Picha za video zinatumwa kwenye mtandao wa intaneti na vyombo vya habari vya kiraia zikionyesha yale yanayojiri kuhusu mgogoro unaoibuka nchini Venezuela kati ya Wahindi wa jamii ya Yukpa wanaoishi katika milima ya Perijá, wamiliki wa ardhi na Rais Chávez. Mgogoro huu kuhusu mipaka ya ardhi umekuwapo kwa takribani miaka 30, yaani tangu pale vikosi vya jeshi vilipowandoa kwa nguvu wanajamii wenyeji ya Ki-Yukpa na kuwapa ardhi hiyo wamiliki wapya walioanzisha mashamba makubwa ya mifugo, hasa ng'ombe, ambao wameendelea kuitumia ardhi hiyo tangu wakati huo. Wahindi wa ki-Yukpa wamejaribu mara kadhaa bila mafanikio kuitwaa upya ardhi waliyoporwa, na hata Rais wa Venezuela, Hugo Chávez, alipata kutangaza miaka 10 iliyopita kwamba tatizo hilo la ardhi limalizwe, lakini mpaka sasa hakuna cha maana kilichofanywa ili kupata suluhisho la kubadili hali ya mambo.
Kwa sasa Wahindi wa ki-Yukpa wameyatwaa tena mashamba hayo makubwa, na wale wamiliki waliokuwa wakiyashikilia na ambao walitegemea nyama na uzalishaji wa mazao ya mifugo kuendesha maisha wanashindwa kuendelea na kazi zao. Hali imezidi kuwa tata kutokana na uwepo wa vikosi vya jeshi katika eneo hilo na kulitenga eneo hilo na maeneo mengine ya nchi, hali ni mbaya kiasi kwamba makundi ya Wenyeji hawawezi kutembea kwa uhuru katika ardhi yao na wakati huohuo waandishi wa habari wanazuiwa kuingia ili kuripoti kuhusu vitendo vya uvunjaji wa Haki za Binadamu, hasa vile vinavyosemekana kufanywa na wauaji wa kukodi wa Kikolumbia ambao wamekuwa wakilenga kila mtu; hivi karibuni tu walimshambulia mpaka kumuua kikongwe wa miaka 109 mwenyeji wa eneo hilo. Pamoja na vikwazo vyote hatimaye WaYukpa walifaulu kujipenyeza katika vikwazo vyote vya kuwasiliana na kuifikia jumuiya ya Machique mnamo tarehe 26 Agosti 2008, na hapo Hugo Chávez ametangaza kwamba ardhi hiyo haina budi kurejeshwa na kwamba haki za wenyeji wa eneo hilo hazina budi kuheshimiwa. Kwa kupitia blogu ya jamii ya Voces Urgentes (Sauti zenye Kuashiria Haraka), wanaibua maswali mengi kuhusiana na hatma ya mgogoro huu na suluhisho lake:
Hivi, kwa nini kuzuiwa huku kwa wenyeji kumevunjiliwa mbali sasa baada ya Chávez kutoa amri? Nini kilikuwa kikizuia taarifa za kinachoendelea kumfikia Chávez? Je, ugandamizwaji, uchokozwaji na utakatifuzwaji wa Wana-Yukpa katika kipindi chote hiki haukutosha? Je, mamlaka zimekuwa zikijibu vipi madai yasiyonyamazishika ya Wahindi wa Ki-Yukpa? Hivi kwa nini Waziri wa Mambo ya Wenyeji wa Serikali ya Watu, Nicia Maldonado, anatoa matamshi ya kuwataka Wa-Yukpa kuheshimu mali za watu binafsi na kuwataka kuishi kwa kutegemea utalii katika eneo lililojitenga na lililo kame? Je, ni nani na kwa vigezo vipi ambapo utengwaji wa maeneo ya wenyeji utafanyika?
Picha ya video iliyopandishwa mtandaoni na coritoj ni moja tu kati ya dazeni kadhaa zilizopo zinazoonyesha mateso ya jamii hii na kadiri mateso haya yanavyoanza kufahamika kwa umma mpana zaidi. Katika picha hiyo, wanajamii hii wanasimulia jinsi mmiliki mmoja wa ardhi alivyojigamba kwao kwamba alikuwa na uwezo wa kufanya chochote kwa sababu tayari viongozi walikwishapokea hongo kutoka kwake, na kwamba kamwe asingetupwa jela hata kama wangekwenda kwa Rais kwa sababu yeye anazo fedha za kutoa ili aachiwe huru:
Picha nyingine ya video iliyotumwa na ProyectoSuri inaonyesha jinsi msafara wa watoa misaada ya kibinadamu walioongozwa na taasisi ya ANMCLA walivyokuwa wakijaribu kupita katika eneo la Wa-Yukpa ili kupeleka misaada ya chakula na dawa kwa wenyeji wa eneo hilo, lakini walizuiwa kupita na maafisa wa kijeshi. Pamoja na hayo, kikosi hichohicho kilichowazuia watoa misaada ya kibinadamu kupita kilikuwa tayari kuruhusu kwa moyo radhi kabisa lori lililobeba chakula cha kulishia nguruwe kupita. Asasi za kiraia zilifaulu kumshawishi dereva wa lori hilo ‘kuona’ kwamba haikuwa haki na ilikuwa kinyume cha katiba kupeleka chakula kwa wanyama wakati ambapo chakula kilichokuwa kipelekwe kwa binadamu kilizuiwa; dereva huyu anaonekana kuelewa kwani alirudisha lori nyuma mpaka mahali kikosi cha jeshi kilipokuwa kimeweka kizuizi. Katika picha hiyo hiyo ya video, wanaonyeshwa baadhi ya Wa-Yukpa wakiwasili katika mpaka kulipowekwa kizuizi na kueleza kwamba jeshi halina haki ya kutawala jamii za wenyeji, na kwamba jamii hizo hazina budi kuongozwa na viongozi waliochaguliwa na watu, na kwamba watu wana haki ya kukaribisha yeyote wanayemtaka kuingia katika eneo lao. Pamoja na juhudi zote hizo, msafara wa watoa misaada ya kibinadamu hawakuruhusiwa kupita ili kupeleka msaada wa chakula na dawa kwa sababu kikosi cha jeshi kiling'ang'ania msimamo wake, baadhi ya watoa misaada walijeruhiwa, na watatu kati yao walikamatwa. Siku mbili
baadaye, Rais alitambua haki ya Wahindi wa Ki-Yukpa kujitawala na kurejesha ardhi yao mikononi mwao.
Dazeni za video nyingine juu ya suala hilo zinaweza kutazamwa hapa.
(Picha ya bendera ya Venezuela na Guillermo Esteves)