wa watoa burudani walioingia kwenye jukwaa la siasa. Wakati mwingine walifanikiwa kugombea na kuunda serikali (kama vile NTR na chama chake cha Telugu Desam kwenye jimbo la Andhra Pradesh) au walichaguliwa kuingia kwenye bunge la India.

Ilipofikia mwaka 2009 ushiriki wa watoa burudani wa Bollywood (au filamu za Kihindi) wenye makao mjini Mumbai pamoja na wale wa Kitamil na Kitelugu waliongezeka zaidi kwenye kampeni za uchaguzi. Muigizaji filamu wa Kitelugu Chirajeevi alizindua chama kipya cha siasa jimboni Andhra Pradesh, wakati mcheza filamu wa Bollywood Sanjay Dutt alishindwa kuteuliwa kwa sababu ya rekodi yake ya makosa ya jinai wakati wa milipuko ya mabomu ya mwaka 1993 mjini Mumbai. Jimboni Tamil Nadu aliyekuwa mcheza filamu na waziri mkuu, Jayalalitha, bado yumo mbioni baada ya kushindwa katika uchaguzi uliopita. Lakini, ni ushiriki wa watu wa Bollywood ambao umeziteka fikra za watu.

Muigizaji filamu wa Bollywood ambaye pia ni mwanablogu Amitabh Bachchan anatoa mwanga wa mawazo yake kuhusu uchaguzi ujao wa India. Anaandika:

“Uchaguzi umewadia. Uchaguzi katika demokrasi kubwa zaidi duniani. Televisheni hazina kingine cha kutangaza bali hii picha ya uchaguzi inayojifungua mbele yetu. Kura za maoni na uchambuzi, kadhalika ni nani atakayeshinda kutokea wapi na ni nani aliyesema hivi kwa nani na kwa sababu gani. Hata maswali ya vyombo vya habari yanayoletwa kwetu yamejaa udadisi unaohusu siasa. Marafiki wamekuwa maadui, maadui wamekuwa marafiki. vyama vyote vinacheza michezo na kutumiana ili kuingia madarakani. Ili kushinda katika miaka 5 ijayo na kubaki serikalini. Kwao siasa ni sawa na dawa ya kuongeza nguvu za kufanya mapenzi, dawa ambayo inawasukuma kuongeza juhudi.”

Mke wa Bachchan, Jaya Bachchan ni mshiriki hai kwenye siasa kwa miaka michache sasa.

Ni nini kinachowasukuma waigizaji wengi wa Bollywood kutoka kwenye Nyanja walizozoea na kutoa michango yao kwenye kampeni za uchaguzi huu wa India? Gaurav Shukla wa Uchaguzi wa India 2009 pengine amevumbua jibu la swali hilo. Anaandika:

“Watu maarufu ambao walizoea kuiweka siasa mbali wameamua kushabikia umuhimu wa kupiga kura. Wataalamu wa mambo wanadhani kwamba mashambulkio ya kigaidi mijini Mumbai ya mwezi Novemba mwaka jana yanaweza yakawa ndio sababu ya mabadiliko haya… Amitabh Bachchan, Aamir Khan, John Abraham, Kamal Haasan, Rakeysh Omprakash Mehra, Anurag Kashyap, Shriya Sharan, Shruti Haasan pamoja na Sushmita Senni ni kati ya wale waliojiunga na pambio.”

Muigizaji filamu wa Bollywood Aamir Khan amesaidia uzinduzi wa kampeni ya kuelimisha wapiga kura kwa ajili ya Asasi ya Mageuzi ya Kidemokrasia kwa kutumia kauli mbiu: “Sachche ko chune, Achche ko chune” — inayomaanisha “Pigia kura watu wakweli, pigia kura watu wazuri.” Pamoja na kuwa sura na sauti ya kampeni ya kuelimisha wapiga kura, Khan alichukua hatua nyingine zaidi aliposaidia kutengeneza filamu za video pamoja na matangazo ya redio.

AamirKhanblog anaandika:

“Matangazo yametengenezwa na kampuni ya muigizaji, Aamir Khan Productions, bila malipo. Orodha ‘A’ ya kundi la Bollywood limetayarisha kampeni hii. Mkuu wa ubunifu ni Prasoon Joshi wa McCann Erickson, Mkurugenzi ni Rakyesh Mehra, mpiga picha ni Avinash Gowarikar na mkuu wa mipango ya habari katika kampeni hii ni Shashi Sinha wa Lodestar Media. Kila mtu anafanya kazi bila malipo kwa ajili ya kampeni.

Kampeni hiyo inarushwa hewani katika lugha za Kihindi, Kimarathi, Gujarati, Kitamil, Kitelugu, Kikannada, Malayalam, Kibengali, Kiassam pamoja na Kioriya ili kwamba iufikie umma.”

Aamir Khan, ambaye pia ni mwanablogu anawakumbusha wapiga kura wa India kuwa wapige kura baada ya kufanya uchambuzi. Aliandika katika makala yake ya blogu:

Kwa Wahindi wote, kumbukeni kupiga kura, na mfanye uamuzi baada ya uchambuzi. Inamaanisha, chunguza wagombea wote kutoka katika eneo lako kabla ya kuamua ni nani wa kumpigia kura.

Khan yuko likizoni mjini Montana, lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari atarejea Mumbai na kupiga kura tarehe 30 Aprili, siku ambayo jiji kuu la biashara na burudani nchini India litapiga kura.

Zaidi ya khan, kundi lote la wacheza filamu na watengeneza filamu wa Bollywood wamejitolea muda wao kwenye programu mbalimbali za kuhamasisha na kuelimisha umma. Pengine, ushiriki muhimu zaidi wa nyanja hii ya burudani ni ule wa kwenye asasi-isiyo-ya-kibiashara inayoitwa Jaagore ( yaani “Amka”). Asasi hiyo imetengeneza filamu za video fupi-fupi zenye nguvu kama ile ambayo mcheza filamu wa kike wa Bollywood Sonam Kapoor anpodokeza kwamba wastani wa mpiga kura nchini india ni miaka 23, wakati ambapo wastani wa umri wa mawaziri katika Bunge la nchi ni miaka 62.

Au, angalia video hii iliyotengenezwa na mkurugenzi wa filamu mmoja wa Bollywood, Rakeysh Omprakash, ambamo anadokeza kuwa katika jimbo la Rajasthan kuna mwanasiasa aliyewahi kushinda uchaguzi kwa kura moja.

Makala hii ni sehemu ya makala zinazohusu uchaguzi wa India 2009.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.