Indonesia: Talaka na Ndoa za Mitala

Najihisi nina hatia ninapoandika kuhusu talaka na ndoa za mitala wakati wa siku ya wapendanao ya Valentino. Lakini mada hizi zisizotamkika ni ukweli wa mapenzi na mahusiano. Katika Indonesia, wanawake wengi wanawataliki waume zao kwa sababu ya mitala.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2006 kulikuwa na karibu ya kesi 1000 za talaka zilizotokana na mume kuoa mke mwingine. Ndoa za mitala pia zinaongezeka – Asasi ya Msaada wa Sheria ya Jumuiya ya Haki za Wanawake wa Indonesia ilipokea taarifa 87 za mitala mwaka 2008, ongezeko kutoka taarifa 16 katika mwaka 2007.

Wanawake zaidi walio katika ndoa za mitala wanaanza kusisitizia haki zao. Abdul Khalik anayeandika kwenye The Jarkata Post ananukuu mitazamo ya wanazuoni kuhusu suala hili:

Mkurugenzi Mkuu wa miongozo ya Kiislamu katika Wizara ya Mambo ya Dini, Nasaruddin Umar: “Kumekuwepo na ongezeko kubwa la talaka kwa sababu wanawake wameanza kupinga ndoa za mitala katika miaka ya karibuni.”

Mwanazuoni wa Kiislamu Siti Musdah Mulia: “Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake hivi sasa wanathubutu kupigania haki zao na kupinga utawala wa wanaume. Hivi sasa wanasema, ‘ina maana gani kuendelea na ndoa wakati ninasononeka'”

Kwa ujumla talaka zimeongezeka katika Indonesia kwenye mwongo mmoja uliopita. Habari moja mwanzoni mwa mwezi huu ilithibitisha mwelekeo huu; na kadhalika wanandoa wanatengana kutokana na tofauti za kisiasa:

Wastani wa talaka ulipanda kutoka 20,000 kwa mwaka kufikia zaidi ya 200,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka kumi.

Amini usiamini, wanandoa wengine huamua kutengana kwa sababu mume na mke wana mwelekeo tofauti kuhusu masuala ya siasa. Hili halikuwahi kutokea hapo awali,” alisema Umar. Mwaka 2005, wanandoa 105 walitaja tofauti za kisiasa kama sababu ya kuachana lakini idadi hii iliongezeka kufikia wanandoa 502 mwaka 2006. Takwimu za mwaka 2007 na 2008 hazijajumlishwa bado. Ofisa huyo alisema asilimia 90 ya ndoa kati watu wa dini tofauti huisha kwa talaka.

Indonesian Matters inanukuu ripoti ya mwaka 2007 kuhusu sababu za talaka:

Ripoti ya Tume ya Taifa ya Kulinda Watoto (Komnas PA) inasema kuwa sababu kubwa za talaka ni mashinikizo ya kiuchumi (asilimia 23), ikifuatiwa na ugomvi katika unyumba (asilimia 19), kutopatana (asilimia 19) kuingiliwa na ndugu (asilimia 14), vurugu (asilimia 12), uzinzi (asilimia 8) na matatizo ya kingono (asilimia 3.6). Takwimu hizi, hata hivyo, zimekusanywa kutoka katika kesi 109 tu

Makala moja ya mwaka 2008 inanukuu sababu za talaka kama ifuatavyo:

kutopatana ( kutokana na uzinzi) – kesi 54000
Kutoelewana – 46000
Hali ngumu ya uchumi – 24000
Kuingiliwa na ndugu – 9000
Matatizo ya kifamilia – 4700
Ndoa za kulazimishwa – 1700
Ugomvi wa ndani ya nyumba – 900
Mitala – 879
Matatizo ya kibaiolojia (kama vile ugumba) – 580
Ndoa kabla ya umri wa ndoa – 284
Kufungwa jela – 150
Tofauti za kisiasa – 157

Ni vigumu kuwa mtalikiwa katika Indonesia. Bloga My Busy Brain anafafanua:

Watu wengine katika Indonesia (sijui nchi nyingine), talaka si chaguo. Hata kama ndoa haina afya, hata kama ndoa yenyewe ni ya mateso, mtu huamua kuendelea na ndoa kwa sababu pengine hawezi kufikiria kuishi peke yake, amechoka sana na anakubali kuwa hiyo ndiyo hatima yake, au ni mtegemezi (hususan kwa wanawake).

Asubuhi hii nilipigwa na barua pepe niliyopokea kutoka kwa rafiki yangu tuliyekuwa naye shule ya sekondari, kwamba haendelei vizuri na amepoteza kilo 7 katika miezi 3 iliyopita kwa sababu yumo katika mchakato wa talaka. Mungu wangu. Siyo nyingine tena. Japokuwa mimi mwenyewe ni mtaliki, sipendi kusikia watu wanapewa talaka kwa kuwa nafahamu ni jinsi gani inavyouma

Parvita naandika zaidi kuhusu unyanyapaa unaoambatana na wanawake waliotalikiwa nchini Indonesia:

Sina tatizo kwamba nimetalikiwa, lilikuwa ni jambo sawa kufanya wakati ule na sijuti asilani. Watu wanaponiuliza mumeo yuko wapi, nawaambia kuwa tumetalikiana. Kwa kawaida ni wao ndio hujisikia vibaya.

Jambo la huzuni ninalotaka kusema hapa, ni kuwa baada ya miaka 3, mtu ambaye nilitarajia na kutumaini kuwa angenipokea kama nilivyo, hajaweza kuikubali hali na ananiangalia kama vile sijatimia. Nina hakika kuwa kuna wanawake wengi katika nchi yangu ambao wanafikwa na hali hii, hasa wale wa kizazi cha zamani au wale wahafidhina. Pamoja na ujasiri wao wa kuishi pekee, wanang'ang'ania ndoa zisizo na furaha kwa sababu wanahofia watu wengine watafikiriaje, au kwa sababu tu hawako huru, kifedha au kiakili.

Katika Indonesia wanawake wanaangaliwa mafanikio yao si kwa yale waliyoyafanya, bali kutokana na waume zao, ni watoto wangapi wanaweza kuzaa na watoto wao wana siha kiasi gani, na watoto wanasoma shule zipi.

Bloga nin's journey alitiwa moyo na makala iliyoandikwa na Umm Faroug kuhusu namna ya kuwa mwanamke wa Kiislamu mwenye siasa kali:

Nikiwa kama mwanamke wa Kiislamu mwenye siasa kali ninatambua haki zangu kama mke, ambazo ni kulishwa, kutunzwa katika makazi, kuvishwa na kuenziwa kwa hali inayonipasa. Nina haki ya kuwa na mkataba wa ndoa unaonihakikishia haki zangu kama itatokea talaka.

Katika hali ya mzaha, Indosingleparent Community anatuma picha ya keki za talaka. Mfanyabiashara ya migahawa wa Kiindonesia Puspo Wardoyo anatoa ‘maji ya matunda ya ndoa za mitala’, mchanganyiko wa matunda manne, na mboga za mitala, mseto wa mboga nne, kwenye migahawa yake.

Picha ya kielelezo kwa hisani ya ukurasa wa Flickr wa Daquella Manera

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.