Binti mdogo ‘haramu’ wa umri wa kuanza elimu ya msingi huko Zhuhai, Kusini mwa Uchina, alikataliwa kujiunga na shule za eneo hilo kwa sababu tu mama yake hakuweza kulipa faini inayotozwa dhidi ya watoto wanaochukuliwa kuwa haramu, tunapata taarifa hii kutoka kwa mwanablogu wa sohu Han Tao.
“Mimi ni mtoto mwenyeji wa hapa. Mimi pia ninataka kupata elimu hii muhimu ya msingi!”
Binti huyo, Xiao Qing, akiwa amebeba bango husimama katika lango la kuingia katika Shule ya Msingi Gongbei Xiawan huku akiwa amejawa na hamu tele ya kujiunga na shule kama wanavyofanya watoto wengine wa kike na kiume. Miaka 7 iliyopita, wazazi wake walimzaa huku wakiwa bado hawajajisajili kwa ajili ya ndoa. Baadaye, baba yake aliitelekeza familia. Kwa kuwa Xiao Qing alizaliwa nje ya ndoa mama yake anapaswa kulipa faini ya yuan 9000 (sawa na dola 1321 za marekani). Anapaswa kulipa faini hiyo katika idara ya uzazi wa mpango ili kupata hati ya hukou (ambayo ni aina ya hati ya ukaazi nchini China) kwa ajili ya binti yake huko Zhuhai. Hata hivyo, mama wa binti huyu hana uwezo wa kumudu kulipa kiasi hicho cha fedha, na tayari binti yake amefikisha umri wa kwenda shule. Mama huyu amehangaika sana kwa kumpeleka binti yake katika idara zinazohusika ili kutafuta msaada. Kwa muda wa miezi miwili mfululizo walikwenda katika idara ya uzazi wa mpango, idara ya elimu, ofisi ndogo ya wilaya na hata katika serikali za mitaa, lakini hakuna msaada walioupata. Wakati muhula mpya wa masomo ulipokaribia na hatimaye kufika huku watoto wengine wa umri wake wakibeba mabegi yao mapya ya shule, Xiao Qing na mama yake walikuwa katika huzuni kubwa. Baada ya mama huyu kushindwa kushawishi mamlaka zinazohusika basi alibuni wazo jingine, aliandika kwenye karatasi “Mimi ni mtoto mwenyeji hapa. Mimi pia ninataka kupata elimu hii muhimu ya msingi!” Alimbebesha binti yake bango hilo na kumwelekeza kusimama nje ya lango la kuingia shuleni, akiwa na matumaini kwamba hatua yake hiyo ingevuta hisia za mamlaka zinazohusika na hata vyombo vya habari. “Kosa nililofanya mimi halimhusu hata kidogo mtoto wangu. Yeye ni binadamu. Kwa nini asipewe Hukou? Kwa nini asiwe na haki ya kupata elimu?” alisema mama yake Xiao Qing's.
Ningependa kuona marafiki wa mtandaoni waliosoma habari hii na picha zake wakiipiga chapa na kuiweka katika mitandao mbalimbali. Ninathamini sana jinsi mnavyojisikia juu ya hali tete inayomkabili Xiao Qing. Waandishi wetu wa habari wanafanya juhudi kubwa kuingilia kati suala hili. Nitawaletea taarifa zozote mpya zitakazojitokeza. Ikiwa unataka kuwasiliana na Xiao Qing, tafadhali nipigie. Simu yangu ni 15819497255.
Hapa chini kuna maoni ya watu mbalimbali yaliyo kwenye blogu ya Han Tao:
Mwandishi: sohu netizen aliyetuma mnamo tarehe 2008-09-23 08:26
Uzazi wa Mpango ni sera ya msingi sana nchini China na uzaaji watoto haramu unaikiuka sera hiyo. Ikiwa tutailegeza kwa ajili ya mtoto mmoja tu, basi sera hiyo haitatekelezeka. Na ikiwa itafanyika hivyo, basi watu watakabiliana na ugumu zaidi wa maisha kwani idadi ya watu itapanda juu kwa kiwango kikubwa. Tulitazame tatizo la binti huyu kwa kuzingatia picha pana zaidi, na si kwa kuangalia mtu mmoja!
Mwandishi: Guest aliyetuma mnamo tarehe 2008-09-23 08:53
Watoto ‘haramu’ nao ni binadamu, wana haki zote za msingi, hasa haki ya kupata elimu. Ikiwa hana haki hizo, je, ina maana binti huyo alizaliwa ili kuwa wa ziada? Je, tunaweza kumnyima haki zake za msingi kwa makusudi kabisa, hata haki zake za msingi za kumsaidia kuishi? Bila shaka hapana. Sasa, kwa nini haki yake ya kupata elimu imeondolewa? Aah! mfumo gani huu wa kijamii! Aah! haya ndiyo maendeleo ya binadamu tunayotaka? Hivi huu ndiyo utawala wa sheria katika nchi hii? Huu ni udhalilishaji mkubwa!
Mwandishi: Guest aliyetuma mnamo tarehe 2008-09-23 09:24
Endapo utaruhusu haki za binti huyu leo, nani ataruhusu haki za watoto wengine hapo baadaye, ikiwa ni pamoja na haki za mtoto wako? Wakati idadi ya watu huko U-China itakapokwenda juu sana, bila shaka watakuwepo watoto wengi wasio na hatia watakaopoteza haki zao!! Ingawa mtoto huyo hakufanya kosa lolote, basi walau mama yake afanye juhudi za kulipia makosa yake ya nyuma! Kwa nini mama huyu hakufanya juhudi ya kukusanya fedha ili kulipa faini inayopaswa? Kwa nini alimuachia binti yake asiye na kosa kubeba mzigo wote? Mama huyu alijitwalia mgogoro huu wa kijamii ili kutatua matatizo yake binafsi. Je, amewahi kuwaza kwamba mpango wake huu utamsababishia binti yake matatizo ya kisaikolojia? Yuan 9000 kama dola za Marekani 1318) si sawa na Yuan 90 000 (sawa na dola za Marekani 13 189). Ni kiasi ambacho angeweza kabisa kukikusanya kama angefanya juhudi zaidi, au siyo? Je, kitendo chake hiki kweli kinaonyesha kwamba yeye anastahili kuwa mama wa binti huyu ikiwa hivi ndivyo anavyomtumia?
Mwandishi: Guest aliyetuma mnamo tarehe 2008-09-23 10:19
Hakuna anayependa kuzaa nje ya ndoa, hasa mwanamke. Bila shaka kuna jambo ambalo halisemeki lililomlazimisha mama huyu kuingia katika hali hii ngumu. Mama asiye na mume ana mambo mazito ya kupambana nayo na hasa katika kulea mtoto wake, kwa hiyo anachohitaji kwa sasa ni msaada. Zaidi ya hilo, uanaharamu hauendani na sera ya mtoto mmoja. Imewekwa hivyo ili tu kuyafanya maisha yao yawe magumu.
Mwandishi: Tea-lover aliyetuma mnamo tarehe 2008-09-24 01:35
Kuzaa ni haki ya kawaida ya kuzaliwa ya kila mwanamke. Tokea mwanzo haikuwa sahihi kwa mfumo tulio nao kwani unaigandamiza haki hiyo. Hata hivyo, tayari msichana ameshaingia duniani, katika mfumo wa kijamii wa Uchina, ama kwa hakika yeye ni kosa chini ya mfumo wa sheria unaotawala nchini humu. Lakini nataka kuwauliza wale waliotoa maneno yasiyofaa iwapo kuingia katika penzi, ambayo ni hali ya kibinadamu, ni jambo lisilofaa. Katika jamii hii iliyojifungafunga kama dubwasha fulani, watu wa koo za kitawala na wenye nazo wanaruhusiwa kuwa na watoto idadi wapendayo, kwa sababu tu wao ni matajiri. Je, hii ina maana kwamba sheria ipo ili kuwabana maskini na papo hapo kuwasafishia njia matajiri? Ni laana iliyoje hii! Ikiwa sheria inatofautiana kutoka mtu hadi mtu, basi ni kana kwamba hakuna sheria! Watoto hawana hatia. Watu ndiyo kiini na mizizi ya nchi, na ni utashi wa binadamu ndiyo unaotoa
mwelekeo sahihi. Mfumo wowote ule unapaswa kwanza kabisa kujali haki za binadamu.
Mwandishi: Guest aliyetuma mnamo tarehe 2008-09-24 09:49
Kwa kusema ukweli mfumo wa hukou haukuwa sahihi tangia mwanzo. Mara tu mtoto anapozaliwa basi anakuwa na haki ya kuishi, ambayo ni moja kati ya haki za msingi za binadamu. Je, mtu huyu atatoweka eti kwa sababu hakupata hukou? Mfumo huu utaishia tu kuwafanya wale waliotendewa vibaya kuichukia jamii. Matokeo yake ni kwamba huenda jamii itajikuta ikilipa gharama zaidi hapo baadaye. Je, tunawezaje kutarajia kuunda jamii iliyoshikamana kutokana na mtindo huu? Hivi, kwa nini serikali isiwatendee watu wake vema zaidi na kwa namna ya kuwastahimili?