- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Jamaika: Miziki Yenye Maneno Machafu Yazuiwa

Mada za Habari: Nchi za Caribiani, Jamaica, Trinidad na Tobago, Lugha, Maandamano, Muziki, Sanaa na Utamaduni, Vyombo na Uandishi wa Habari, Wanawake na Jinsia

Utata wa muda mrefu juu ya usahihi wa kurushwa hewani kwa miziki fulani umezuka tena nchini Jamaika [1]. Kufuatia majadiliano yaliyotokea baada ya kutolewa kwa kibao kipya cha Vybz Kartel [2] na Spice [3] kinachoitwa Rampin Shop [4], chenye mashairi yenye lugha kali, Tume ya Utangazaji ya Jamaika [5] imetangaza kuzuia kurushwa hewani kwa nyimbo zote zenye mashairi yanayohusu ngono [6]. Kuzuiwa huko kulianza rasmi tarehe 6 Februari, 2009 na kumezuia nyimbo zote zinazosifu uchezaji wa muziki unaofanana na kitendo cha kufanya ngono kwa kasi au “daggering”, [7]kadhalika nyimbo zozote zinazotumia zana za kuhariri zinazochuja matusi na uchafu mwingine.

Bloga wa Kijamaika, Girl With a Purpose [8]anaandika [9] kwamba anafikiri amri hii ya kuzuia iliyowekwa itafanikiwa kuzuia miziki michafu itakayosikilizwa “pengine kwa asilimia 50 ya muda… kupitia redio na televisheni”, wajibu mkubwa bado ni wa watu wazima katika jamii yetu, hasa wazazi, ambao inawabidi wajichunge wao wenyewe na wajue kwamba:

Ni makosa, kuwaachia watoto wao wasikilize miziki iliyojaa ngono na uchafu, kunawakuza watoto kabla ya wakati wao na kuwafundisha vitendo vya ngono na unyama.

Mwelekeo mwingine katika majadiliano haya yanahusu mitindo mingine ya muziki ukiachilkia mbali muziki wa dancehall [10] (yaani, soca [11] na calypso [12], hip hop [13], miziki ya kufoka n.k.), hasa kutokana na kwamba Jamaika ndiyo inaingia kwenye msimu wa Kanivali [14] – kipindi ambacho miziki ya soca inachukua jukwaa la kati visiwani kote. Katikati ya vilio vya unafiki kutoka kwa wasanii wengi wa Kijamaika ambao wanahisi kwamba mtindo wa Dancehall pekee ndio unasakamwa, Bloga wa Kijamaika, MadBull [15] aliyeko huko Cayman [16], anaandika kwamba anaunga mkono amri hiyo [17] na anafikiri kuwa amri hiyo ienezwe na kuzuia mtindo wowote wa muziki unaotarajiwa kurushwa hewani. Anashangaa katika blogu yake:

Vipi kuhusu soca, hip hop na mingineyo? Sijali ni mtindo upi! Kama mashairi ni machafu, nayo pia iangushwe! Hivyo ndivyo ninavyofikiri!

Bloga wa Kijamaika mwenye siasa kali, Agostinho [18], alichapisha katika blogu yake [19]barua aliyoiwasilisha kwa wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini humo [20]ambamo alijadili haja ya muziki wa dancehall kubadili sura yake. Ilhali anaikubali nafasi ya muziki wa dancehall katika jamii ya Kijamaika na umuhimu wake katika utamaduni maarufu, anahisi kwamba muziki wa dancehall unawajibika kwa jamii iliyoikuza na unapaswa kubadili sura yake…

Siyo tu kwa maslahi ya ukweli uliopo kwamba (muziki huo) umejiongezea nguvu na umuhimu katika jamii, bali pia kama njia ya kuonyesha ubunifu wake. Kama tunavyofahamu, (ubunifu) unaweza kwenda zaidi ya mada za ngono na unyama. Visingizio vinavyohusu ukosefu wa elimu kati ya wengi wa watengenezaji pamoja na wasanii wa muziki huo ni kutusi akili na kina cha ubunifu uliopo kwenye utamaduni/muziki. Yote haya lazima yahusishwe na mahitaji yetu muhimu ya maendeleo ya taifa, kujivunia utamaduni na maendeleo ya kweli.

Mwanablogu Stunner’s Afflictions [21]pia anafafanua mawazo yake kuhusu amri hiyo [22]. Anaunga mkono hatua hiyo ya Tume ya Utangazaji, anasema kuwa amri hiyo ilikuwa inahitajika tungu kitambo:

Ni kazi yao kuangalia lipi ni jema kurushwa hewani kama inavyoelezwa katika Taratibu za Televisheni na Sauti. Hivyo kwa nini walingojea mpaka umma ulipopiga kelele na kutia shinikizo ili wachukue hatua za kuzuia mambo kama hayo? Walikuwa wakifanya nini na wanafanya nini, na pesa zangu za kodi nilizozipata kwa shida? Tume ya utangazaji inabidi inabidi iongeze bidii na tukio hili linawadhihirishia.

Makala yake iliyofuatia katika siku ya Wapendanao ya Valentino [23] ilitaka kuwakumbusha wasomaji jambo moja muhimu:

Siyo miziki yetu yote ya dancehall/Reggae isiyovutia. Bado kuna miziki mizuri sana inayorushwa hewani.

Anaendelea kwa kuonyesha mfano wa video ya muziki mmoja wa namna hiyo, “Love Reigns” [24]uliochezwa na Tarrus Riley [25]pamoja na Bugle [26], wawili kati ya wanamuziki wapya wa Jamaika.

Tangu kutolewa amri ya kuzuia miziki yenye matusi, pameanza wimbi la kuunga mkono utengenezwaji wa bidhaa chanya kutoka kwa watengeneza burudani wa Kijamaika. Yard Flex [27], jarida lililojipachika cheo cha Gazeti kuu la burudani Jamaika, liliripoti [28] kuhusu Tychicus, mtu anayejiita nabii na mponyaji ambaye alifanya maandamano ya mtu mmoja kupinga nyimbo zote zinazosifu uchezaji wa muziki unaofanana na kitendo cha kufanya ngono kwa kasi au “daggering”, [29](tychicus) amebuni mitindo safi ya kucheza ambayo anadai imetoka kwa Muumba.

Mjadala huu bado unaendelea kwani amri ya kuzuia ina siku 10 tu, na utekelezaji pamoja na madhara yake bado hayajaonekana. Wanablogu wa Jamaika wanaunga mkono amri hiyo, na wanaona kuwa huu ni wakati wa wasanii wa Jamaika kuongeza bidii na kuudhihirishia ulimwengu ubunifu wao.