Afrika ya Kusini: Matumizi ya Simu za Viganjani Kupambana na UKIMWI

Afrika ya Kusini imegundua silaha mpya katika vita dhidi ya VVU/UKIMWI – simu za viganjani. Kwenye mchakato mpya, jumbe za maandishi zitakuwa zikitumwa kila siku kuwahamasisha Wa-Afrika ya Kusini kwenda kupimwa na kutibiwa ugonjwa huo.

Mradi huo, unaoitwa Mradi wa Masiluleke au Project M, ulitangazwa rasmi wiki iliyopita wakati wa kongamano la Pop!Tech 2008 huko Maine, Marekani. Mradi huo umerahisishwa na mteremko unaotokana na umaarufu wa simu za viganjani nchini Afrika ya Kusini, na unatumia simu hizo za viganjani kupambana na idadi kubwa ya VVU na kifua kikuu (TB). Sehemu ya kwanza ya mradi huo itatuma takriban jumbe za bure zipatazo milioni moja kwa umma wa kawaida kila siku kwa mwaka mmoja, wakiuasa umma kwenda kwenye vituo vya VVU na kifua kikuu. Jumbe hizo zitatumwa kama sehemu ya jumbe zinazoitwa “Tafadhali Nipigie Simu”, ambayo ni aina ya ujumbe unaotumiwa sana katika Afrika.

White African anafafanua mradi huo pamoja na teknolojia yake:

“Gustav Praekelt – mmoja wa wataalamu wa simu za viganjani wenye ufahamu mkubwa – anasaidia kuendesha programu hiyo. Mradi huo unafanywa kwa kutumia nafasi ya bure ya herufi au alama 120 katika mfumo wa jumbe za “Tafadhali Nipigie Simu” unaotumika huko Afrika ya Kusini, wanaweka jumbe zitakazowafanya watu waende kutibiwa VVU kwa faragha, hivyo kutohofu doa au aibu inayoambatana na matibabu hayo.

Doa au aibu, pamoja na taarifa potofu, vinaaminika kuwa ndiyo sababu kuu zinazosababisha Wa-Afrika ya Kusini wachache mno kujitokeza kutibiwa VVU. Japokuwa takriban watu wapatao milioni 5.7 nchini Afrika ya Kusini wanaishi na VVU, kwa mujibu wa waandalizi wa mradi huo ni asilimia 5 tu ya watu wamepimwa virusi hivyo. Afrika ya Kusini pia ina idadi kubwa ya kesi za Kifua Kikuu, ugonjwa ambao unaua wengi wenye VVU.

Mradi M umeundwa ili kusaidia kupambana na magonjwa hayo mawili. Ulichipuka kutoka kwenye programu ya Pop!Tech Accelerator na umewakusanya pamoja wadau wa kimataifa, wakiwemo iTech, the Praekelt Foundation, frog design, Nokia Siemens Networks na the National Geographic Society. 3 Sheep anaeleza kwamba utumiaji wa simu za viganjani unaofanywa na mradi huu unaonyesha ni jinsi gani simu hizo zimejikita katika utamaduni wa Afrika ya Kusini, na anaongeza:

“Nchi nyingi hazina miundombinu inayotumia mtandao wa waya na zinaangalia mitandao ya simu za viganjani kama njia ya mawasiliano… huko nyuma njia nyingine za mawasiliano kama vile redio, zingetumika kufanya kazi kama hii lakini mradi huu wa Afrika ya Kusini unaonyesha umuhimu wa kuziangalia njia zote ili kuufikia umma.”

Japo huu sio mradi wa kwanza wa aina hii huko Afrika ya Kusini, waandaaji wanasema haya ni matumizi makubwa zaidi ya simu za viganjani yaliyowahi kujaribiwa ili kutuma taarifa za afya. Na mpaka sasa mradi huo una matumaini makubwa. Majaribio ya kwanza ya kampeni hii inayotumia ujumbe wa simu za viganjani ulisaidia kuongeza wastani mara tatu zaidi ya watu wanaopiga simu kwenye huduma ya simu ya UKIMWI mjini Johannersburg. Kama mradi utafaulu baada ya kuzinduliwa, kunamatumaini kwamba mradi huu utaweza kusambazwa sehemu nyingine Afrika.

Akitoa maoni katika ujumbe uliotumwa kwenye African Globalization, ahellgeth, anaamini kwamba mradi huu una matumaini makubwa.

“Utumiaji wa teknolojia ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe wenye nguvu kwa umma. Utrumiaji wa ujumbe wa simu za viganjani unatoa fursa kwa watu kuusoma ujumbe mara kwa mara, ikilinganishwa kuangalia ujumbe kwenye matangazo ya biashara au mara moja tu kwenye vipeperushi. Ujumbe kwenye simu za viganjani hukaa kwenye simu kwa siku kadhaa, hii inamruhusu mtumiaji kurejea na kuangalia ujumbe huo. Nadhani ujumbe utawafikia watu na kunasa na utawahamasisha kuchukua hatua… jumbe hizi ni sawa na matangazo kwa ya wazi kwa umma kwa kutumia simu za viganjani.”

Akiblogu katika Design in Africa, Dave anaafiki kwamba mradi huu una uwezekano wa kufanikiwa:

Ni suala muhimu linalotatuliwa, ufumbuzi rahisi na unaoeleweka umebuniwa kwa kujumuisha hazina au nguvu za wadau, na kuna manufaa yanayopimika kwa watu na jamii na gharama za kupokea ujumbe bure. Safi sana!

Akiblogu katika Wise Advice, lablady, anaona ni jambo linalosumbua kidogo kwamba teknolojia imwekwa kwenye ulingo mkuu katika vita dhidi ya VVU/UKIMWI. Anasema:

“Katika nukta au wakati gani ambapo jamii imefanya chaguo hili kuwa rahisi, na lenye uwazi na mvuto kwa watu masikini waliobanwa na janga la VVU, kwenda kununua simu za viganjani badala ya kondomu? Naliona hili ni jambo lililo kinyume, kwamba teknolojia sasa imekuwa ni chombo kinachoanzisha kampeni ambayo katika wakati mwingine, ingekuwa ni kampeni ya umma kwenye ngazi za chini kwenda kupima damu na kuelimishwa zaidi. Je dharau kwa upande wangu kuhoji kwa nini umma mzima umiliki simu za mkononi kabla ya kunufaika na mkakati wa kinga ya afya kupingana na ugonjwa unaoweza kuzuilika?”

Naye Catherine Forsythe, akiblogu kwenye DogReader, anaongeza kwamba jumbe hizi hatimaye zitaweza kuchukuliwa kama “jumbe za kero” za afya.

“Swali linaweza kuwa ‘ni kwa muda gani mbinu hii inaeweza kufanya kazi?’ Baada ya kusoma kwa mara ya kwanza, jumbe hizi za afya kwa umma zinaweza kufutwa mara moja kama vile zinavyofutwa jumbe nyingine za kero.”

Ni matumaini ya Project M kwamba haitakuwa hivyo. Awamu zijazo za mradi huu zitajumuisha usambazwaji wa vifaa vya kupimia VVU majumbani, pia uendelezwaji wa “huduma za vituo vya simu mtandaoni,” na utumiaji wa ujumbe wa maandishi wa simu za mkononi ili kutoa huduma binafsi za taarifa za afya kwa wale wanaotibiwa UKIMWI.

Picha ya Simu ya Kiganjani na JonJon2k8 kwenye Flickr.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.