- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Nia ya Mwanablogu Mmoja Kumsaidia Mtoto Kamba huko Madagaska

Mada za Habari: Popular Post, First Post!, One month, Two Posts, Three months, Five Posts, Six months, Ten Posts, One year, Two years, Twenty-five Posts, Fifty Posts, Five years, Seventy-five Posts, One Hundred Posts, Ten years, Madagaska, Harakati za Mtandaoni, Uandishi wa Habari za Kiraia, Sauti Chipukizi

Ikiwa unataka kwenda sambamba na habari mpya mpya kutoka Madagaska, inawezekana kabisa ukawa ni msomaji wa Madagascar Tribune [1]. Na kama wewe ni mdau wa gazeti hilo, hivi karibuni yawezekana ulishakutana na habari [2]iliyoandikwa na mwandishi wa habari Herimanda R kuhusu upasuaji wa maradhi ya nadra na mafanikio yake ambao ulifanyika katika kitengo cha tabibu za mishipa ya fahamu cha Hospitali ya Ravoahangi mnamo tarehe 10 Juni. Mtoto wa mwaka mmoja Tombotsara Ambinindrazana, ambaye milele atajulikana kwa jina la “mtoto Kamba” ndani ya jamii ya wanablogu duniani, alizaliwa na hitilafu nadra sana katika sehemu ya mbele ya viungo vya pua meningoencephalitis [3], hitilafu iliyosababisha uvimbe mkubwa kujitokeza kwenye paji lake la uso, kama inavyoonekana pichani:

Makala [4] kutoka katika jarida la Midi Madagasikara inadokeza kwamba ni kesi 37 tu ambazo zimeshawahi kutokea katika hospitali ya Ravoahangy. Lakini jambo ambalo makala zote hazikulielezea ni la mazingira ya kusisimua yanayoambatana na habari hii [5]ya kijana mwanablogu pinduani mwenye umri wa miaka 18, Diana Chamia, ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kuelimisha umma juu ya hali ya mtoto kamba katika ujumbe wa blogu yake aliouita “Nisaidieni ili niwasaidie wengine [6]


Diana Chamina pichani, akiwa na mtoto Kamba kabla ya upasuliwaji ambao ulifanikishwa kwa juhudi za Diana.

Diana [7], kijana mwanafunzi wa uandishi wa habari huko Mahajanga, Madagaska, alijifunza kublogu katika warsha ya uandishi wa kiraia [8]iliyoandaliwa na Foko Madagascar [9], asasi iliyofadhiliwa na mradi wa Sauti Zinazoinukia (Rising Voices). Wanblogu wengine kutoka mahajanga ni Cylnice [10], Jombilo [11], Lomelle [12], Mielmanja [13], Rondro [14], Tonkataly [15], Ysiastella [16] pamoja na Zouboon [17].


Mabloga kutoka kilabu cha kublogu cha Foko huko Mahajanga, wakiwa na Diana alivalia nyeusi katikati.

Lakini ni Diana ndiye aliamua kuitumia blogu yake kama ulingo wa harakati za kijamii. Kama navyoeleza katika ujumbe wake wa tarehe 19 mwezi wa nne [18], Diana alikutana na mtoto kamba na mama yake, Philomène Georgine, baada ya kupitiliza kituo chake cha basi cha kawaida baada ya kupitiwa na mawazo.

Nilipanda basi nambari 5 kutokea nyumbani kuelekea soko la Mahabibo, lakini nilikuwa nimejawa mawazo au pengine ilikuwa ni hatima tu ya kukutana na huyu mtoto. Nilipitiliza kituo. Tulikuwa tayari katika kituo cha jengo la jiji ndipo nilipogundua nimekosea. Wakati nikirudi kuelekea sokoni, nikamuona huyu mama aliyekuwa amebeba mtoto mgongoni, na mwingine mikononi na mfuko mkubwa mwekundo begani. Huyu aliyekuwa mbele alikuwa amezibwa na na sari ya kijani. (Nikajiuliza inakuwaje anamsitiri mtoto namna ile katika hali ya hewa ya joto kali la Majunga). Upepo ulipopiga ukaonyesha sura ya mtoto.

Diana anaendelea kuelezea maongezi yake na Philomène, ambaye, pamoja na jitihada zote, hakuwa amefanikiwa kupata msaada kwa ajili ya upasuaji ili kuondoa uvimbe ule mkubwa uliokuwa kwenye paji la uso la mwanawe. Siku ile ile Diana alijiwekea nadhiri kwamba atafanya jitihada zitakazomuwezesha Kamba kupasuliwa ili naye apate makuuzi kama watoto wengine bila ya kutupiwatupiwa macho na wapita njia, hali ambayo mama yake alikwishaizowea.

Kwa miezi michache iliyofuatia Diana aliwahamasisha wanblogu wenzie ili wamsaidie katika wito wake. Kundi zima la mradi wa kublogu wa Foko wakaitikia wito na kumsaidia Diana kuanzisha Zaza sy Vavy Gasy [19](“Kwa mama wa Ki-Malagasy na mwanawe”) , tovuti ya lugha mbili yenye lengo la kuongeza misaada na ufadhili kwa ajili ya upasuaji aghali utakaoondoa uvimbe kwenye paji la uso la Kamba. Kadhalika ukurasa wa Facebook pia ulianzishwa [20].

Kampeni hiyo ndefu ya Diana imeandikwa na kuorodheshwa vyema na mratibu wa mradi wa Foko, Joan Razafimaharo, kwanza katika blogu yake binafsi [21], na pia katika blogu ya jumuiya ya kitaifa ya wanablogu Malagasy Miray [18].

Wakati huo huo huko nchini Kanada, Jean Razafindambo, mtaalamu muhamiaji wa Ki-Malagasy mwenye mizizi imara huko Mahajanga alikuwa akiperuzi kwenye mtandao wa intaneti siku hiyo ambayo mjukuu wake wa kiume alikuwa amezaliwa, na ndiyo alipokumbana na blogu ya Diana. Kama Razafindambo alivyolieleza jarida la the Ottawa Citizen [22], “Nilimfikiria mjukuu wangu, alikuwa ni mwenye afya, na kama (Kamba) angalikuwa mjukuu wangu, ningefanya nini?” Kwa msaada wa wafanyakazi wenzake na watu baki, Jean na mkewe baku walichangisha karibu ya dola 1500 kwa kukimbia nusu-mbio ndefu za mji wa Ottawa ajili ya matibabu ya Kamba mnamo mwezi wa tano.


Mtoto Kamba akipona vizuri.

Kama unavyoona pichani hapo juu, mtoto kmaba anapona vilivyo ikizingatiwa kuwa upasuaji wake ulikuwa nyeti (ulichukua zaidi ya masaa 8). Upasuaji ule usingewezekana kutokea ghairi ya moyo mwema na jitihada zisizokoma za Diana. Ni mara ngapi tunawapita watu wanaohitaji msaada na kuilaumu tu serikali kwa kutotoa huduma nzuri za afya na makazi? Ikesha tunatembea mbele. Lakini Diana hakupita. Bila silaha nyingine zaidi ya blogu na nia yake, ameweza kubadilisha milele maisha ya mtoto ambaye amejulikana duniani kama mtoto kamba. Unaweza kusikiliza moja kwa moja kutoka kwa mama yake Kamba, Philomene na kutoka kwa Diana mwenyewe katika filamu ifuatayo yenye vielelezo katika kiingereza.