Madagascar: Kuishi ughaibuni hubadili uhusiano

Katika makala iliyochapishwa mwezi Machi, wachumi William Easterly na Yaw Nyarko wanaeleza kwamba katika nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara, kiasi cha fedha kinachotumwa na wahamiaji wanaotoka bara hilo ni wastani wa asilimia 81 ya misaada ya fedha kutoka nchi za kigeni kwa kila nchi.

Dhima ya waMadagascar walio nchi za mbali kwa maendeleo ya nchi yao imewahi kujadiliwa hapo kabla katika ulimwengu wa wanablogu wa Madagascar. Hivi karibuni wanablogu walijadili athari ya kuishi ughaibuni kwa mienendo ya WaMadagascar na jinsi mabadiliko hayo yanavyoathiri uhusiano na marafiki na ndugu zao walio nyumbani.

News2dago anasimulia ni kwa namna gani alipoteza urafiki wa karibu aliokuwa na rafiki yake mmoja wa tangu enzi za shule. Anaeleza kwamba uhusiano wao ulififia polepole mara tu baada ya rafiki yake kuondoka kwenda zake Ufaransa:

Nilikuwa na uhusiano mzuri na rafiki yangu tangu tulipokuwa madarasa ya juu ya sekondari. Tuliketi dawati moja. Mara ya mwisho kumtia machoni ilikuwa mwaka 1992 wakati wa mahafali ya kumaliza elimu ya sekondari na kutunukiwa cheti. Rafiki yangu alipata bahati ya kuendelea na masomo ya juu nchini Ufaransa. Mimi nilichagua kubaki nyumbani, ulikuwa uamuzi binafsi, hakuna wa kumlaumu kwa hili. Miaka ilipita na mawasiliano na rafiki yangu, ambayo mwanzoni nilipata mara kwa mara, polepole yalianza kufifia. Siku moja nilipata taarifa kutoka kwa mtu tuliyefahamiana naye kwamba rafiki yangu yule alikuwa amekwishafunga ndoa. Niliendelea kumwandikia barua-pepe lakini pasipo kupata jibu lolote.

News2dago anaongeza kwamba yeye pia alipata fursa ya kusafiri kwenda Ufaransa mwaka 2005, lakini baada ya kutafakari vyema aliamua kubaki nyumbani. Anataja baadhi ya sababu za kufanya hivyo: udugu hupotea miongoni mwa WaMadagascar mara baada ya kufika Ufaransa, kila mmoja anakuwa na lwake, hakuna kukutana ili kucheza mchezo wa karata, pia alitumia pesa ambazo zingemuwezesha kwenda ughaibuni ili kuusimamisha mradi anaoufanya sasa. “Ni afadhali kufanya hivi kuliko kushughulika na watu walio ughaibuni na vyeti vyao vya mbwembwe vya elimu.”

Anaongeza:

Kuna kipindi nilimpigia simu ili tupige soga na kujikumbusha mambo ya zamani. Nilimwambia kwamba Mungu akipenda, huenda nitakuja huko kufanya kazi na kuwa mmoja wenu. “Kweli?” aliniuliza. Tangu nilipomweleza hayo, kila nikimpigia nakutana na ujumbe wa kunitaka kuacha ujumbe wa sauti.

Katika habari inayohusiana na hiyo, news2dago alisema kwamba mpwa wake alirejea Madagascar kutokea Ufaransa ili kufunga ndoa na Mmadagascar mwenzake aliyekutana naye ughaibuni. Walihakikisha kwamba harusi nzima imepangwa vema, hata walileta mpiga picha mtaalamu kutoka Ufaransa. Walimwomba watumie kifaa chake cha kuunganisha intaneti ili kupanga fungate lao katika eneo la Mahajanga mara baada ya harusi. Pamoja na hayo yote hawakuona ulazima wa kuaga walipokuwa wanaondoka kurudi zao Ufaransa. Ama kwa hakika kuishi ughaibuni hubadilisha watu.

Akieleza kuguswa na taarifa hiyo, Ravatorano anaamini kwamba tabia ya kujifanya kutojali au kuwapuuza marafiki wa zamani haipo tu miongoni mwa raia wa nchi moja ughaibuni. Hata hivyo, anaamini kwamba ni jambo stahiki kuonyesha heshima kwa watu waliokusaidia. Simp alidakia kishabiki: “Wasameheni kwani wao ni binadamu tu … matendo mema ndiyo mbegu za bahati njema na matendo maovu ni kama jambia la hukumu la Damocles.”

lehilahytsyresy anajaribu kutoa maelezo ya sababu kwa nini watu wanatelekeza urafiki wa kweli kwa ajili ya urafiki wa kutumiana (mg):

“Wamadagaska wanapobinywa na ukweli wa maisha ya ughaibuni,, ushindani mkali na maisha yaliyojaa madhila mengi kila siku, kwa hiyo ni jambo la kawaida kwamba mtazamo wa “ni rafiki ikiwa ni tajiri” utawale, maana mtazamo huu ni muhimu ili mtu upate kuishi. Kwa bahati mbaya, tabia hiyo huwaingia mno watu kiasi kwamba mtazamo huo huutumia hata dhidi ya ndugu zao, na hatimaye anakuwa ndugu wa kweli endapo tu ni “mtu aliye nazo”.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.