Wakati wanablogu kadhaa wa Kiirani (pamoja na wale wa-Kiislamu) waliongeza makala zao na jitihada nyingine za kidijitali, kama vile “Google bomb” kulaani uvamizi wa Israeli katika ukanda wa Gaza, wanablogu wengine wanasema kwamba serikali ya Irani inatumia ‘mwanya wa mgogoro wa Gaza’ kukandamiza vyombo vya habari na asasi za kiraia ndani ya nchi hiyo.
Wiki iliyopita, utawala wa Irani uliifungia Kargozaran, moja ya jarida mashuhuri la mabaliko, kwa sababu ilichapisha tamko la chama cha wanafunzi (Tahkim Vahadat) ambalo liliilaani Israeli lakini pia liligusia kundi moja la Wapalestina wenye siasa kali ambalo hujificha kwenye mahospitali na mashule, kama ni kundi la magaidi.
Nik Ahnag, bloga mashuri na mchoraji wa vikaragosi, alichora picha za vichekesho zinazohusu uvamizi wa Gaza na mizani ya nguvu zisizolingana kati ya Israeli na Palestina kwenye upande mmoja na ukandamizaji wa serikali ya Irani kwenye upande mwingine. Moja ya michoro hiyo inaonyesha nyundo kubwa yenye chapa ya Gaza ikilipiga jarida la Kargorazan. Katika mchoro huo inaonekana kwamba waalimu, wanawake na wanafunzi ndio wanaofuatia katika zoezi la kulengwa shabaha.
Mwanablogu Jamhour anaandika kuhusu tamko lililopelekea kufungwa kwa jarida hilo la mabadiliko. Anasema [Fa]:
Inawezekana kuwa mantiki ya tamko hili ni kuwa wengi wa wanasiasa wa Kiirani wanafikiri, lakini hawawezi kuthubutu kusema, kwamba mgogoro wa Gaza ni kisingizio [cha utawala wa Irani] cha kukwepa matatizo ya kiuchumi na kijamii yanayoongezeka. Leo hii inatupasa kujiuliza na kutathmini, mapambano ya mwaka jana kati ya Hamas na Fatah huko Gaza ambapo mamia ya Wapalestina waliawa na kujeruhiwa. Ghasia zilikuwa kali kiasi kwamba ziliwafanya baadhi ya waunga mkono wa Fatah wakimbilie Israeli kwa ajili ya hifadhi.
Bloga huyo anahitimisha kwamba mashambulizi ya kinyama ya Israeli pamoja na ufisadi wa baadhi ya viongozi wa Kipalestina unarutubisha makundi ya kigaidi na yale yanayochochea ghasia na chuki za kikabila na kidini.
Katika blogu ya Mibibi tunasoma [Fa]:
Kufungwa kwa Kargozaran kumewafanya watu wengi wapoteze ajira, na imekuwa vigumu zaidi [bila ya majarida yasiyo rasmi] kuwapa habari zinazohusu Gaza watu ambao hawaziamini idhaa za televisheni za serikali pamoja na tovuti zake.
Bloga Hossein Ghazian naye analalamika na kupinga uchujwaji wa habari. Bloga huyo anasema [Fa]: “Kama hatuwezi kuitetea Israeli na kuongea dhidi ya Wapalestina, maneno yangu ya kuulani uvamizi na ubabe wa Israeli yatakuwa hayana maana kadhalika hayatakuwa na uzito…”
St Behesht anaandika kuhusu “Kushindwa kwa televisheni ya Irani pamoja na kuchujwa kwa habari”. Bloga huyo anasema [Fa]:
Siku hizi, katika kila sehemu ya Irani ambako watu huongelea siasa, huongelea ugomvi wa Israeli na Hamas. Idhaa ya televisheni ya Irani inachochea mjadala huo, lakini utawala wa Irani haujagundua bado kwamba propaganda zao kwenye televisheni matokeo hasi dhidi ya Hamas. Tofauti na malengo ya televisheni ya Irani, kuna watu zaidi ya wachache ambao wanachukua upande unaoipinga Hamas na kuiunga mkono israeli…. Kwa bahati mbaya utawala wa Irani haujalielewa hili, na wanaendelea na njozi zao wakitumaini [kuwa propaganda zao] zanawashawishi Wairani.