- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Irani: Mwaka Mpya Waanza na Ujumbe Kutoka Kwa Obama

Mada za Habari: Marekani ya Kaskazini, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Iran, Marekani, Mahusiano ya Kimataifa, Sanaa na Utamaduni, Siasa, Utawala

Mwaka huu, sherehe za mwaka mpya wa Ki-Irani zilianza na ujumbe usiotarajiwa kutoka kwa rais wa Marekani Barak Obama, uliolekezwa kwa watu wa Irani na kwa mara ya kwanza, kwa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, ujumbe huo ulitoa rai ya kuanza upya kati ya nchi hizo mbili. Wanablogu kadhaa wametoa maoni kuhusu ujumbe huo, na wengine wanaanza kuziona zama mpya baada ya zaidi ya miaka 30 ya misukosuko kati ya mataifa haya mawili.

Mohammad Ali Abtahi, makamu wa rais wa zamani, anadhani ujumbe wa Obama ni wa muhimu sana na anaandika: [1]

Kwa jina la jamhuri ya Kiislamu ya Irani, pia nawapongeza taifa la Irani na viongozi wake. Bila ya shaka hii ni fursa ya kihistoria. Hatuwezi kudharau umuhimu wa Marekani katika hali ya sasa ya Irani. Bila ya shaka hatuwezi kupuuza nyayo za Marekani katika kila majalada ya wasifu wa Irani hasa yale ya kiuchumi hata kama ni kwa uchache, kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya taifa la Irani. Kutuma ujumbe wa pongezi kunaweza kuwa ni fursa muhimu kisiasa, kiuchumi na kihistoria, leo hii na hata baada ya kubadilishwa serikali ya Marekani. Kadhalika kupuuza kunaweza kuifanya hali izidi kuwa ya hatari zaidi ya ilivyokuwa wakati wa utawala wa Bush kwa sababu Obama anaweza kukusanya viongozi wa kisiasa na maoni ya wananchi dhidi ya Irani.

Mwanablogu ambaye pia ni mwanahabari Masih Alinejad anaandika [2] [fa] kuhusu sababu zilizoifanya Idhaa ya Taifa ya Televisheni kutotangaza ujumbe wa Obama. Anaongeza:

kama Obama angeongea kama Bush na kuitathmini Irani kama tishio, Idhaa ya Televisheni ya Taifa ingetangaza mara kadhaa. Mwanablogu huyu anatukumbusha ile hotuba ya mashuhuri ya Bush ambayo aliita Irani mwanachama wa kundi la waovu ilitangazwa mara kadhaa kwenye televisheni ya taifa.

Zandgieh Sagi ameuita [3] [fa] ujumbe wa Obama kama ujumbe chanya na jambo ambalo linawastahili watu wa Irani. Mwanablogu huyu anasema kuwa jambo la kwanza ambalo serikali ya Irani inaweza kulifanya ni kutumia lugha inayofaa kisiasa.

Katika blogu ya In View from Iran tunasoma [4]:

Kuna hatua nyingi ambazo serikali ya Marekani inaweza kuzichukua ili kujenga imani. Siyo zote ambazo zitategemea nia ya serikali ya Irani ya kuanzisha mazungumzo na Marekani. Nauona ujumbe wa Obama wa mwaka mpya kama ujumbe chanya, lakini tunahitaji zaidi ya hilo.

Mmoeeni anaandika [5] [fa] kwamba wakati televisheni ya Irani haikutangaza habari zinazohusu ujumbe wa Obama, rais wa Irani aliweza kuwatukana viongozi wa Marekani huko Marekani. Mwanablogu huyo anaongeza, kwa kejeli, kwamba Ahmedinejad atasema kwamba kuna uhuru wa kweli nchini Irani.

Sherehe za Mwaka Mpya
Wairani walisherehekea Norouz (Nowruz) kunako siku ya kwanza ya msimu wa kuchipuka mimea. Katika dhifa hii, baadhi ya Wairani huweka maua kwenye kaburi la Cyrus Mkuu [6], mwanzilishi wa ufalme wa kwanza wa Persia katika Pasargad [7] (pichani juu). Kwenye tovuti ya Okoa Pasargad imeandikwa [8] [fa] kwamba utawala wa jamhuri ya Kiislamu hausaidii wageni wanaozuru sehemu hii ya kihistoria, lakini katika miaka ya hivi karibuni watu wengi wamekuwa wakizuru ili kuusherekea mwaka mpya huko Pasargad.