Angola: Ebola Inapokaribia, Mipaka yafungwa

Kutokana na kuzuka tena kwa virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, serikali ya Angola imeamua kufunga mpaka kati ya nchi hizo mbili, katika jaribio la kuzuia kuingia kwa virusi hivyo hatari katika himaya ya taifa hilo., Hivyo kusitisha mara moja uhamiaji wa kawaida unaoendelea kati ya Lunda Norte (jimbo lililoko kaskazini mashariki ya nchi) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Lazima izingatiwe kwamba jimbo la Lunda Norte ni sehemu ya migodi ya dhahabu, anyowavuta wafanyakazi wengi wahamiaji. Nelo de Carvalho [pt] anaandika katika blog do Nelo Ativado kuhusu vizingiti vilivyoko kwenye mpaka huo na changamoto ambazo serikali inazikabili:

“Kusema kwamba mpaka lazima ufungwe na kwamba mtu yeyote asiingie au kutoka nchini, kwa kutumia mpaka huo. Hakuna hata mbu anayeambukiza ugonjwa wa dengue atakayeweza kupenya, na kama akiweza kupenya, ni lazima aandamwe. Ni mkakati ambao hata mtoto inabidi autekeleze wakati akicheza mchezo wa polisi au mwanajeshi au hata jenerali. Kwa hiyo hatuna mamlaka au mamlaka ya kisheria kufikiria mara mbili juu ya hili. Tunaweza kuomba na kutumaini kwamba kila kitu kitakwenda kama tunavyotarajia. Wakati huu wa kuuanza mwaka, tunawaombea bahati nzuri Waangola wote, kuwe au kusiwe na ebola.”

Kwa mujibu wa Katibu wa Afya wa Angola, serikali inajitayarisha kuwafahamisha wananchi juu ya mpango uliowekwa ili kuzuia maambukizi ya virusi hivi vyenye nguvu. Pamoja na jimbo la Lunda Norte, hatua hizo pia zitatekelezwa katika majimbo ya Moxico, Malanje, Uige na Lunda Sul. Inaaminika kwamba kumekuwepo na kesi zipatazo 40 za ebola, na zaidi ya vifo 10 vilivyoripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika miezi miwili iliyopita.

Miaka miwili iliyopita, virusi hivyo, pia vikitokea kutokea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, hasa kutokea kwenye jimbo la Kasai Magharibi, vilisababisha vifo vya watu wapatao 180. Blogu ya Lampeirota inalalamika kuhusu hali hii:

“Mara kwa mara, huongelea kuhusu ugonjwa huu. Sina tabia ya kufikiria kuhusu jambo hili, najikinga nyuma ya dhana kwamba siyo rahisi kwa ugonjwa kunikuta nikiwa sijajiandaa.

Namna hii [ya kufikiria] ni potofu. Hatuwezi kuwa na uhakika juu ya mambo kama haya. Husambaa kila mahali kwa haraka sana.

Nawasikitikia wanaoukabili huu ugonjwa.

Siyo kifo kinachonitisha. Ni njia ya kukielekea”.

Pia kwa mujibu wa mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Angola, Diosdado Nsue-Micawg, inahisiwa kwamba ushikaji wa miili ya nyani waliokufa kwenye misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ndiyo chanzo cha kuibuka tena kwa ugonjwa huu. Japokuwa kwa bahati nzuri hapajakuwa na kesi za ugonjwa wa ebola nchini Angola, Katibu wa Afya anasema kwamba nchi hiyo imejiandaa kupambana na hali yoyote itakayojitokeza kutokana na uzoefu wake na ugonjwa wa homa na kuvuja damu wa Marbug, ugonjwa wenye hatari pungufu zaidi ya ebola.

Hii ni mara ya nne kwa virusi vya ebola kuzuka ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo tangu ulipoibuka kwa mara ya kwanza mwaka 1976. Ugonjwa unaoambukiza haraka huzua homa, kutapika, kuharisha pamoja na kutokwa damu ndani na nje ya mwili. Mnamo mwaka 2005 watu 329 walifariki kutokana na ugojwa wa Marbug kwenye jimbo la kaskazini la Uige nchini Angola, Karibu kabisa na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.


Picha ya kitaalamu ya vijidudu vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola. Picha kwa hisani ya CDC/Cynthia Goldsmith. Kupitia mtumiaji wa Flickr hukuzatuna.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.