Ulimwengu wa wana-blogu wa Afrika ya Kusini umelipuka kutokana na matukio ya havi karibuni kwamba mawaziri 11 na manaibu wao 3 wamejiuzulu, mmojawapo akiwa ni mmoja wa mawaziri wa kutumainiwa kabisa nchini humo, Trevor Manuel, na Makamu wa Rais, Phumzile Mlambo-Ngcuka. Hebu fuatillia hapa chini kuhusu wanavyosema wanablogu…
Kutoka Cape Town Property Bubble…
Waziri wa Fedha Trevor Manuel ni miongoni mwa mawaziri 11 na manaibu watatu waliotangaza kujiuzulu. Barua zao za kujiuzulu zilipokelewa na Rais Thabo Mbeki “ambapo kwa masikitiko makubwa, ilimpasa kuzipokea”, ilisema taarifa kutoka Ofisi ya Rais Jumanne iliyopita.
Katika blogu yangu mwenyewe, Waiting in Transit habari ya “Serikali ya Afrika ya Kusini yaachia ngazi, nini kitafuata?” inaeleza:
“Hivi, nini kinaendelea?!?” sasa ni aina ya mshtuko unaompata karibu kila raia wa Afrika ya Kusini kutokana na taarifa zinazomiminika kila wakati zikichochewa na kujiuzulu kwa mawaziri 11 siku ya Jumanne, mmojawapo akiwa ni Trevor Manuel (Hapana! Usiachie Ngazi!) na manaibu mawaziri watatu. Waziri huyu alijiuzulu baada ya Makamu wa Rais, Phumzile Mlambo-Ngcuka, kujiuzulu siku moja kabla akisema kwamba alitaka kutoa nafasi kwa “rais mpya” kuchagua wasaidizi wake mwenyewe na “sababu binafsi” (Kwa hakika, ni kweli kabisa).
Mawaziri waliokwishajiuzulu ni pamoja na…
Makamu wa Rais, Phumzile Mlambo-Ngcuka;
Waziri wa Fedha Trevor Manuel;
Waziri wa Ulinzi Mosiuoa Lekota;
Waziri katika Ofisi ya Rais Essop Pahad;
Waziri wa Usalama wa Taifa Intelligence Ronnie Kasrils;
Waziri wa Huduma za Magereza Ngconde Balfour;
Waziri wa Biashara za Umma Alec Erwin;
Waziri wa Sayansi na Teknolojia Mosibudi Mangena;
Waziri wa Kazi Thoko Didiza;
Waziri wa Majimbo na Serikali za Mitaa Sydney Mufamadi; na
Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Geraldine Fraser-Moleketi.…orodha hiyo haijajumuisha manaibu mawaziri watatu: Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Aziz Pahad; Naibu Waziri wa Fedha Jabu Moleketi; na Naibu Waziri wa Huduma za Magereza Loretta Jacobus.
Baada ya kujiuzulu kwa Rais, ambayo peke yake lilikuwa ni pigo kubwa kwa nchi, hasa kuhusu kutengemaa kwake, n.k. sasa tunashuhudia mengine haya … Hiki ni KIMBUNGA cha aina yake. Ama kwa hakika, si ajabu kwamba Kamati Kuu ya Taifa ya ANC hivi sasa inajilaumu kwa uamuzi wake wa kumwondoa Mbeki kwenye Urais, wakitumia uamuzi wa hivi karibuni juu ya kesi iliyokuwa ikimkabili Jacob Zuma ambapo mahakama iliitupilia mbali kwa madai kwamba “ilihusishwa na mambo ya siasa” (wakimshutumu Mbeki kuhusika), naamini hawakutarajia mambo tunayoona hivi sasa, au labda walitarajia na huenda hiki ndicho walichokitaka.
Kgalemo Motlanthe, ambaye ni swahiba mkubwa wa Zuma tayari amechaguliwa kuwa Rais wa Kipindi cha mpito, hasa baada ya Makamu wa Rais kujiuzulu, maana yake ni kwamba sasa watapata fursa ya KUWEKA watu wao kwenye kila nafasi.
Sijui nini kingine kitatokea, jambo hili si zuri kwa upande wa kuinua imani ya wawekezaji nchini, haitashangaza kuona Rand inaporomoka kuliko ilivyowahi kufanya hapo kabla, maana yake tunapeperushia mbali Ndoto ya 2010. Mambo yote yamekaa vibaya, vinginevyo binafsi nafikiri ni mpaka mwujiza utokee.
Kutoka katika blogu ya Thee East Coast News Watch…
Rais Thabo Mbeki tayari amewasilisha nyaraka katika Mahakama ya Mambo ya Katiba kuomba ruhusa ili kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na Jaji Chris Nicholson.
*Hapa unaweza kusoma hotuba yake kamili ya kujiuzulu*
Mbeki aliwasilisha nyaraka hizo siku moja tu baada ya kulitangazia taifa kwamba amejiuzulu.
Hatua hiyo inafuatia tamko la Jaji Nicholson hivi karibuni katika Mahakama Kuu ya Pietermaritzburg kwamba huenda Mbeki na Waziri wa Sheria waliingilia kati katika uamuzi wa kumfikisha mahakamani Jacob Zuma. Wiki iliyopita Baraza la Mawaziri lilitamka kwamba lilikuwa likitafakari kuchukua hatua za kisheria dhidi ya tamko hilo la jaji kuhusu uingiliaji wa kisiasa. Inasemekana kwamba Baraza hilo nalo limewasilisha nyaraka katika Mahakama hiyo ya Mambo ya Katiba.
Dispatch Now anazungumzia mipango ya kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa nchini Afrika Kusini…
Mama wa Rais Thabo Mbeki anayeondoka madarakani, Epainette, anaunga mkono mipango ya kukigawa chama cha ANC na kuanzisha chama kipya cha siasa.
Taarifa za mipango ya wanaomwunga mkono Mbeki za kuunda chama kipya ziliibuka mwishoni mwa juma lililopita baada ya tamko la Kamati Kuu ya Taifa ya ANC kutangaza uamuzi wake wa kumuondoa madarakani Mbeki kutoka katika nafasi ya juu kabisa nchini humo.Waziri wa ulinzi, Mosiuoa Lekota, makamu wake Mluleki George na Gauteng Premier Mbhazima Shilowa wanasadikiwa kuongoza juhudi hizo za kupiga kampeni ili kuanzishwa kwa chama hicho kipya ambacho bado hakijapewa jina.
Mpaka Jumapili iliyopita George hakuwa tayari kuthibitisha au kukanusha tetesi kuhusu juhudi hizo, alisema tu kwamba tangazo lingetoka katika siku za hivi karibuni.
Mnamo siku ya Jumatatu, Ma'Mbeki, kama anavyojulikana nguli huyu katika medani za siasa za Afrika ya Kusini mwenye umri wa miaka 92 alisema kwamba alikuwa na taarifa kuhusu mipango hiyo na aliiunga mkono ili kukigawa chama cha ANC kwa sababu hana imani na hali ya baadaye ya chama hicho chini ya Rais Jacob Zuma.
Blogu ya The East News Watch Blog pia ilikuwa na taarifa kuhusu mtu aliyekuwa akipendekezwa na ANC kushika nafasi ya urais kabla ya mawaziri waliotajwa hapo kujiuzulu…
ANC ilikuwa imetangaza kwamba Makamu wa Rais wa chama hicho Kgalema Motlanthe alikuwa ameteuliwa na chama kushika nafasi ya Rais katika kipindi cha mpito mara baada ya kuondoka Rais Thabo Mbeki mnamo siku ya Alhamis.
Kiongozi mwandamizi wa ANC Jessie Duarte alisema kwamba ingawa Bunge lilikuwa bado kupiga kura lakini kwa hakika hiyo ilikuwa ni utaratibu tu.
“Bw Kgalema Motlanthe ndiye chaguo la ANC kuwa Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Bila shaka ataapishwa mara moja baada ya kujiuzulu kwa Rais Thabo Mbeki na kuanza majukumu yake rasmi tarehe 25 Septemba.”
Raia wengi wa Afrika ya Kusini wamegubikwa na mshtuko kutokana na matukio yanayotokea hivi sasa mbele ya macho yao, hakuna ajuaye nini kitaendelea baadaye, wengi wana mashaka na hatma ya mambo yote haya.
Picha iliyoko juu ya majumba ya Bunge la Afrika ya kusini huko Cape Town imepigwa na Nick Boalch na inatumika kupitia hati miliki za umma.