Wanablogu wa Bahrain wanaujia juu uamuzi wa Waziri wa habari wa nchi hiyo wa kuzuia upatikanaji wa tovuti mbalimbali, kadhalika kuzuia matumizi ya tovuti vivuli [proxy sites] zinazoruhusu watumiaji kuperuzi tovuti nyingine zilizozuiwa na zana za kuchuja habari. Ayesha Saldanha anaangalia maoni kutoka Bahrain.
Bloga Ammaro anaandika kwa jeuri:
WAZIRI; HUU NI UJUMBE MAALUM KWAKO. UNAWEZA KUFUNGA MLANGO, UNAWEZA KUFUNGA MILANGO MIWILI, LAKINI HAUTAWEZA KUUCHUJA MTANDAO WA INTANETI, UPENDE USIPENDE. KUNA NJIA MILIONI MOJA NA MOJA ZA KUVIZUNGUKA VIZINGITI VYAKO, NA HAUTAWEZA KUKABILIANA NAVYO VYOTE.
Bloga Rayyash anasema:
Nilistuka wakati nilipoisoma amri iliyotolewa na Waziri wa Habari wa kuzuia tovuti kwenye matandao wa intaneti. Sababu iliyonifanya nishangae haikuwa ile inayohusiana na uamuzi wa kuzuia tovuti za ngono, ambao nakubaliana nao na kuwataka wazifunge, lakini ni kwa ile sehemu inayosema kuwa tovuti yoyote ile inaweza kuzuiliwa. Sababu ni kwamba siamini kuwa serikali za Kiarabu zina nia njema.
Hussein Marhoon ana mtazamo tofauti kidogo:
Kimsimamo, ninapinga kufungwa kwa tovuti zikijumuishwa zile za ngono hata kama sifahamu thamani ya “kupinga”. Ninajua kwamba kuna wimbi la kidini linaloanza kuathiri kila sehemu ya maisha yetu.
Jenan anauliza:
Kwa nini hatufaidi uhuru wa kujieleza na tuko wapi kwenye suala la kuruhusu uhuru wa kujieleza?
Mohammed Marhoon pia anauliza:
Je hatumo kwenye zama za mageuzi na uwazi? Hakuna kisingizio cha kumuweka mlinzi kwa mtumaji na mpokeaji!
Bloga The Redbelt anasema:
Ngoja nijaribu kukuchorea picha:
Ni katika miaka ya 1980. Hakuna intaneti wala setilaiti za idhaa za televisheni. Mawasiliani pekee tuliyonayo na dunia ni kwa kupitia mikanda ya video, kanda, vitabu na majarida. Katika wakati huu, kufungiwa kwa kitu kuliweza kufanya kazi. Kama serikali ikisema kutokana na sababu moja au nyingine kwamba filamu kwa mfano, haikubaliki na haitakiwi, wengi wa watu, kama sio wote, wasingeweza kuiona. Kanda zingeweza kufikiwa na kupokonywa kwa urahisi. Halafu nini? Kufungia vyombo vya habari katika zama zile kuliweza kufanya kazi. Lakini hiyo ilikuwa zamani sana, ZAMANI sana. Hebu muangalie kaka yangu, alikuwa ni ndoto tu mwaka '86 na akazaliwa mwaka '87. Hivi sasa ni mrefu wa sentimita 186, ana ndevu za beberu, ana leseni ya gari na shahada ya chuo. Vyombo vya habari vimekua vivyo hivyo.
Eyad anajiuliza kuhusu mantiki ya biashara:
Tusiangalie intaneti kama tu njia kuu ya mawasiliano bali pia kama bidhaa, watu majumbani wanalipia kiwango kizuri cha pesa kila mwezi ili kuweza kutumia intaneti, na wanaridhia kufanya hivyo, kwa kuzingatia ukweli kwamba [makampuni ya mawasiliano] yanawekeza vikubwa kwenye mitandao na teknolojia ili kuweza kufikisha huduma zao majumbani na kwenye biashara mbalimbali nchini, je itakuwaje, katika mazingira haya, kama watu wataacha kulipia huduma za intaneti au wakichukua hatua nyingine kama vile kuchangia malipo, watoa huduma za kuunganisha intaneti watawezaje kutetea uwekezaji na juhudi zao za kuboresha huduma wakati serikali haisaidii lolote.
Funaki anasema:
Tumebarikiwa na akili za kuweza kufanya maamuzi na kutofautisha kati ya mema na mabaya. Sihitaji mtu wa nje aje kuniambia ni lipi jema na lipi baya.
Yagoob anasisitiza jambo hilo hilo – na ana ombi kwa Waziri:
Watu lazima wawe huru kufanya watakalo mtandaoni, ikiwa ni jambo salama au ikiwa ni dhambi hiyo si biashara ya serikali… Sisi siyo ng'ombe ambao wanahitaji kuswagwa na kuonyeshwa njia ya ‘za haki’ au njia ‘za serikali’. […] Mheshimiwa, kuzuia tovuti hizi kutaendelea kudhalilisha uhuru waliopewa watu wa Bahrain kupitia katiba, kadhalika kuwanyima watu wa Bahrain tovuti za maana bila sababu yoyote. Tafadhali fikiri tena na uondoe vizuizi vilivyowekwa kwenye tovuti hizo na uturuhusu sisi kama wananchi kuongeza maarifa, elimu na kuhamasishwa…
Hussain Yousif anasema:
Ninapenda kuishukuru serikali kwa kutukumbusha kwamba Bahrain ni toleo jipya la nchi za dunia ya tatu ambako uhuru ni jambo linaloongelewa tu lakini halipo.
Bloga Silly Bahraini Girl anachachafya:
Hii siyo hatua nyingine ya kukinza uhuru wangu wa kujieleza kwani niko huru kusema na kuandika ninachotaka, hata yeyote hatanisikiliza. Kitu ambacho niko huru kufanya ni kuperuzi mtandao wa intaneti kama ninavyotaka, kwa kuwa mimi ni mtoto kwenye macho ya mamlaka – mtoto ambaye lazima aambiwe anachoruhusiwa na asichoruhusiwa kusoma. Na kwa kuwa hakuna anayenisikiliza, ningependa kuwashukuru watawala kwa kuzizuia tovuti zote hizo na ningependa kuwaomba waufunge mtandao mzima wa intaneti, kwani hatuna manufaa nao.
Sous, mwanamke wa Kiswidi anayeishi Bahrain, ana hasira:
HUU NI WEHU! WEHU MKUBWA!! SIWEZI KUPUMUA! HUU NI WEHU!
Suad anajiuliza:
Je maofisa hawafikirii madhara hasi yatakayotokana na uamuzi wao na umuhimu wanaozipa tovuti ambazo hazina thamani wala nafasi katika jamii. Je hawafikirii kwamba watu wengi zaidi watataka kuzifikia tovuti hizo hivi sasa kwani vyote ambavyo ni haramu hutamaniwa zaidi? Wananchi na taifa wamefaidika vipi na kufungwa kwa tovuti hizo isipokuwa kutia doa sifa ya Bahrain kwenye maendeleo ya mageuzi, kutokuwa kwake na uwazi, mabavu yake dhidi ya uhuru wa kujieleza na kurejea kwenye enzi za giza?
Mohammed Zainal yuko katika hali ya kutoamini:
Inasikitisha, na haichekeshi, makala yangu iliyopita ilihusu jinsi gani teknolojia inavyoendelea na jinsi watu wanavyoitumia ili kuendeleza matumizi mapya kila siku, wanavyobadilisha namna za kupashana habari, wakiwahamasisha watu kwa kutumia zana za mtandao [web 2.0 ++]
Je hii ndio “zama yetu ya kukutana” inavyopaswa kuwa?
MuJtAbA AlMoAmEn anafikiri kuwa kuzuiwa kwa tovuti siyo suluhisho:
Ni kweli kuwa kuna majukwaa ya kikabila mtandaoni ambayo yanapaswa kufungwa lakini ni lazima nikubali kwamba majukwaa ya kwenye mtandao yaliyo kwenye upande mwingine wa kisiasa/kidini hayakufungwa na yanaendelea kufanya kazi usiku na mchana yakirusha matusi na kutishia machafuko. Sioni manufaa yoyote ya kitaktiki yatakayotokana na kufungwa, na wakati sikubaliani na cheche za kikabila, ninakubali kwamba kinachoendela ni matokeo ya watu wa kweli walio kwenye matatizo na waliotitia kwenye ukabila. Kinachoendelea katika majukwaa ya kwenye mtandao kinaonyesha, kwa kiwango kikubwa, maoni ya walio wengi katika jamii yetu. Na suluhisho la kisiasa halipo katika mikono ya Waziri wa habari au mwingine yeyote
Hayat anahoji jinsi ya uamuzi ulivyofanywa:
Ninaamini kuwa kuzuiwa kwa tovuti ni uamuzi duni na unavunja haki ya uhuru wa kujieleza na kupata habari. Hakuna demokrasi bila ya uhuru wa kujieleza… na hakuna demokrasi ya kikatiba inayozuia tovuti… na si haki kufunga tovuti kupitia amri za kiholela za serikali ambazo hupitishwa na mamlaka ya serikali, mamlaka ya sheria na usalama wa taifa… si sahihi kwa mamlaka haya kuingiliana na kufanya kazi pamoja kama wanavyofanya… kuna utofautishaji upi kati ya matawi ya mamlaka haya?
Khalid anasema:
Ninaamini kwamba mamlaka ya sheria ndiyo mamlaka pekee yanayoweza kufanya uamuzi ama wa kufunga au kutofunga tovuti
Qassim Ahmed ana fikira:
… mamlaka ya bahrain yanataka kuzuia mtandao wa intaneti ili watu walilie kile walichozuiwa, ili kwamba wakiruhusu tena tovuti za ngono, unyama na za kuangalia filamu na tovuti vivuli pamoja na nyinginezo… watu watasema: “Uhuru umerejea tena!”
Katika ujumbe mwingine, Ammaro ameng'amua ni nini hasa kinachoendelea:
Je unakumbuka [filamu ya] matrix? Unakumbuka jinsi katika dunia yote unamoishi, ambayo uliamini ni ya kweli, ilikuwa katika ukweli halisi, ni ya kutengenezwa? Ni mauzauza tu? Hivyo ndivyo pengine mtandao wa intaneti ulivyo nchini Bahrain. Intaneti ilikuwa ni mauzauza yaliyotengenezwa na serikali ya Bahrain, ili kukufanya ufikirie kuwa ulikuwa unawasiliana na dunia iliyoko nje, wakati katika ukweli halisi ulikuwa umetengwa na kila kitu, na watu wengine wote. Kila tovuti uliyoitembelea ilitengenezwa na watu wa Wizara ya Habari; kila moja. Kuna jamaa anayeandika kwenye tovuti ya CNN, anayetunga habari za ulimwengu, na kuna jamaa mwingine anayeandika tovuti ya BBC. Ni dhahiri kuwa wanakaa pamoja wakati wanafanya hivyo; habari zinafanana sana katika tovuti hizi mbili… […] Tumekuwa tukiishi katika uongo. Tovuti za habari zinazofungwa si tovuti za kweli na ‘hazifungwi”. Ukweli ni kwamba haya ni madhara ya hali mbaya ya kiuchumi ulimwenguni, na wizara imelazimika kuwafukuza kazi idadi kubwa ya wafanyakazi kwa sababu ya upungufu wa fedha, haikuweza kuhudumia tovuti nyingi kama ilivyokuwa awali. Kwa hiyo, zimefungwa.