Malaysia: Mafunzo Yanayotokana na Mafuriko

Wiki iliyopita mafuriko yaliyakumba maeneo kadhaa katika jimbo la Sarawak nchini Malaysia. Zaidi ya watu 8000 waliokolewa wilayani Bau na kupelekwa kwenye makazi 24 ya muda mfupi. Mafuriko hayo yalikuwa mabaya zaidi katika kipindi cha miaka mitatu. Maji yalifurika na kufikia wastani wa kima cha kiuno.


Mafuriko wilayani Bau, Sarawak.Picha kutoka kwenye blogu ya Denis.

Mwanablogu a better future anaishauri serikali iorodheshe mafunzo yaliyotokana na mafuriko hayo:

“Msaada wa haraka uliendelea vizuri lakini serikali ingeweza kufanya vizuri zaidi kama wangeweka alama za maeneo yaliyofurika kwa kutumia minara ya mianzi au njia nyingine zenye vibao vinavyoeleza wazi vina vya maji. Hilo lingefanya kazi ya ufuatiliaji iwe rahisi kadhalika ingewasaidia watumiaji wa barabara kufanya maamuzi ama ya kuogelea au la. Alama hizo zingeweza kutumika wakati wa kupanga mustabali utakaoboresha barabara kuu.

“Bila ya kuwa na vielelezo sahihi ya vina vya mafuriko katika sehemu zinazoathirika mara kwa mara vitakavyosaidia mipango ya baadaye na pia utekelezaji wa miradi, tutaendelea kuwa na matatatizo yasiyo ya lazima yanayotokana na utekelezaji dhaifu wa vyombo husika.

“Ninatuamini kuwa serikali imeweza kujifunza na kwamba mafuriko yatakayotokea hapo baadaye hatakuwa na madhara, siyo tu katika wilaya ya Bau bali pia katika Sarawak yote na ikiwezekana Malaysia yote. Barabara kuu ni lazima zijengwe ili kuhimili hali yoyote ya hewa, kwa maana kwamba kiwango ambacho barabara hizo zitajengwa ni lazima kiwe ni kiwango cha kitachakowa juu ya kima chochote cha mafuriko. Vituo vya polisi na majengo muhimu ya serikali, ikiwezekana, ni lazima yawe kwenye sehemu ambazo haziathiriki na mafuriko. Kama haiwezekani, basi viwanja vitakapojengwa majengo ya serikali lazima yajazwe kifusi ili kiviinua juu ya kima cha mafuriko. Na njia za kufikia majengo hayo lazima zitengenezwe kuhimili mafuriko, ikiwezekana.”

Mwanablogu, The Lost Aborigine anawahimiza viongozi walipe kipaumbele swala la mafuriko zaidi ya maswala mengine ya mambo ya nje:

“Vipi kuhusu misaada kwa sehemu zilizoathirika hasa vijiji masikini kama vile Serian, Padawan, Bau na sehemu kama vile Sibu pamoja na Miri? Kwa nini tunashupalia mambo ya Gaza wakati watu wetu wenyewe wanakufa bila msaada? Tabia ya Wamalaysia ni ya kudharau mambo ya ndani na kushupalia mambo mengine ambayo hayahusiki moja kwa moja nasi.”

Nana Tatu naye anandika kwamba mafuriko yalikuwa mabaya zaidi katika miaka 20:

“Mto Sarawak jana ulionyesha nguvu zake wakati ulipopasua kingo zake na kumiminikia kwenye ufukwe wa Kuching. Na wakazi wa Kuching wanaeleza kwamba mafuriko haya ni mabaya zaidi katika miaka 20, yalizua foleni kubwa za magari, yalisitisha biashara na kuwajaza hofu wale waliotegemea kwamba maafa zaidi yangelitokea. Hapakuwa na maonyo ya tahadhari. Mafuriko ya mwaka huu ni zaidi ya yale yaliyotokea mwaka 2004. Pia mafuriko haya yalisababisha shule 119 zifungwe.”

Mwanablogu, Sounding Intelligent anaandika sababu zilizosababisha mafuriko:

“Sipo katika nafasi ya kueleza ni nini hasa iliyokuwa sababu ya mafuriko ya hivi karibuni lakini ninaamini kwamba mafuriko haya yalisababishwa na watu. Je ni nani aliyejenga kingo ambazo zilisababisha mito ipite kwenye mikondo myembamba? Nani aliyeharibu makonde ambayo huko nyuma yaliweza kufyonza maji ya mvua? Ni nani aliyechangia ongezeko la joto duniani?

“Ongezeko la joto ni tishio la kweli. Linaathiri mizunguko ya hali ya hewa, linaongeza kiwango cha mvua na kuyeyusha barafu kila sehemu duniani, na kusababisha maporomoko ya athari.

“Pamoja na maonyo haya, watu wengine bado wanaendelea na ubinafsi, wanakataa kuupokea mfumo wa nishati safi au kupunguza nyayo zao za gesi ya ukaa.”

Janga la mafuriko halikutokea tu Malaysia. Mafuriko pia yalizikumba sehemu mbalimbali za Phillipines, Indonesia na Fiji.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.