Meksiko inakabiliwa na wimbi la uhalifu wa jinai, ambamo wote raia wa ndani na wageni wanaviziwa kutekwa nyara. Tukio la karibuni lilitokea katika Saltillo, Coahuila, wakati mtaalamu wa kuzuia utekaji nyara wa Marekani, Felix Batista alitekwa na watu waliovaa vinyafo usoni. Batista alikuwapo nchini humo kuendesha semina kama mfanyakazi wa kukodiwa wa kampuni ya usalama yenye makao huko Texas ASI Global LLC. Uzoefu wake katika nchi za Marekani ya Latini katika kupambana na uhalifu wa aina hii uantafutwa na vikundi ambavyo vina nia ya kuukwepa uhalifu huu wa jinai. Hata hivyo, kutekwa kwake kunadhihirisha kuwa kila mmoja yu hatarini.
Bloga, The Mex Files ana maswali machache ya kuuliza kuhusiana na tukio hilo:
Kama Batista ni mtaalamu imekuwaje akaruhusu atekwe yeye mwenyewe?
Batista alikuwa mfanyakazi wa “kampuni ya usalama” yenye makao huko Texas ASI Global. Imeelezwa kwamba alikuwa huko Saltillo kwa shughuli za kibinafsi, je alikuwa akimfanyia nani kazi huko?
Je kampuni ya ASI Global si moja ya kampuni za Kimarekani zinazopokea fedha kwa ajili ya “Mpango wa Merida”… Na hili linatuambia nini juu ya utendaji kazi wa wataalamu wake wa ukufunzi?
Takwimu kadhaa zinaonyesha kuwa utekaji unatokea kwa takriban mara 2 kwa siku na hasa katika majimbo ya mpakani kaskazini mwa nchi. Meksiko ina wastani wa juu zaidi wa utekaji ikilinganishwa na nchi yoyote ile duniani. Matukio haya huathiri marafiki na familia za waliotekwa, kama alivyoathirika bloga Tony Scotti, ambaye ni rafiki wa Batista:
Ninamfahamu Felix, na ni mtu anayeweza sana. Felix ana uzoefu wa zaidi ya mika 20 katika shughuli za kuokoa waliotekwa. Felix ni mtu anayejulikana, ambaye mara nyingi hunukuliwa kwenye magazeti na hata katika jarida la mwezi huu la Usalama. Kujulikana kwake kunaweza kuwa ndio kulikopelekea kutekwa kwake. Baada ya kusoma magazeti ninaweza kuhisi kwamba Felix aliwekewa mtego, na aliwekewa mtego huo na mtu anayemuamini.
Bloga El Nahual wa blogu ya Mexico Para los Mexicanos [es] anahofu kuhusu matokeo ya kitendo hiki katika nchi:
Jambo la kwanza kufanya ni kucheka. Na jambo la pili linalonijia ni woga… kama mtaalamu wa kijeshi mstaafu mwenye uzoefu wa miaka 24 katika nyanja ya usalama anaweza kutekwa, je sisi wengine tuna nafasi gani ya kusema kwamba hatuwezi kutekwa?