- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Martinique: Uhuru na “Ubeberu” wa Kifaransa

Mada za Habari: Nchi za Caribiani, Ulaya Magharibi, Guadeloupe, Martiniki, Ufaransa, Maandamano, Siasa, Utawala, Vyombo na Uandishi wa Habari

Bloga wa Kimartinique le blo de [moi] [1] [FR], katika makala yake nyingine inayohusu harakati za wafanyakazi wa Martinique na Guadeloupe [2]anapambana na Christophe Barbier, mhariri wa maoni katika gazeti la Kifaransa, L'Express. Katika mahojiano ya redio ya C dans l'air [3] hivi karibuni, Barbier alijibu ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa msikilizaji aliyeuliza, “kwa nini tusizipe Idara za Ng'ambo uhuru wao?” Barbier akajibu:

“(…) Ikiwa (visiwa hivyo) vitageuka kuwa kiwanda cha utalii cha Marekani, au vitaangukia kwenye udhibiti wa majangili (wa kimafia) ambao watapageuza kweupe, au patakuwa Haiti mpya, uhuru hauwezekani bila ya kushamiri kwa uchumi! Mara moja vitakuwa tegemezi kwa nchi nyingine na (utegemezi huo) utakuwa mbaya zaidi ya kuwa tegemezi kwa Ufaransa.”

le blog de [moi] amekasirika:

Kweli? Christopher Barbier??? “Itakuwa”?!!! Na hapa, ngoja nikwambie, bila kuficha (na wale wote ambao wamekuwa wakinisoma kwa muda wanajua msimamo wangu kuhusu suala hili): hakuna sababu nzuri ya kuunga mkono uhuru! Maneno haya, na sauti ya dharau iliyotumika, na nyodo… yote yako wazi! Kwa sababu hatimaye siku moja tukiamua kuruka kiunzi na kuwa huru, huo utakuwa ni uamuzi wetu, liwalo na liwe, sawa! Baada yetu [Wafaransa] pataharibika??? Hao watoto wakubwa [Idara za Ng'ambo] hawatajua jinsi ya kujilinda au kuepuka vipingamizi vinavyoambatana na kuwa taifa huru? Hayo ndiyo maneno ya kunadi ili kufafanua kwa nini Idara za Ng'ambo ziendelee kupakatwa na Ufaransa? Yesu wangu!

Katika maoni, Elsie anapinga kuwa maoni ya Barbier yalikuwa na dharau:

…Pengine alichotaka kusema ni kuwa nchi ndogo kama Martinique (au Guadeloupe), katika mazingira magumu ya visiwa vya Karibeani, kitakuwa na hali ngumu kujikimu na kuwazuia wauza madawa ya kulevya na magenge yao ambao wamejaa katika kanda hiyo, bila ya msaada wa taifa kubwa (Marekani badala ya Ufaransa?). Hili si suala la kujua kuwa pengine watu watakaoliongoza taifa watakuwa wana uwezo au la, ni kusema tu kuwa nchi ndogo, kutokana na nguvu ndogo za kijeshi, inaweza tu kuishi chini ya kivuli cha taifa kubwa ambalo linailinda…

Lakini Elsie hakubaliani na dhana kwamba ni Ufaransa pekee ndiyo inayoweza kutoa ulinzi huo.

wk de l'ile antoa mifano kadhaa ambayo maoni ya Barbier yanadhihirika:

Bila kuficha, sifikiri kuwa alichokisema kilikuwa na ubeberu… alizungumza ukweli katika lugha ya dharau, na bila ya shaka, kwa kukurupuka: “kiwanda cha utalii cha Wamarekani”: Iangalie St Lucia, Jamhuri ya Dominika na Haiti, Montego Bay katika Jamaika, Barbados…” chini ya udhibiti wa majangili (wa kimafia) ambao wanapageuza kweupe”: Angalia St Martin, Anguilla…” Haiti mpya”: Sina la kuongeza…

wk de l'ile anaendelea:

Lazima nikubali kuwa, kutokana na chuki fulani kwa upande wa serikali na ninaposoma maoni ya wasomaji wa magazeti ya Le Monde, Le Figaro, La Liberation… Nachefuka ninapouona ujinga mwingi kuhusu sisi ni nani… Wakaribeani wa Kifaransa… kiasi kwamba nina mgogoro wangu mdogo wa kuunga mkono uhuru…

Matumaini yangu ni kuwa kwa kufuata mifano ya mafanikio na kushindwa kwa mataifa yaliyoko kwenye kanda yetu, tukitilia maanani historia yetu ya kipekee na uhusiano wetu na Ufaransa Bara, Afrika na Asia, kwamba hatutajipiga risasi mguuni na kuwa tutaziweka taasisi pahala pake na maendeleo ambayo yatazingatia sisi ni nani. Kuufafanua utaifa wetu kwa utambuzi finyu, unaochochewa na itikadi za kitaifa, ni njia hatari kwa maoni yangu. Na tuhuishe jamhuri inayovuka mabara (tujikumbushe ile dhana nzuri ya Marlène Parize)