Jamhuri Ya Kidemokrasi ya Kongo: Mahojiano na Kabila Yaamsha Gadhabu

Ulimwengu wa wanablogu wa Kikongo ulijaa shutuma kali dhidi ya mahojiano ya hivi karibuni ya rais wa Kongo, Joseph Kabila kwenye gazeti la New York Times. Katika mahojiano hayo, Kabila anaongelea kuhusu Rwanda, AFRICOM, uwekezaji wa China, na upenzi wake wa pikipiki.

Pia aliongelea ugumu wa kupata misaada mizuri; na wanablogu wengi wamemchabanga kwa hilo. Kabila anailaumu rushwa na kuutupa mpira kwenye utawala wa Mobutu na udhaifu wa maofisa wake yeye mwenyewe, badala ya kukubali wajibu wa matatizo ya serikali yake.

Swali: Je una watu wazuri wa kukusaidia?

Jibu: (baada ya kimya kirefu) Mobutu aliiongoza nchi hii kwa zaidi ya miaka 37. Aliunda tabaka la wanasiasa pamoja na fikra na hatujaweza kuzing'oa. Taratibu za zamani ni mbaya – rushwa, utawala wa hovyo hovyo, utawala mbovu na mambo kama hayo. Kosa letu kubwa ni kuwa hatujapata muda wa kutosha kufundisha na kutengeneza makada wetu wenyewe. Hauhitaji watu elfu moja kuibadilisha nchi. Hapana, unahitaji watu 3, 4, 10, 15 ambao wana imani, wana nia, na wenye azma. Je ninao hao watu 15? Pengine 5, 6, 7, lakini bado hatuna 15.

Kwenye mtandao wa Forum Realisance [Fr] Musengeshi Katata anaandika kuwa Joseph Kabila amejeruhi kila Mkongo aliyesoma mahojiano yale:

Maprofesa wote wa vyuo vikuu, maofisa wa jeshi, waalimu, mafundi, wakandarasi, madaktari, maofisa wa benki, wafanyakazi wenye ujuzi, wazazi wanaosomesha watoto wao, mawaziri, wanasheria, manaibu… n.k. ambao wanafanya kazi kila siku ili kujenga taifa la kesho; watu wote hao wameshushwa kufikia kundi la ndani la watu 15? Anageuza kibao, je huyu kweli ni mkuu wa nchi anayeongea au ni sawa tu na kocha mbovu wa timu ya mpira wa miguu au mpira wa mabavu?

Inadhihirika, kwamba raisi huyu, ambaye hajapata matokeo yoyote mazuri, anataka kuwafanya wananchi wake – na hili linawafurahisha watu wengi wa Magharibi wakati huu usiotabirika wa misukosuko – kuwa ni wajinga na wasiojua kazi.

Swali ni kuwa: Anafanya nini madarakani, mchawi huyu, kama hawezi kumuamini mtu yeyote na kama inavyodhihirika kwamba hajui jinsi ya kuchagua watu anaowahitaji ili sera zake zipate matokeo?

Joseph Kabila, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2002 (Wikipedia)

Joseph Kabila, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2002 (Wikipedia)

Congoliberte anadhani kuwa kama Kabila kweli anaamini kwamba kuna watu saba tu kwenye serikali yake ambao wana thamani, wakati wa kusafisha nyumba umefika:

Kama anaweza kuwategemea watu 6 au 7 pekee, au watu chini ya 10, ili kuendesha nchi, katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 70. Hili ni jambo makini…

… Wakongo wanahitaji maelezo juu ya baraza la mawaziri lenye washauri dazeni, serikali yenye wanachama karibu ya 60, bunge lenye wawakilishi 500 na maseneta 120..

… Wazalendo na wenye vipaji vilivyojificha, ambao wako kwa maelfu, wanachapa kazi kwenye vivuli vya wale walioliteka taifa nyara. Wanawake na wanaume wa Kongo wamsubiri [Kabila] asafishe “banda lake la nguruwe”… Kwa nini asibuni, aunde baraza la washauri wa rais pungufu ya 10 na baraza la mawaziri pungufu ya watu 15… ni sasa au kamwe haitawezekana, huu ndio wakati wa kufanya uamuzi mzuri…

Mouvement Libération du Congo – Diaspora anafikiri kuwa maelezo ya Kabila kuhusu uhaba wa viongozi wanaoweza kazi yanafanana na yale ya wakoloni:

Kwa wale miongoni mwetu wanaofahamu kuwa “uhalifu wa kimipango katika Afrika ya Kati” umefaidika kwa huduma za Wazungu, inawezekana kuwa Joseph Kabila anatuma ishara kwa “wakuu” wake ili kufafanua mbinu anazotumia.

Kusoma majibu ya Joseph Kabila aliyoyatoa kwenye New York Times kulikuwa ni sawa na kuwa kwenye adhira na Karel De Gutch, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, aliyedai kuwa hakuwaona wanasiasa wanaopaswa kupewa cheo cha uanasiasa kati ya wale wanaomzunguka Kabila. Kama unafahamu manung'uniko ambayo yalisababishwa na tamko la De Gutch na unaposikia maelezo hayo hayo yakitoka kwenye mdomo wa “rais” (yaani Kabila) ni lazima utajisemea wewe mwenyewe “taarifa hii inanifanya nijihisi vibaya”. Tunakabiliwa na kuanguka kwa sera zilizonzishwa kwenye misingi ya utengano, ghasia, rushwa, na uongo, Joseph haraka anatafuta visingizio: Fikra za Mobutu, za akina mobutu, za wanaoamini U-mobutu. Mahojiano haya yangekuwa na ushawishi kama Joseph angetaja hatua tatu au nne ambazo zilitekelezwa kwa ajili ya manufaa ya Wakongo katika miaka yake 7 ya kutawala. Hakuna hatua zozote ambazo anaweza kuzitaja.

Kuna wanablogu ambao pia walijadili matamshi ambayo Kabila aliyatoa kuhusu Rwanda, nchi ambayo ina mahusiano magumu na Kongo. Pamoja na mambo mengine, mpaka sasa Rwanda imekataa kumuwasilisha nchini Kongo Laurent Nkunda, aliyekuwa mkuu wa kundi la waasi wanaowaunga mkono Watusi ambao walikuwa wakifanya vitendo vyao mashariki mwa Kongo. Kabila alimueleza mwandishi wa New York Times:

” Je ni maslahi gani Rwanda iliyonayo nchini Kongo? Ningependa kuamini kuwa ni maslahi sawa. Lakini kama kuna ajenda ya siri, na maslahi ya Rwanda ni kutaka kudhibiti uchimbaji wa madini na mambo kama hayo kinyume cha sheria, na kama wana mkono kwenye kwenye kila jambo linaloendelea Kivu ya kaskazini na Kusini, basi bado tupo mbali sana na kuaminiana. Hebu tuwape faida ya kutofahamu, kwa mara nyingine tena, pengine kwa mara ya mwisho.”

Mwanablogu The Mushaki Pager anashindwa kuelewa ni nini kilichomfanya Kabila achukue msimamo huo mkali:

Hii si Diplomasia. Je anataka kuwakasirisha watawala wa Rwanda? Je alifanya makubaliano na Ufaransa ambayo yalimruhusu kutumia lugha ya uchokozi dhidi ya Warwanda, ambao rais wao hivi karibuni alisema kuwa wana urafiki thabiti baina yao na Kinshasa?

Afrique des Grands Lacs alipachika tafsiri ya kifaransa ya mahojiano hayo na anaandika:

Bwana Kabila alithibitisha tena kuwa Rwanda itamuwasilisha Laurent Nkunda na kuwa atafikishwa mbele ya haki nchini Kongo. Hata hivyo, swali ni kuwa ni zana ipi aliyonayo Kabila ambayo itahakikisha kufikishwa kwa Nkunda (nchini Kongo)…

Ninashangaa kwamba Kabila alitamka wazi kuwa hakuna hati ya kukamkamata Nkunda. Kauli hii inayojipinga kwenye mahojiano hayo ni ishara ya wazi kuwa Kabila hashughulikii tena suala la kumuwasilisha Nkunda nchini Kongo. Kama mkuu wa nchi mwenyewe “anasahau” amri ya kimataifa ya kumkamata Nkunda iliyotolewa na vyombo vya sheria vya nchi yake, je ni vipi unategemea amri hiyo kuwa na nguvu?

Kwenye Forum Réalisance [Fr], Katata anakosoa mahojiano yale, hasa juu ya matamko ya Kabila kutokuwa na maana. Anavilaumu vyombo vya habari vya magharibi:

Inashangaza kwamba rais aliyechaguliwa anaweza kuonyesha uwezo mdogo kwenye mahojiano na gazeti muhimu kama hili la The New York Times:

Wengi watasema: hii inatokana na maswali aliyoulizwa na nini alichokuwa akikitafuta mwandishi katika mahojiano. Nafahamu kuwa hilo linawezekana: zaidi ya yote lile lilikuwa ni tangazo kwa ajili ya rais wa Kiafrika ambaye wanataka kumtengenezea sifa, na si kutaka kupima ukomavu wa mantiki yake na uwezo wake wa kisiasa. Kwani Wamarekani wanayo dhana yao juu ya Afrika: bara la masikini, wadhaifu, na wasiojiweza ambao Wamarekani wanawahitaji ili wajisikie kuwa wao ni watu wenye nguvu kijeshi, kisiasa na kichumi. Bara kongwe la ombaomba ambalo watu hulipatia misaada iliyokithiri, ambayo inatumika kutatua, kwa njia moja au nyingine, matatizo ambayo haifahamu jinsi ya kuyatatua.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.